Na Robert Kalokola, Diramakini Blog
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Geita, Zahara Michuzi amesema, ujenzi wa uwanja wa michezo unaojengwa kwa Bilioni 2.4 eneo la Magogo Kata ya Bombambili Mjini Geita utafungua fursa za kiuchumi kwa wananchi wa Geita.
Mkurugenzi wa Mji wa Geita Zahara Michuzi akizungumza na vyombo vya habari baada ya kukagua ujenzi wa uwanja wa mpira unaoendelea kujengwa mjini Geita. (Picha na Robert Kalokola).
Amesema, fursa hizo zitatokana na kuja kwa wageni wengi kutokana na michuano ya ligi kuu itakayokuwa inachezewa katika uwanja huo.
Ametaja baadhi ya fursa hizo kuwa ni kama huduma za hoteli kwa wageni wataohitaji kulala, huduma za vyakula mbalimbali,usafiri na nyingine nyingi.
Amesema, wameongeza nguvu za usimamizi kwa kufika eneo la mradi mara kwa mara kuhakikisha ujenzi unakamilika kwa wakati ili uanze kufungua fursa za kiuchumi kwa wananchi wa Mji wa Geita kama vile biashara ya hoteli na huduma za chakula kwa wageni watakaofika wakati wa ligi kuu.
Sehemu ya uwanja wa Mpira unaojengwa wa Halmashauri ya mji wa Geita. (Picha na Robert Kalokola).
Aidha, amefafanua kuwa ujenzi wa unatarajiwa kukamilika mwezi Novemba mwaka kwa sababu mkandarasi anayetekeleza mradi huo ana vifaa vya kutosha na wao kama Halmashauri wanamsimamia kwa ukaribu zaidi.
Mkurugenzi Michuzi amesema hayo wakati akikagua ujenzi wa uwanja akifuatana na baadhi wataalamu wa Halmashauri hiyo ambao ni Afisa Utumishi wa Halmashauri ya Mji wa Geita Thecla Gasembe,Afisa Habari wa Mji, Trovina Kikoti pamoja na Mhandisi wa ujenzi wa Halmashauri hiyo Major Samwel.
Ujenzi huo umeanza mara baada ya timu ya Geita Gold Football Club inayomilikiwa na Halmashauri ya mji wa Geita kufuzu kushiriki mashindano ya Ligi Kuu soka Tanzania Bara.
Mkurugenzi wa mji wa Geita, Zahara Michuzi (katikati) akiwa na Mhadisi wa mji huo, Major Samwel na Mkandarasi wa ujenzi huo wakikagua ujenzi wa uwanja huo.(Picha na Robert Kalokola).
Kutokana na ujenzi huo kukamilika Novemba mwaka huu,kwa sasa Halmashauri ya mji Geita imeamua kukarabati uwanja wa Shule ya Wasichana Nyankumbu utumike kwa michezo yote ya nyumbani wakati ukisubiriwa uwanja wa kisasa wa Geita Stadium ukamilike katika hatua ya kwanza ya ujenzi.
Mhandisi wa Halmashauri hiyo Major Samwel amesema ujenzi huo unafanywa na Mkandarasi mzawa ambaye ameungana na mwenzake wote wakiwa wa mjini Mwanza chini ya usimamizi wa Ofisi ya Mkurugenzi kupitia ofisi ya Mhandisi huyo.
Amesema ujenzi umefikia kiwango cha 21% na hadi sasa hakuna kiasi chochote ambacho mkandarasi amelipwa ikiwa ni dalili ya mkandarasi kuwa na uwezo mkubwa wa kutekeleza mradi huo.
Kifusi cha udongo kikimwagwa katika ujenzi wa uwanja wa mpira katika mji wa Geita. (Picha na Robert Kalokola).
Mkurugenzi wa mji wa Geita Zahara Michuzi( wa tatu kutoka kushoto) akiwa na Afisa Utumishi Thecla Gasembe (wa kwanza kushoto) na Mhandisi wa mji wa Geita Major Samwel.(Picha Robert Kalokola).
Ameongeza kuwa kwa hatua ya kwanza ya ujenzi huo ,wanajenga eneo la kuchezea mpira (pitch), eneo la njia za kukimbilia mbili,jukwaa la viongozi, vyumba vya wachezaji kubadilishia nguo, vyumba vya waandishi wa habari kurushia matangazo na jengo la huduma ya kwanza na matibabu.
Amefafanua kuwa,uwanja huo unatajia kubeba watu 12,000 kwa wakati mmoja baada ya kukamilika ujenzi na umesanisifiwa kwa ajili ya matumizi ya nyasi za kawaida.
Uwanja huo unajengwa kwa fedha iliyotolewa na Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGML) kama uwajibikaji kwa jamii (CSR) .