NA MWANDISHI DIRAMAKINI,Dar
Aliyewahi kuwa Mkurugenzi wa Tume ya Jiji la Dar es Salaam, Mbunge wa Ubungo na Waziri kipindi cha Serikali ya Awamu ya Tatu, Mheshimiwa Charles Ndiliana Ruwa Keenja amefariki Dunia leo Agosti 5,2021.
Ni wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Seifee iliyopo jijini Dar es Salaam.
Pia taarifa za awali zimemdokeza Mwandishi Diramakini kuwa, marehemu Keenja ambaye alizaliwa Desemba 24, 1940 wametwaliwa pamoja na mkewe.
Msemaji wa familia, Bariki Keenja akiwa nyumbani Mikocheni B amesema, vifo vya wazazi wao vimewashtua na kuwahuzunisha sana.
Amesema, Baba yao alifariki asubuhi katika Hospitali ya Saifee ambapo alikuwa akipatiwa matibabu kwa wiki moja kutokana na tatizo la moyo ambalo lilikuwa likimsumbua kwa muda mrefu.
"Kutokana na hali hiyo alikua akipata maumivu ya kifua ya mara kwa mara. Kuhusu taarifa za mama bado haijathibitishwa mpaka sasa na kuna watu wameitwa hospitali,"amesema.
Mbunge huyo wa zamani katika Jimbo la Ubungo Dar es Salaam kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) amewahi kuishauri serikali kufanya uamuzi mgumu wa kulipanga upya jiji hilo.
Kupitia chapisho la habari yake katika Gazeti la Serikali la Habari leo miaka kadhaa iliyopita alinukuliwa akisema hiyo ni njia pekee ya kulifanya jiji hilo kwenda sambamba na hadhi ya majiji mengine duniani.
Kwamba, endapo serikali itathubutu kufanya hivyo, kero za foleni, ujenzi holela, barabara finyu na ukosefu wa mitaro ya kutosha katika maeneo mengi ya Jiji, yatakuwa historia.
Alisema hayo katika mahojiano maalumu, yaliyofanyika jijini Dar es Salaam.
"Kwa ujumla, asilimia 80 ya Jiji ni hovyo kabisa na tunajidanganya tunajenga Jiji ambalo naamini kuna siku tutalibomoa, kwa sababu tunakaribisha balaa.
"Kero haipo katika foleni tu, kila kitu Dar ni hovyo, ujenzi hovyo, miundombinu hovyo, lakini haya yote yana tiba, tena inayoweza kuwa historia ni kufanya uamuzi mgumu wa kulipanga upya Jiji.
"Tatizo si pesa, bali uamuzi, sisi hatujaamua na gharama za kutoamua ni kubwa mno, angalia muda unaopotea njiani, uchafuzi wa mazingira unaotokana na moshi na hata matumizi makubwa ya mafuta kwa kusimama kwenye foleni. Ndiyo, yaweza kuonekana kuwa ni gharama kubwa sana, kweli ni gharama, lakini kuiogopa gharama ni kukaribisha hatari zaidi katika siku za usoni.
Ni bora tuwahi sasa kufanya uamuzi mgumu, kwa sababu sehemu kubwa ya Jiji haijaharibiwa, tuwahi kuijenga," alisema Keenja, Mwenyekiti wa zamani wa Tume ya Jiji la Dar es Salaam, aliyejipatia umaarufu mkubwa kutokana na kulirejeshea hadhi jiji.
Na ni kutokana na utendaji huo, haikushangaza kuona akipata ubunge kwa urahisi mwaka 2000 katika Jimbo la Ubungo na baadaye kuteuliwa na Rais Hayati Benjamin Mkapa, kuwa Waziri wa Kilimo na Chakula kuanzia mwaka 2000 hadi 2005.
Akizungumzia foleni, alisema kuna kazi kubwa inayopaswa kufanyika, lakini akashauri bora huduma nyingine za kijamii zisambazwe katika maeneo tofauti ya Dar es Salaam, lengo likiwa kuzuia safari zisizo za lazima kwenda katikati ya jiji.
"Kuna mengi ya kufanya, lakini tuanzie na kusambaza huduma za jamii. Leo hii mtu ana shida ya kamba ya viatu, lazima afunge safari huko aliko hadi Kariakoo au katikati ya Jiji. Kwa mtaji huu, msongamano utakosekana? Na ikumbukwe foleni hizi zina gharama kubwa, kuanzia suala la muda, uchafuzi wa mazingira kutokana na moshi na hata matumizi makubwa ya mafuta ambayo yanachangia kuharibu bajeti za watu," alisema Keenja.
