TANZANIA KUANZISHA KIWANDA CHA CHANJO YA CORONA

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

Serikali imeanza mchakato wa kutengeneza chanjo ya Virusi vya Corona hapa nchini ili kupunguza gharama ya kuagiza nje ya nchi na kuzifanya ziwe karibu na wananchi.
Akizungumza na waandishi wa Habari leo jijini Dodoma Katibu Mkuu, Wizara ya Afya- Idara Kuu ya Afya Prof. Abel Makubi amesema kiwanda hicho hakitatengeneza chanjo ya UVIKO tu bali na magonjwa mengine.

"Wataalamu tunao wengi na kiwanda hicho hakitatengeneza chanjo ya UVIKO 19 pekee, hata ikiisha tutaendelea kuzalisha chanjo nchini,"amesema Prof. Makubi.

Aidha, Prof. Makubi amesema Serikali haina mpango wa kuwauzia wananchi chanjo ya ugonjwa UVIKO 19 wala kuruhusu mtu yeyote kuingiza chanjo hiyo kinyume na utaratibu utakaowekwa.

Wakati huo huo, Prof. Makubi aliyeambatana na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Carolyne Nombo amewataka viongozi na wasimamizi wa shule kuzingatia mwongozo wa kudhibiti ugonjwa wa UVIKO 19 ili kujikinga bila kuathiri shughuli za kijamii na kiuchumi.

Amesema wakati shule na baadhi ya taasisi za vyuo zinatarajiwa kufunguliwa hapo kesho, mwongozo utakaotumika ni ule ule uliotumika mwaka jana na umepitiwa upya ili kuendana na mahitaji ya sasa.

Prof. Makubi amesema, Serikali inalazimika kuwakumbusha viongozi wa shule na Taasisi za Elimu kuimarisha mifumo ya malezi kwenye mabweni, kufanya ukaguzi na ufuatiliaji wa mara kwa mara kuhusu afya za wanafunzi.

"Mambo muhimu ni viongozi wa shule na vyuo kuandaa miundombinu ya maji na upatikanaji wa barakoa kama ilivyokuwa mwaka jana na kuchukua hatua stahiki iwapo kutagundulika kuna maambukizi bila hofu wala taharuki," alisisitiza Prof. Makubi.

Aidha, Prof. Makubi amesisitiza elimu ya kujikinga na ugonjwa huo iendelee kutolewa kwenye maeneo mbalimbali hasa nyumba za ibada, shuleni na vyuoni.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu Elimu Prof. Carolyne amesema Wizara kwa kushirikiana na Tamisemi itasimamia miongozo hiyo iliyotolewa na Wizara ya Afya.

"Miundombinu yote ifufuliwe ikiwemo matumizi ya vitakasa mikono, barakoa asilia na maji yanayotiririka," amesisitiza.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news