NA MWANDISHI DIRAMAKINI
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu iliyopo katika Jiji la Ilala mkoani Dar es Salaam imeshindwa kumuunganisha Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe na wenzake watatu wanaokabiliwa kwa tuhuma za kesi ya uhujumu uchumi yenye mashtaka ya ugaidi.
Ni kutokana na mawasiliano mabaya kwenye Ukumbi wa Mahakama ya Mtandao (VC) kati ya Kisutu na Gerezani la Ukonga ambapo ndipo walipo washtakiwa hao.
Mapema leo Agosti 5,2021 kesi hiyo ambayo imepangwa kusikilizwa kwa ajili ya mtandao ilikuja kwa ajili ya kutajwa mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba na kumuunganisha Mbowe na wenzake baada ya yeye kusomewa mashtaka peke yake, lakini ilishindikana baada ya Mbowe na wenzake kushindwa kupata mawasiliano mazuri kutoka mahakamani.
Katika kesi hiyo, upande wa mashtaka unawakilishwa na Wakili wa Serikali Pius Hilla, Christopher Msigwa na Grace Mwanga huku upande wa utetezi ukiwakilishwa na Wakili wa utetezi Peter Kibatala, Jonathan Mndeme, John Malya na Frederick Kihwelo.
Wakati Mahakama inaendelea, washtakiwa Mbowe na wenzake walikuwa wakionekana kwenye video ya ukumbini hapo, lakini wao walikuwa hawaoni kitu ndipo Mbowe akalalamika kuwa, haoni picha ya mahakamani.
"Mheshimiwa hatuwaoni, tunawasikia sauti tu, lakini hatuwaoni," amedai Mbowe.
Wakati marekebisho yakiendelea kufanyika Wakili Simba alishauri kuahirishwa kwa kesi iwapo mawasiliano yatashindikana kutengemaa ushauri ambao ulikubaliwa na pande zote mbili.
Baada ya dakika kadhaa za juhudi za wataalamu wa teknolojia ya mawasiliano kushindikana, washtakiwa waliulizwa kama wako tayari kuendelea kusomewa mashtaka katika hali hiyo, lakini Mbowe alikataa na hivyo pande hizo mbili zikakubaliana kurudi mahakamani kesho, kwa makubaliano ya washtakiwa wawepo mahakamani.
Wakati huo huo, wafuasi wa CHADEMA waliokuwa wamekusanyika nje ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu baada ya kuzuiwa kuingia ndani wanashikiliwa na Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam.
Wafuasi hao waliokuwa wamefika kwa ajili ya kufuatilia kesi ya Mwenyekiti wa chama hicho Taifa, Freeman Mbowe ambaye hata hivyo hakufikishwa mahakamani walikamatwa baada ya kutoa mabango yenye jumbe mbalimbali na kuanza kuimba.
Hata hivyo, askari waliokuwa kwenye magari mawili waliteremka kisha kuwazunguka na kuwakamata baadhi yao na wengine kufanikiwa kukimbia.
Mheshimiwa Mbowe ambaye alifikishwa mahakamani Julai 26, 2021 anakabiliwa na mashtaka mawili ambayo ni kula njama za kutenda kosa na kutoa fedha kwa ajili ya kufadhili shughuli za ugaidi, huku wenzake watatu wao wakikabiliwa na mashtaka 7.