Alionya kuna hatari kadhaa za kiuchumi zinazoweza kujitokeza, kutokana na shughuli nyingi kucheleweshwa na foleni. Katika kuthibitisha jinsi foleni ilivyogeuka kero Dar es Salaam, taasisi moja ya utafiti ya CEP inaonyesha kwamba safari nyingi zisizozidi umbali wa kilomita 16 tu, zinalazimu kutumia hadi saa mbili, achilia mbali muda ambao abiria anapoteza kituoni kusubiri usafiri.
Mbali ya kupendekeza kuanzishwa kwa vituo vya kibiashara, vitakavyosaidia wakazi wengi wa Jiji kupata huduma huko waliko badala ya wote kuelekea katikati ya mji, Keenja alipendekeza pia kuongeza barabara mbadala na pia kujenga barabara za juu katika makutano ya barabara kuu.
"Flyovers ni suluhu mojawapo, lakini pia kuna barabara zinazostahili kuimarishwa ili kuondoa msongamano.
"Angalia, anayetaka kwenda Tanga lazima apite Ubungo, hakuna ulazima, ingeimarishwa Barabara ya Bagamoyo, watu wakapita huko Pangani mpaka Tanga. Lakini hali haikuwa hivyo, kwamba ukitaka kwenda nje ya Dar es Salaam, safari lazima ianzie Ubungo! Tunapaswa kubadilika,"alisema Keenja na kuonya kwamba, mbali ya sababu za kiuchumi na kiafya, hali inaweza kuwa mbaya endapo kunaweza kutokea matatizo yoyote ya amani.
"Hivi yakitokea machafuko leo hii, watu watakimbilia wapi, ni kuangamia tu kwa sababu hatuna barabara, angalia kote, kila pande ya Jiji hali ni hiyo, ndiyo maana nasema, si barabara tu, kila jambo tukiamua kwenda hatua kwa hatua, tunaweza, lakini kwa kusubiri fedha taslimu, kamwe hazitapatikana kwa sababu matatizo daima huwa hayaishi,"alisema.
Akizungumzia ujenzi holela, licha ya kusikitishwa na jinsi jiji linavyokosa mpangilio, alisema anashangazwa kuona sheria zipo, lakini hazifanyi kazi.
"Ndiyo kuna sheria za mipango miji, lakini hazifuatwi, badala yake watu wanajijengea hovyo hovyo na kuigeuzia kibao serikali kwa kudai huduma kule wanakokuwa
kimsingi serikali ndiyo iliyopaswa kutenga maeneo, kuweka huduma zote muhimu na kuelekea aina ya ujenzi
Lakini ni kinyume, mtu ananunua kiwanja, anachokoza ujenzi, akiona watu wanaongezeka, wanaanza kudai maji, umeme, barabara na mengineyo bila kujua huko waliko serikali haijapangia bajeti, lakini kwa sababu kosa limeshatendeka, basi wakati ni huu, hatujachelewa ili hapo baadaye tusijute zaidi.
"Kote duniani, mji hupangwa, si kwamba watu wanajipangia, lazima tuwe na Master Plan
Dar ninayoijua mimi ilikuwa na viwanja vya wazi zaidi ya mia moja, lakini sasa havifiki hata 30, watu wanajigawia na kujijengea kiholela, Kariakoo ndio usiseme,"alisema.
Kutokana na kukithiri kwa ujenzi holela, ameshauri uandaliwe mradi utakaokwenda awamu kwa awamu, ili kuupanga mji, akitolea mfano Magomeni Mapipa kwamba maghorofa matatu yanaweza kuweka familia nyingi pamoja, huku wakihamishwa kwenda nyumba zao hivyo kutoa mwanya kwa serikali kubomoa nyumba na kuupanga mji kwa mpangilio mzuri wenye hadhi ya Jiji.
"Tukianzia hapa, tutakwenda sehemu nyingi, mwisho wa siku mji utajikuta umepangiliwa vizuri ajabu, ndiyo maana nashauri kwa sababu huku tumeshaharibu, tuanzie kuupanga mji kule ambako hakujaharibiwa,"alisema.
Utafiti wa awali wa Diramakini Blog umebaini kuwa, tangu Serikali ya Awamu ya Nne hadi ya Sita ziiingie madarakani kwa asilimia kubwa, mapendekezo ya Mheshimiwa Charles Keenja yamefanyiwa kazi huku mengine yakiendelea kutekelezwa kwa kasi kubwa.