Na Mwandishi Wetu, Morogoro
MKUU wa Wilaya ya Morogoro, Albert Msando akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Morogoro katika hitimisho la uzinduzi wa progamu yaraConnect amesema uzinduzi huo umekuja wakati muafaka mkoani humo kwani kwa sasa wapo mbioni kuanzisha mpango uitwao ‘Moro Digital’ wenye lengo la kuhakikisha mkoa unatoa huduma zote muhimu kwa wananchi kwa njia ya kidigitali.
Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Albert Msando (kushoto) akimsikiliza Meneja Masuluhisho ya Kidigitali wa kampuni ya mbolea ya Yara Tanzania, Deodath Mtei (wa pili kulia), alipokwenda kuzindua programu ya yaraConnect mjini Morogoro. Kushoto kwake ni Bwanashamba Mwandamizi wa Yara, Maulidi Mkima, Bwanashamba Mauzo mkoa wa Morogoro, Andrew Mwangomile na Meneja Biashara wa Yara Kanda ya Kusini, Andrew Ndundulu.
Akizungumza mjini humo amesema, Yara imewatangulia hatua moja mbele, akawapongeza kwa maono hayo kwa kupiga hatua kwa haraka huku wengine wakichelewa.
“Ni imani yetu sisi kama mkoa hatua hii mliyoichukua itaenda kuwasaidia wafanyabiasha, mawakala na wasambazaji wa pembejeo, na kwa kusaidika kwao wataenda kutoa huduma kwa ubora na mkulima atafaidika,”amesema.
Meneja Masoko wa kampuni ya mbolea ya Yara Tanzania, Sheila Chatto (kulia) akizungumza katika uzinduzi wa programu ya yaraConnect kwa Mkoa wa Morogoro.
Pamoja na hayo amesema ni imani yake data na taarifa zote watakazozikusanya na kuziweka ndani ya programu hiyo zitawasaidia katika kuboresha sera na sheria zao za kilimo na ziwekwe katika mfumo wezeshi kwa serikali kuzipata ili ijue ni hatua zipi za kisera ama kisheria zinapaswa kuchukuliwa katika kumsaidia wakala na mkulima kwa ujumla wao.
“Taarifa ni muhimu sana katika sekta ya kilimo, husaidia kufanya maamuzi kwa haraka zaidi, ukiwa na taarifa sahihi unajua ni mpango au hatua gani uchukue katika kurekebisha au kuboresha huduma unayotoa, nisisitize kuwa wakati mnaendelea kuboresha App hii basi mhakikishe mnatushirikisha taarifa zote muhimu ziweze kutusaidia kwa pamoja.
Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Albert Msando (kulia) akizungumza na wauzaji pamoja na wadau wa mbolea ya Yara mjini Morogoro wakati wa Uzinduzi wa Programu ya yaraConnect inayowezesha upatikanaji wa elimu ya utaalamu wa kilimo. Kutoka kushoto ni Bwanashamba Mwandamizi wa kampuni ya mbolea ya Yara Tanzania, Maulidi Mkima na Meneja Masuluhisho ya Kidigitali wa Yara, Deodath Mtei.
“Sisi kama Serikali tunaita makampuni mengine zaidi ya kuzalisha mbolea humu ndani kwa kuwawekea mazingira bora ya kufanya biashara, najua ninyi ni wasambazaji wa mbolea kutoka nje, ni matumaini yangu tunaweza kukaa pamoja na kuona ni jinsi gani ya kufanya biashara kwa manufaa ya wasambazaji wenu na wananchi,”amesema mkuu huyo wa wilaya.
Akizungumzia uzinduzi wa programu ya yaraConnect yenye malengo ya kutoa elimu ya kilimo kidigitali, Meneja Masuluhisho ya Kidigitali wa Yara, Deodath Mtei amesema, umepokelewa kwa muitikio mkubwa na wadau wa sekta ya kilimo katika mikoa yote saba nchini kulikofanyika uzinduzi huo huku zaidi ya wauzaji rejareja 350 wakiwafikia.
