Hawa ndiyo waliotajwa kuhusika katika kuwatishia watu kwa bastola Dar

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es salaam linawashikilia watu wanne kwa tuhuma za kutishia watu kwa bastola wanazozimiliki kihalali.
Watuhumiwa wote silaha zao zinashikiliwa na Polisi na taratibu za kisheria zitafuatwa ikiwa ni pamoja na kuwafutia umiliki wa silaha hizo.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Muliro Jumanne ameyasema hayo leo wakati akizungumza na waandishi wa habari.

Amewataja watuhumiwa hao kuwa ni Isack Robert Wile maarufu Wambura,(44) mkazi wa Sinza E, Rashid Iddi Mshana (36) mkazi wa Mwenge, Mussa Rashid Mshana (39) mkazi wa Mwenge na Ibrahim Shaibu (52) mkazi wa Kinyerezi.

“Mtuhumiwa wa kwanza, Isack Robert Wile (Wambura) akiwa katika Bar iliyopo Sinza alitoa silaha yake bastola aina ya Browning yenye namba TZCAR 72791 na kuanza kutishia Watu huku akiwa amelewa pombe,"amesema Kamanda Muliro.

“Mtuhumiwa wa pili, Rashid Iddi Mshana alionekana kwenye video clip iliyosambaa kwenye mitandao akitishia, Polisi walimkamata Mtuhumiwa huyo akiwa na silaha bastola yenye risasi 10 ndani ya magazine ikiwa inamilikiwa na kaka yake aitwae Mussa Rashid Mshana,”amesema.

Kamanda huyo amesema, mtuhumiwa wa tatu Mussa Rashid Mshana anatuhumiwa kwa kosa la uzembe ambapo alimwachia silaha mdogo wake ambaye ni Rashid Iddi Mshana.

Amesema, mdogo wake huyo alijirekodi akitishia watu kwa silaha na kutuma mkanda mfupi wa video kwenye mitandao ya kijamii.

“Mtuhumiwa wa nne, Ibrahim Shaib Agosti 1 saa 12:00 jioni maeneo ya Vijibweni Kigamboni alimtishia kumuua kwa silaha jirani yake aitwae Chacha Mwita walipokuwa wanagombania mipaka ya kiwanja katika maeneo yao, Mtuhumiwa alikamatwa akiwa na silaha bastola aina ya LUGER ikiwa na risasi sita,"amesema Kamanda Muliro.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news