Na Lusungu Helela, WMU
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt.Damas Ndumbaro amezitaka Halmashauri zote nchini ambazo zinapakana na maeneo ya Hifadhi kupanga matumizi bora ya ardhi huku akiwataka Wananchi kuacha kulima na kuanzisha makazi kwenye mapito ya wanyamapori.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt.Damas Ndumbaro akisalimiana na Mzee Maarufu, Elia Laizer akiwa na Mbunge wa Monduli Fredrick Lowassa ( katikati) mara baada ya kuzungumza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika kata ya Makuyuni katika kijiji cha Makuyuni Juu mkoani Arusha ambapo amewataka Wananchi wa Kijiji hicho kutoa taarifa kwa Maafisa Wanyamapori pindi wanapowaona wanyamapori wakali na waharibifu wakiwemo tembo baadala ya kuanza kuwarushia mawe hali inayopelekea tembo kuleta athari kwa binadamu.
Aidha, Waziri Dkt.Ndumbaro ameendelea kusisitiza kuwa Wananchi wanatakiwa kuheshimu maeneo ya Hifadhi huku akisisItiza kuwa idadi ya tembo haijaongezeka kama inavyodaiwa baadala yake idadi ya watu ndio imeongezeka
Amesema kwa mujibu wa takwimu mwaka 1961 wakati nchi inavyopata uhuru idadi ya watu ilikuwa milioni nane huku idadi ya tembo nchi nzima ilikuwa 300,000 ambapo kwa sasa idadi ya watu imeongezeka hadi kufikia milioni 62 huku idadi ya tembo imepungua hadi kufikia 60,000
Akizungumza leo katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye kata ya Makuyuni katika Kijiji cha Makuyuni Juu mkoani Arusha, aliwataka wananchi wa kijiji hicho kuacha kulima na kujenga makazi yao kwenye njia za wanyamapori (shoroba) ili kuondokana na adha wanayopata kutoka kwa wanyamapori
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt.Damas Ndumbaro ( kushoto) akiwa kwenye picha ya pamoja na Mbunge wa Monduli Fredrick Lowassa wakifurahia jambo mara baada ya kupewa heshima na kabila la Kimasai mara baada ya kufanya mkutano wa hadhara katika kijiji cha Makuyuni Juu kilichopo mkoani Arusha ambapo amewataka Wananchi wa Kijiji hicho kutoa taarifa kwa Maafisa Wanyamapori pindi wanapowaona wanyamapori wakali na waharibifu akiwemo tembo baadala ya kuanza kuwarushia mawe hali inayopelekea tembo kuleta athari kwa binadamu.
Alisema kuongezeka kwa matukio ya watu kuvamiwa na wanyamapori wakali na waharibifu hakutokani na idadi ya tembo kuongezeka bali kunachangiwa na idadi ya watu kuongezeka na kuanza kulima na kuanzisha makazi karibu kabisa na maeneo ya Hifadhi pamoja na kuziba njia za wanyamapori
Kufuatia hali hiyo, Dkt.Ndumbaro alisema Serikali itaendelea kutoa elimu ya kujihami na wanyama wakali na waharibifu katika maeneo yote yanayovamiwa na wanyamapori hao huku akisema suluhisho la kudumu kwa wananchi wa maeneo yote nchini ikiwemo Kata ya Makuyuni ni kuacha kulima na kujenga kwenye mapito ya wanyamapori na badala yake maeneo hayo wayatumie kwa ajili ya kulishia mifugo.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt.Damas Ndumbaro akikabidhiwa fimbo maalum na Mzee wa kabila wa Kimasai, Olotaika Ole Kisasalawe huku akishuhudiwa na Viongozi wa Kimila wa kabila hilo mara baada ya kuvishwa vazi heshima na kabila hilo ikiwa ni zawadi ya kumshukuru mara baada ya kufanya ziara ya kikazi katika kijiji cha Makuyuni Juu kilichopo mkoani Arusha ambapo amewataka Wananchi wa Kijiji hicho kutoa taarifa kwa Maafisa Wanyamapori pindi wanapowaona wanyamapori wakali na waharibifu akiwemo tembo baadala ya kuanza kuwarushia mawe hali inayopelekea tembo kuleta athari kwa binadamu
Akizungumza katika mkutano huo, Dkt.Ndumbaro amewataka wakazi wa Kata ya Makuyuni pindi wanapoona makundi makubwa ya tembo kuacha kuwafukuza kwa kuwapiga mawe badala yake watoe taarifa kwa Maafisa Wanyamapori ili wafike kwa ajili ya kutoa msaada wa kitaalamu wa kuwaondoa tembo hao bila kusababisha madhara kwa binadamu.
"Serikali haipendi kuona wananchi wanajeruhiwa na wengine wanapoteza maisha yao kwa ajili ya wanyamapori ilhali jukumu la Serikali ni kulinda mali na maisha ya wananchi wake, toeni taarifa acheni kupambana wenyewe hamtaweza, " alisisitiza Dkt.Ndumbaro.
Katika hatua nyingine, Dkt.Ndumbaro aliwaeleza wananchi hao kuwa Serikali imekuwa ikitoa kifuta jasho na kifuta machozi kama kanuni zinavyoelekeza kwa wale wote walioathiriwa na wanyamapori wakali na waharibifu na sio fidia kwani uhai wa binadamu una thamani kubwa na hakuna fidia itakayoweza kuwa mbadala wa maisha ya binadamu.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt.Damas Ndumbaro akizungumza na wananchi wa kata ya Makuyuni katika kijiji cha Makuyuni Juu kilichopo mkoani Arusha ambapo amewataka Wananchi wa Kijiji hicho kutoa taarifa kwa Maafisa Wanyamapori pindi wanapowaona wanyamapori wakali na waharibifu akiwemo tembo baadala ya kuanza kuwarushia mawe hali inayopelekea tembo kuleta athari kwa binadamu.
"Sisi kama Serikali tumekuwa tukitoa pole kwa wale walioathiriwa na wanyama hao ikiwa ni utamaduni wa kuonesha kuwa tumeguswa na jinsi wanyamapori hao walivyosababisha hasara ila hiyo sio fidia" alisisitiza Dkt.Ndumbaro.
Katika hatua nyingine, Dkt Ndumbaro ameshidi kulifanyia kazi suala la kuchelewa kwa vifuta jasho na vifuta machozi huku akiwataka wananchi pindi wanapovamiwa na wanyamapori hao kufuata taratibu zinazotakiwa ili madai yao yaweze kufika wizarani kwa ajili ya kufanyiwa kazi kwa muda muafaka.
Tags
Habari