Na Nuru Mwasampeta-WM
Kiwanda cha Kwanza cha Baruti nchini kimewekwa jiwe la msingi Wilaya ya Kilwa mkoani Lindi na Naibu Waziri wa Madini, Prof. Shukrani Manya.
Naibu Waziri wa Madini, Prof. Shukrani Manya kulia na Mkuu wa Wilaya ya Kilwa, Zainab Kawawa wakivuta kamba kuashiria kuweka jiwe la msingi wa Kiwanda cha Baruti Kata ya Mandawal Wilaya ya Kilwa mkoani Lindi tar 12 AgostI, 2021.
Kiwanda hicho kinachojengwa mkoani Lindi na kuwekwa jiwe la msingi tarehe 12 Agosti, 2021 mchakato wake ulianza mwaka 2016 na unatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Oktoba, 2021.
Akizungumza mara baada ya kuweka jiwe la msingi katika kiwanda hicho, Prof. Manya ameupongeza uamuzi wa mwekezaji kuamua kuwa wa kwanza kuwekeza katika masuala ya baruti na kuutaka uongozi wa kiwanda hicho kusimamia matumizi ya baruti hizo ili zisitumike katika njia zisizofaa.
"Kuna nyakati unasikia baruti zinatumika kuharibu mazalia ya samaki kutokana na watu wasiowaaminifu kujitafutia mali kwa njia zisizofaa, niwaombe zisiwe baruti zinazotoka kiwandani hapa,"alisisitiza Profesa Manya.
Katibu Tawala wa Halmashauri ya Wilaya ya Lindi Haji Mbaruku, akitambulisha wageni waliohudhuria katika hafla ya uwekaji jiwe la msingi la Kiwanda cha Baruti wilayani humo tarehe 12 Agosti, 2021.
Akijibu changamoto ya vibali vinavyohitajika katika kuendesha kiwanda hicho iliyowasilishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo Emmanuel Teekishe, Prof. Manya alisema suala hilo litafanyiwa kazi kwa kushirikiana na Mamlaka nyingine za Serikali ikiwa ni pamoja na Mkemia Mkuu wa Serikali, Wizara ya Mawasiliano na Uchukuzi, Wizara ya Viwanda ili kuona namna ya kuweka suala hilo chini ya mwamvuli mmoja.
Aidha, kuhusu changamoto ya kukatikakatika kwa umeme, Prof. Manya aliwatoa hofu wawekezaji nakuwaeleza changamoto itafikia mwisho kutokana na mradi mkubwa wa Uzalishaji umeme wa Mwl. Julius Nyere kukamilika.
Amesema Serikali ya Tanzania imeamua kutokomeza kabisa changamoto hii na kuwataka kuwa wavumilivu kuelekea kwenye mapinduzi makubwa ya kiuchumi kwa kuwezesha ujenzi wa viwanda na mazingira bora ya uwekezaji nchini.
Wananchi wa Kijiji cha Mavuji Tarafa ya Mandawal wakimsikiliza Naibu Waziri alipozungumza nao mara baada ya kuweka jiwe la msingi katika kiwanda cha baruti katika kijiji hicho tarehe 12 Agosti, 2021.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Nitro Explosive Emmanuel Teekishe akiwasilisha taarifa ya mradi kwa Naibu Waziri wa Madini, Prof. Shukrani Manya mara baada ya kuweka jiwe la msingi kiwanda hicho tarehe 12 Agosti, 2021.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kilwa, Zainab Kawawa alisema wananchi wanatamani uwekezaji unaopiga hatua si tu kuwa na wawekezaji lakini suala la kupiga hatua za kimaendeleo kuwa changamoto.
"Tunataka mapato, ajira lakini kilwa ipendeze na kukua kiuchumi," alisisitiza Kawawa.
Aliongeza kuwa, kukiwa na wawekezaji katika halmashauri mapato yanapatikana lakini pia wawekezaji wanakuwa wameacha alama katika kijiji na kuchangia katika kutatua kero mbalimbali za wananchi.
Kawawa alitoa rai kwa wananchi wa eneo lake kuzingatia na kusimamia kikamilifu suala la elimu. "tukazane watoto waende shule ili waweze kupata ajira katika miradi inayowekezwa katika wilaya yetu"alisisitiza.
Aidha, Kawawa amewataka wananchi kutoa ushirikiano kwa wawekezaji pi di wanapofika katika maeneo yao ili asi tuone tija itokanayo na uwekezaji wao.
Akiwasilisha taarifa ya kiwanda hicho Emmanuel Teekishe Mkurugenzi wa Nitro Explosive alisema mpaka sasa wameajili wafanyakazi 117 wageni wakiwa ni wawili tu.
Akizungumzia changamoto wanazokutana nazo alisema wanakutana na changamoto za utitili wa vibali, umeme kukatika katika, wananchi kuchoma misitu hovyo ambapo wameiomba serikali kusaidia katika kutatua changamoto hizo.
Ndoto hii ilianza mwaka 2013 ambapo ujenzi rasmi ulianza 2016 kwa ajili ya makazi ya wafanyakazi nyumba 8 kwa ajili ya wafanyakazi.