NA MWANDISHI DIRAMAKINI
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Wasafi ambayo ndiyo wamiliki wa Wasafi Media, Diamond Platinum amemuaga rasmi mtangazaji maarufu wa habari za michezo na uchambuzi,Maulid Kitenge (chumvi).
Wasafi chini ya Diamond ni miongoni mwa makampuni makubwa nchini ambayo inamiliki lebo ya muziki ya WCB, studio za kurekodia muziki Wasafi Records, vyombo vya habari kama Wasafi FM na Wasafi TV, majukwaa ya kusambaza nyimbo mtandaoni Wasafidotcom na pia kampuni hiyo ndio waandaaji wa tamasha la Wasafi Festival na nyingine nyingi.
“Kwanza kabisa nikushukuru kwa mchango wako mkubwa katika taasisi ya Wasafi Media, kwa kuwa nasi bega kwa bega kuanzia Media changa mpaka leo imekuwa Media nambari moja nchini katika kila report...
"Hakika haikuwa rahisi, shukrani sana na sasa nina amani ukirudi nyumbani.Mbali ya ushiriki wako kwenye Media, siku zote umekuwa ni kama kaka ama Uncle kwangu...na ninakuahidi kwenda kwa kasi ile ile ambayo siku zote umenisihi kuifanya, ili kutimiza malengo ya WASAFI MEDIA kuwa chombo kikubwa cha habari Afrika na kulipa heshima Taifa letu," ameandika Diamond Platinum katika ukuta wake wa Tweter kama alivyokaririwa na Diramakini Blog.
Uamuzi huo unafikiwa ikiwa ni mwishoni mwa mwaka 2019, mtangazaji huyo maarufu wa habari za Michezo Tanzania, Maulid Kitenge kumeweka wazi kuwa ameachana na Kituo cha Redio cha EFM na kujiunga Wasafi FM inayomilikiwa na mwanamuziki, Diamond Platinumz.
Maulid Kitenge alikuwa mtangazaji wa EFM tangu mwaka 2015 akitokea Redio One na ITV, ambapo akiwa EFM alikuwa kama Mkuu wa Idara ya Vipindi vya Michezo, huku akitangaza vipindi vya michezo vya Sports Headquarters na E-Sport, pamoja na kusoma magazeti kwenye Kipindi cha Joto la Asubuhi ndani ya EFM.
Miongoni mwa vipindi alivyoanzisha na kuleta mageuzi makubwa katika michezo ndani ya Wasafi ni pamoja na Sports Arena na Sports Court huku akionyesha ubunifu wa hali ya juu katika uchambuzi wa magazeti katika stesheni hiyo kila siku asubuhi.