Klabu ya KMC FC imeanza rasmi kambi kwa ajili ya kujiandaa vizuri na msimu mpya wa Ligi kuu soka Tanzania Bara 2021/2022 .
Klabu hiyo ya Manispaa ya Kinondoni ya Jijini Dar es Salaam, imeweka kambi Mkoani Morogoro ambapo itakuwa huko kwa maandalizi ya msimu mpya wa mwaka 2021/2022
KMC FC iliondoka Jijini Dar es Salaam Jana asubuhi na ilifika salama mkoani humo ambapo ndio imeweka kambi yake.
KMC FC ikiwa mkoani humo kwa maandalizi hayo ya msimu mpya itakuwa na programu mbalimbali za mazoezi pamoja na kucheza mechi za kirafiki kama program inavyoonyesha kwa lengo la kuwapima na kuwaweka vizuri wachezaji kujiandaa na michezo ya Ligi Kuu itakayoanza Septemba 27 mwaka huu.
Aidha kuhusu suala la usajili, Klabu inaendelea kufanya usajili na wakati wowote kwa utaratibu wa klabu utakapokamilika itaanza kuwatambulisha wachezaji wote ambao wamesajiliwa katika dirisha kubwa lililofunguliwa mapema Agosti mwaka huu.
Hata hivyo KMC FC inawajulisha mashabiki, wapenzi na Watanzania kwa ujumla kuwa usajili unaoendelea kufanyika umezingatia matakwa ya mwalimu na kwamba inasajili wachezaji wenye viwango vya hali ya juu na bora watakaoleta manufaa makubwa katika Timu yetu.
Imetolewa leo Agosti 26
Na Christina Mwagala
Afisa Habari na Mahusiano KMC FC