Waaswa kutoficha wahalifu

Na Abubakari Akida,MOHA

Wananchi wa kijiji cha Paris kilichopo Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja Visiwani Zanzibar wametakiwa kutowaficha wahalifu wanaopatikana katika maeneo yao ili kuweza kuishi kwa amani na salama ili lengo la nchi kuendelea kiuchumi litimie.
Hayo yamesemwa leo na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Khamis Hamza Chilo wakati akizungumza na wananchi wa kijiji hicho kwenye mkutano wa hadhara ambapo kabla ajazungumza nao alipata nafasi ya kusikiliza maoni mbalimbali kutoka kwa wananchi hao.

Amewataka wananchi hao kutoyafumbia macho matendo ya uhalifu ikiwemo uuzaji na utumiaji wa dawa za kulevya,matendo ya udhalilishaji,uporaji na wizi.

“Kuna wengine wamesema yapo matukio ya kihalifu hapa yanafanyika, watu wanaiba hapa, watu wanatembea uchi, bangi zinauzwa hapa, sasa akitokea mtu anatokea sehemu ya mbali kama mlivyosema anafanya matendo ya uhalifu basi mripoti kwa Jeshi la Polisi,mkishajua huyu ndio muuza unga maarufu hata mimi niambieni nitawatauma askari wangu waje wamshughulikie,msimpige wala msichukue sheria mkononi chukueni hatua za kinidhamu na kisheria sio mumpige mtakuja kutengeneza balaa lingine,” amesema Naibu Waziri Chilo.

Awali mkazi wa kijiji hicho, Said Mpangaleni akizungumza katika mkutano huo amesema kuwepo kwa uhalifu uliokithiri katika Kijiji chao imepelekea kudumaa kwa shughuli za kimaendeleo watu wakihofia usalama wao

“Hapa pana genge la uuzaji na utumiaji dawa za kulevya na ndio linaratibu uhalifu wote katika kijiji hiki,mtu akishakula maunga yake kinachofuatia ni uhalifu tu kwa kweli tumekua tukiishi kwa hofu,bora sisi wanaume tuna afadhali lakini dada zetu wanaporwa mchana kweupe,serikali itusaidie kwenye hili kwani kwa hali hii huo uchumi tunaoambiwa hatuwezi kuupata hali huku ni tete,"amesema Said.

Wakitoa neno la shukrani baada ya mkutano huo wawakilishi wa wananchi hao wameiomba serikali kufungua kituo cha polisi katika maeneo hayo kwani itarahisisha udhibiti wa uhalifu katika Kijiji chao hali itakayopelekea kustawi kwa amani huku pia wakiomba kuongezwa kwa askari wa ulinzi shirikishi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news