CHADEMA wasusia mwaliko wa NEC kesho

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) imesema haitashiriki hafla ya kukabidhi taarifa ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 itakayofanyika kesho Agosti 21, 2021 Ikulu, Dar es Salaam.
Badala yake itaendelea kuweka nguvu zaidi katika ajenda zake za kipaumbele.

Taarifa ya CHADEMA iliyotolewa leo Agosti 20, 2021 na Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje, John Mrema imesema wamepokea mwaliko kutoka NEC lakini hawatakwenda huku wakitoa sababu tano.

"Tumepokea mwaliko kutoka kwa Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa ajili ya Mwenyekiti wa Taifa, Katibu Mkuu, Mgombea Urais na mgombea umakamu wa Rais kuhudhuria shughuli hafla ya kukabidhi kwa Rais taarifa ya uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.

"Chama kupitia barua ya Katibu Mkuu kimemjulisha Mkurugenzi wa Uchaguzi kuwa hatutashiriki hafla iliyopangwa kufanyika Ikulu Agosti 21," amesema Mrema katika taarifa hiyo ambayo ilitaja sababu tano za chama hicho kutoshiriki.

CHADEMA ambacho mgombea wake katika nafasi ya urais alishika nafasi ya pili, kimesema hakukuwa na uchaguzi na hawawezi kushiriki tukio lolote linahohalalisha uchaguzi huo, lakini pia kilisema kwa sasa kinaelekeza nguvu zake kuhakikisha mwenyekiti wao na wanachama wanaoshikiliwa na vyombo vya dola wanaachiliwa huru.

Kadhalika CHADEMA imesema aliyekuwa mgombea wao alilazimishwa kukimbilia nchi za nje, NEC imepuuza barua yao juu ya orodha ya wabunge wa viti maalumu na kwa sasa chama hicho agenda yake kuu ni Katiba mpya.

"Kwa sababu tajwa Chama hakitatuma mwakilishi katika hafla hiyo badala yake tutaendeleza nguvu kutetea uhuru, haki, demokrasia na maendeleo ya watu,"wameeleza.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news