“Sababu kubwa iliyotufanya tuanzishe programu hii na kuilekeza kwa wauzaji wa rejareja ni ukweli kuwa wao ndio wa mwisho kabisa wanaokutana na watumiaji wa bidhaa zetu ambao ni wakulima na hivyo ni rahisi kwao kufikisha elimu hiyo kwao kwa urahisi,”amesema.
Meneja Masuluhisho ya Kidigitali wa kampuni ya mbolea ya Yara Tanzania, Deodath Mtei, akifafanua hoja mbalimbali katika uzinduzi wa programu ya yaraConnect kwa Mkoa wa Morogoro.
Meneja huyo ameongeza kuwa, licha ya muitikio huo mkubwa. lakini pia waliweza kupata mrejesho kutoka kwa wauzaji hao na pia kukutana na changamoto ambazo kwa namna moja ama nyingine zitawasaidia katika kuchukua hatua ya kuzipatia ufumbuzi.
Moja ya changamoto amesema ni upatikanaji wa mtandao wa intaneti kwani ufanyaji kazi wa programu hiyo unategemea upatikanaji wa mtandao wa intaneti.
“Tutashirikiana na Serikali na wizara zake ili kulipatia tatizo hili ufumbuzi, sisi Yara kama kampuni tutafanya jitihada zote ili kuona changamoto hizi zinapatiwa ufumbuzi,"amesema.
Aidha, Mtei aliongeza kuwa katika maeneo kadhaa waliyozindua programu ya yaraConnect baadhi ya wauzaji walitaja changamoto ya ujazo wa mifuko ya mbolea na mfumuko wa bei kuwa moja ya sababu inayoathiri biashara zao.
Meneja Biashara wa Yara Kanda ya Kusini, Andrew Ndundulu ( kulia), akizungumza na wauzaji pamoja na wadau wa mbolea ya Yara jijini Morogoro wakati wa Uzinduzi wa programu ya Yaraconnect inayowezesha upatikanaji wa elimu ya utaalamu wa kilimo. Kutoka kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Albert Msando, Bwanashamba Mwandamizi wa kampuni ya mbolea ya Yara Tanzania, Maulidi Mkima na Meneja Masuluhisho ya Kidigitali wa Yara, Deodath Mtei.
“Ni kweli suala la mfumuko wa bei kwa ujumla kwa sasa hapa nchini unaathiri bidhaa zote za pembejeo za kilimo, na hii nikimaanisha kuwa sio pembejeo za Yara peke yake, ni matumaini yangu mamlaka husika inashughulikia suala hili ili kuona ni jinsi gani ya kulipatia ufumbuzi.
“Kuhusu ujazo, kama Yara tutaangalia uwezekano wa kuwa na ujazo wa kilo mbili au tano ili kuwawezesha wakulima wadogo wadogo wawe na uwezo wa kumudu gharama za manunuzi.
“Yara ipo kwa ajili yao, na kwa wauzaji wetu waendelee kutumia programu hii wale ambao hawajajisajili wajisajili ili kupata mafunzo ya utaalamu wa pembejeo zetu na kilimo kwa ujumla na pia kujikusanyia pointi zitakazowawezesha kupata zawadi kutoka Yara,”amesema meneja huyo.
Mmoja wa wauzaji wa pembejeo za kilimo za Yara wa mjini Morogoro, akishukuru kampuni ya mbolea ya Yara Tanzania kwa kuwaletea programu ya yaraConnect baada ya kuzinduliwa mjini humo.
Naye mmoja wa wauzaji rejareja wa mbolea ya Yara kutoka Kilosa, Robert Mashaka naye kama wenzake alitoa changamoto kwa Yara kuona namna ya kuwa na mifuko yenye ujazo mdogo akisema wateja wao wengi ni wakulima wadogo hivyo itawapa unafuu wa kumudu gharama za manunuzi.
Uzinduzi wa yaraConnect wa Kampuni ya kusambaza mbole ya Yara umefanyika katika mikoa saba ya Kilimanjaro, Arusha, Tabora, Iringa, Njombe, Mbeya na Morogoro.
Tags
Habari