NA MWANDISHI DIRAMAKINI
Robert Manunba ambaye aliwahi kuwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai nchini (DCI) amefariki akiwa na umri wa miaka 68.
Kifo chake kimeripotiwa usiku wa Agosti 30,2021 katika Hospitali ya Taifa Muhimbili iliyopo mkoani Dar es Salaam alipokuwa akipatiwa matibabu.
Binti yake ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma, Rose Manumba amethibitisha kifo cha baba yake kupitia akaunti yake ya mtandao wa kijamii wa Instagram leo Jumanne Agosti 31, 2021.
DCI Manumba alijiunga na Jeshi la Polisiolisi mwaka 1976 na kulitumikia kwa miaka 37 hadi alipostaafu mwaka 2013.
Katika utumishi wake amefanya kazi mbalimbali ikiwemo afisa upelelezi wa chumba cha mashtaka (1976 – 1977), Mwendesha mashtaka wilaya ya Kibondo na Kasulu (1977 – 1984).
Pia Mkufunzi wa Chuo cha Polisi Dar es salaam (1984 – 1987), Mkuu wa Upelelezi wilaya ya Kinondoni (1987 - 1990), na Kaimu Mkuu wa upelelezi Mkoa wa Dar es salaam (1990 – 1993).
Pia, amewahi kuwa Mkuu wa upelelezi (RCO) wa mkoa wa Arusha ( 1993 – 1995), Mkufunzi mkuu wa Chuo cha Polisi Moshi (1995 – 1996), Mkuu wa kitengo cha makosa ya kughushi (1996 – 1997).
Mkuu wa kitengo cha usalama wa nchi, intelijensia na madawa ya kulevya (1997 – 2001), kabla ya kuteuliwa na Rais Hayati Benjamin Mkapa mwaka 2001 kuwa Naibu Mkurugenzi wa upelelezi wa makosa ya jinai akimsaidia aliyekuwa DCI wa wakati huo Adadi Rajab.
Mwaka 2006 Rais Rais wa Awamu ya Nne, Dkt.Jakaya Kikwete alitengua uteuzi wa DCI Adadi Rajab na kumteua kuwa Balozi wa Tanzania nchini Zimbabwe.
Aidha,alimpandisha Manumba kuwa Mkurugenzi mpya wa upelelezi wa makosa ya jinai ambapo aliifanya kazi hiyo kuanzia mwaka 2006 hadi 2013 alipostaafu.