Askofu Kasala:Wana Geita njooni mpate chanjo ya Corona

Na Robert Kalokola, Diramakini Blog

MAKAMU wa Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) na Askofu wa Jimbo la Geita, Flavian Kasala amewataka wananchi kuona umuhimu wa chanjo na kujitokeza kuchanja ili kuweza kupambana na wimbi la tatu la virusi vya Uviko-19.
Baadhi ya wananchi waliojitokeza katika ukumbi wa Gedeco mjini Geita katika zoezi la uzinduzi rasmi wa Chanjo ya Uviko19 mkoa wa Geita. (Picha na Robert Kalokola).

Askofu Kasala ametoa wito huo leo katika uzinduzi rasmi wa chanjo ya kupambana na maambukizi ya virusi vya Uviko-19 Mkoa wa Geita uliofanyika katika ukumbi wa Gedeco Mjini Geita uliozinduliwa na Mkuu wa Mkoa wa Geita, Rosemary Senyamule.

"Katika awamu hii ya mzunguko wa tatu, tatizo hili limejidhihirisha kuwa ni kubwa sana, ni nafasi kwa sisi kuonesha imani kubwa kwenu katika kutusimamia kwani uwepo wenu ni kwa ajili ya ustawi wa Taifa, kwani utaalamu wa kisayansi na imani kwa viongozi wetu mimi binafsi nakubali kuingia katika chanjo na natoa wito kila mmoja ajitafakari na aone umuhimu na kupata chanjo,"amesema Askofu Kasala.
Mkuu wa Mkoa wa Geita Rosemary Senyamule akachomwa Chanjo ya Uviko-19 baada ya kuzindua rasmi zoezi la kuchanja wananchi wote katika mkoa wa Geita. (Picha na Robert Kalokola).

Akizungumza kwenye uzinduzi huo, Mkuu wa Mkoa ameishukuru serikali kwa kuwajali wananchi kwa kuwaletea Chanjo ili kuwakinga na Maradhi hayo yaliyo kwenye wimbi la tatu la maambukizi tangia kuibuka kwa ugonjwa huo mwaka 2019.

Aidha, Mkuu wa Mkoa ametoa rai kwa wananchi kwenda kupata chanjo hiyo kuanzia leo siku ya uzinduzi kwenye vituo vilivyobainishwa ambapo kwa Mkoa wa Geita wananchi wapatao elfu 50 watapata chanjo hiyo kwa awamu ya kwanza kwenye vituo 18 yaani vituo vitatu kwenye kila wilaya.

"Serikali yangu inajali na inawatakia mema watanzania wote, natoa wito kwa Makundi yote yaliyobainishwa kwa awamu ya kwanza kwenda kupata chanjo hii muhimu,"amesema.

Mkuu wa Wilaya ya Geita,Wilson Shimo pamoja na mambo mengine ametoa rai kwa wananchi kufanya mazoezi ya viungo na kuzingatia lishe bora kwa kula vyakula vyenye mlo kamili pamoja na vitamini C.

"Tunachokifanya hapa ni kwa maslahi ya afya zetu,twendeni tukapate chanjo kwani pamoja na maneno mengi yanayozunguka, lakini hili tatizo lipo,"amesema Mwinyiheri Baraza, kwa niaba ya Chama Cha Mapinduzi Mkoa.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Geita, Japhet Simeo amebainisha kuwa, chanjo ya ugonjwa wa Uviko-19 (COVID-19) inasaidia kupunguza uwezekano wa mgonjwa kupata dalili kali na hatarishi na inapunguza upotevu wa uhai wa watu.

Aidha, Mganga Mkuu amesema kwa awamu hii ya kwanza wamepokea chanjo yenye dozi elfu hamsini, lakini Mkoa wa Geita unatarajia kuchanja jumla ya wananchi laki tatu ili kupambana na maambuzi ya ugonjwa huo.
Mwandishi wa habari wa Gazeti la Majira Mkoa wa Geita, Mutta Robert akichanjwa katika uzinduzi wa Chanjo ya Uviko-19 mkoa wa Geita. (Picha na Robert Kalokola).
Mwandishi wa habari wa ITV mkoa wa Geita Basil Elias akichanjwa kwenye uzinduzi rasmi wa Chanjo ya uviko19 mkoa wa Geita.(Picha Robert Kalokola).

Mkoa wa Geita umezindua rasmi zoezi la kutoa chanjo kwa watu Agosti 4, mwaka huu ikiwa ni baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuzindua rasmi Julai 28, mwaka huu Ikulu jijini Dar es salaam.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news