NA MWANDISHI DIRAMAKINI
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimemuomba radhi Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kuandikwa vibaya na gazeti la chama la Uhuru.
"Tunamuomba radhi Rais kwa kumlisha maneno, ukifuatilia mahojiano yoyote BBC hakuna sehemu amezungumza na muungwana ni vitendo. Tayari bodi imewasimamisha kazi Mkurugenzi Mtendaji, Ernest Sungura, Mhariri mtendaji na Rashid Zahoro ambaye alikuwa msimamizi gazeti;
Hayo yamesemwa leo na Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo wakati akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi ndogo za chama zilizopo Lumumba mkoani Dar es Salaam.
Pia ndugu Chongolo ametangaza kusimamisha uchapwaji wa gazeti la Uhuru kwa siku saba kuanzia leo Jumatano kwa kuandika habari ya kupotosha juu ya Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.
Kupitia gazeti hilo nakala ya leo lilionekana kumlisha maneno Mwenyekiti huyo wa chama Taifa ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan.
“Gazeti la Uhuru ni letu,hatuwezi kulikana, maneno yameandikwa kwenye gazeti letu, nianze kwa kumuomba radhi Rais wetu kwa kumlisha maneno ambayo hajayasema, mahojiano yote ukifuatilia hakuna aliposema yaliyoandikwa kwenye kichwa cha habari cha Uhuru leo.
“Asubuhi ya leo niliagiza Bodi ikutane, Bodi imewasimamisha kazi Viongozi ambao wameonekana kuhusika moja kwa moja kwenye shughuli ya uendeshaji, wa kwanza Mkurugenzi Mtendaji Ernest Sungura, wa pili Mhariri Mtendaji na wa tatu Rashid Zahoro ambaye alikuwa Msimamizi wa Gazeti la leo na nimeipongeza Bodi kwa uamuzi wao mzuri.
“Bodi imeunda Tume ya kuchunguza sababu ya hili kutokea na nimewapongeza, pia kwa Mamlaka yangu nimesimamisha kuanzia leo uchapaji wa Gazeti la Uhuru kwa siku saba "amefafanua Chongolo.
Aidha,Chama Cha Mapinduzi (CCM) leo asubuhi kilisema kimesikitishwa na habari iliyoandikwa ukurasa wa mbele ikimnukuu Rais Samia akisema hatogombea Urais 2025.