Singiba Buchadi, Dephina Buchadi, Doratea Mathayo, Wilbard Teobardi, Albert Buchadi na Valenzi Silvester wakazi wa Kongowe wapo mikononi mwa Jeshi la Polisi kutokana na tuhuma zinazowakabili.
Kwa mujibu wa Kamanda huyo, Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linawashikilia watu hao sita kwa tuhuma za kuwashambulia na kuwarekodi video za utupu watu wawili waliokuwa faragha na kisha kuzisambaza mitandaoni kwa madai kwamba wamewafumania.
Hatua hiyo imekuja kufuatia agizo la Waziri wa Mambo ya Ndani George Simbachawene, alilolitoa Agosti 6, 2021 mkoani Dar es Salaam baada ya kuona video inayosambaa mitandaoni ikionesha mwanamke na mwanaume waliokuwa faragha wakidhalilishwa kwa kupigwa wakiwa watupu.
Watuhumiwa hao wanashikiliwa kutokana na kitendo ambacho walikifanya kwa kutoa adhabu wakati hakuna mwenye mamlaka ya kufanya hivyo zaidi ya Mahakama.
“Hivi karibuni kumejitokeza tabia ya baadhi ya Watu wanawavamia Wapenzi ambao wanafanya faragha zao, tabia hii ambayo imeshamiri kama clip nyingi zinavyorushwa ni kinyume cha Sheria kabisa kuwaingilia Watu walio kwenye faragha na wakati mwingine wengine kufanya hivyo kwa kisingizio kwamba wamefumania, litakuwa fumanizi kama halijawa jambo la kupanga au Watu kujikusanya na kwenda kuvamia sehemu na pia lazima Mke au Mume awe na cheti halali cha ndoa na sio kusema huyu alikua hawara yangu.
“Wanaodhalilika zaidi katika hili ni Wanawake, wengine wanakuwa uchi wa mnyama hawana nguo wanapata kipigo, naaagiza Polisi Mikoa yote kufuatilia hasa lile tukio linalozunguka kuanzia jana kuhakikisha wanakamatwa na kufikishwa Mahakamani,"amesema Waziri Simbachawene.