NA MWANDISHI DIRAMAKINI
Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Simon Sirro amesema kuwa, Jeshi la Polisi linaendeshwa kwa maandishi na kuna taratibu, hivyo wanasubiri barua kutoka kwa Waziri wa Afya, Dkt.Dorothy Gwajima ili waangalie wanatekeleza vipi agizo lake la kumkamata na kumuhoji Mbunge wa Kawe, Askofu Josephat Gwajima.
Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Simon Sirro
Ameongeza kuwa, maelekezo hayo ameyaona kwenye mitandao ya kijamii, hivyo anasubiri barua rasmi ili waangalie jinsi ya kuyatekeleza kwani serikali inakwenda kwa maandishi.
Katika mahojiano na Clouds Fm, IGP Sirro pia amesema wataangalia kama kweli kuna jinai au la! ambayo ina haja ya kufungua mashitaka.
Amesema, pia kama hawatakuta jinai watashauri jinsi ya kumaliza hilo suala katika njia nzuri.Zinazohusiana, soma hapa>>>
Awali kupitia habari iliyoripotiwa na DIRAMAKINI Blog, Mheshimiwa Dkt.Doroth Gwajima ambaye ni Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto aliliagiza Jeshi la Polisi pamoja na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini ( TAKUKURU) kumkamata na kumhoji mbunge wa Kawe, Askofu Josephat Gwajima.
Ni ili athibitishe kauli anazozitoa dhidi ya Serikali na viongozi kuhusu chanjo ya Uviko-19 inayotolewa hapa nchini.
Ametoa agizo hilo leo Agosti 17, 2021 katika kijiji cha Kyatunge wilayani Butiama akibainisha kuwa Askofu Gwajima amekuwa akitoa taarifa za kupotosha kwa makusudi jambo linaloivuruga wizara yake na Serikali katika mapambano dhidi ya ugonjwa huo.
Awali akizungumzia kuhusiana na Chanjo ya (Uviko-19) Waziri Gwajima amewataka Watanzania kujitokeza kuchanja kwani chanjo ni salama kabisa na kwamba uzushi wowote unaozushwa juu ya chanjo unapswa kupuuzwa akapongeza uongozi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara chini ya Mganga Mfawidhi Dkt. Joachim Eyembe kwa kazi nzuri wanayofanya kuhudumia wananchi kwa ufanisi.
Akawataka watumishi wa afya mkoani Mara na Tanzania kwa ujumla, kutoa elimu ya corona na kuhimiza Wananchi kuchanja.
"Watu wengi wanaolazwa na kutumia Oxygen ni wale ambao hawajachanja, chanjo ni salama, uzushi na upotoshaji unaotolewa upuuzwe.
"Mtu anakataa chanjo ya Uviko-19 lakini anatumia dawa za TB na mipira ya Kondomu ananunua wakati hatuna kiwanda. hizi zote zinatolewa nje, kwa hiyo chanjo ni salama kabisa hata Rais Hayati Magufuli watu hawakumuelewa alisema tusikimbilie chanjo bali tujiridhishe na serikali ya Awamu ya Sita imejiridhisha tayari na ndio maana imeruhusu chanjo ambayo ni Salama kabisa Wananchi tuepukeni uzushi na upotoshwaji juu ya chanjo. Chanjo zilikuwepo na zitakuwepo vinginevyo tungekuwa vilema na viwete Kutokana na polio na surua," amesema Waziri Gwajima.