Dkt.Kasululu: Wananchi 2,300 wamepata chanjo ya UVIKO-19 mkoani Rukwa

NA MWANDISHI MAALUM

Serikali imebainisha mafanikio ya zoezi la kutoa chanjo ya kinga dhidi ya ugonjwa wa virusi vya Corona (UVIKO-19) ambapo wananchi wapatao 2,300 tayari wamejitokeza kupata chanjo hiyo mkoani Rukwa tangu kuzinduliwa kwa zoezi hapo mwanzo mwa mwezi huu.

Hayo yamebainishwa Agosti 17, 2021 na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Dkt. Boniface Kasululu wakati akiongea na waandishi wa habari kwenye kituo cha Afya Halmashauri ya wilaya Kalambo.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Dkt. Boniface Kasululu akiongea kwenye mkutano wa kuhamasisha wananchi kujitokeza kupata chanjo ya hiari jana kwenye kijiji cha Matai wilaya ya Kalambo mkoa wa Rukwa.

Mganga Mkuu huyo alisema takwimu zinaonesha tangu kuzinduliwa kwa zoezi la kutoa chanjo hapo Agosti 03 mwaka huu wananchi wengi kwenye wilaya tatu za mkoa wa Rukwa wameendelea kujitokeza ambapo jumla ya watu 2,300 wamekwishapatiwa chanjo kwa hiari kati ya dozi 20,000 zilizopokelewa mkoani.

Dkt. Kasululu akiwa kwenye kituo cha Afya Matai Wilaya ya Kalambo alitumia fursa hiyo kuendelea kuwasihi wananchi kuwa chanjo zinazotolewa na Serikali ni salama na kuwa zimefanyiwa tathmini mathalani hadi sasa kitaifa watu zaidi ya Laki Mbili tayari wamepata chanjo hiyo ya UVIKO 19 kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Afya.

“Kama Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan amechanja, Mkuu wa Mkoa wetu Joseph Mkirikiti amechanja nami pia nikiwa Mganga Mkuu wa Mkoa nimechanja pia zaidi ya watu wengi tayari wamechanja hakuna haja ya kuogopa kuchanja chanjo hii ya UVIKO 19” alinukuliwa Dkt. Kasululu.

Alipoulizwa kuhusu changamoto kwenye zoezi hilo Dkt. Kasululu alibainisha kuwa Wilaya ya Kalambo bado kuna mwitikio mdogo ukilinganisha na halmashauri zingine kutokana na baadhi ya taarifa za upotoshaji wa baadhi ya watu.
Sehemu ya wananchi wa kijiji cha Matai wilaya ya Kalambo mkoa wa Rukwa wakifuatilia mada kuhusu uhumimu wa chanjo dhidi ya UVIKO-19 iliyotolewa na wataalam wa afya jana.

Awali akifungua kampeni ya usawazishaji wa vikope kwa wananchi wenye matatizo mbali mbali ya macho Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Sebastian Waryoba aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Rukwa aliwasihi wananchi wa Wilaya ya Kalambo kuendelea kujitokeza kupata chanjo ya UVIKO 19 huku wakichukua tahadhari zingine.

Mkuu huyo wa Wilaya alibainisha kuwa pamoja na kuchukua jitihada zingine za kujikinga na UVIKO 19 ni budi wananchi wakaendelea kumwomba Mungu aliepushe Taifa letu na janga la Corona.

“Tuendelee kumwomba Mungu atuepushe na ugonjwa huu wa Corona na Tanzania iendelee kuwa nchi salama huku tukizingatia ushauri wa wataalam wa afya” alisema Waryoba.

Mkoa wa Rukwa ulipokea dozi 20,000 za chanjo UVIKO 19 ambapo awali ilitenga vituo 11 vya kutoa chanjo lakini kutokana na ukubwa na mtawanyiko wa watu imelazimu kuongeza vituo pia kutumia huduma vikoba (mobile clinic) ili kuwafikia wananchi wengi waliopo mbali na vituo vya afya.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news