NA MWANDISHI DIRAMAKINI
Awali Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, (IGP) Simon Sirro amethibitisha kuuawa kwa askari wawili kwenye mapambano ya kurushiana risasi yaliyotokea eneo la Daraja la Salenda jirani na Ubalozi wa Ufaransa mkoani Dar es Salaam.
Tukio hilo limetokea leo Agosti 25, 2021 baada ya mtu mmoja ambaye hajafahamika kuzua taharuki baada ya kufyatua hewani risasi huku akisikika akisema kuwa anawatafuta polisi.
Akizungumza katika kikao kazi cha maofisa wa polisi, IGP Sirro amesema mtu huyo naye ameuawa kwa kupigwa risasi.
“Mmeziona clip zinaruka sasa hivi akaingia barabara kubwa akawa anatamba na SMG na yeye amepigwa risasi na askari wetu hivyo, askari wetu wamefariki na yeye amefariki,” amesema IGP Sirro.
Kwa upande wake, Kamishna wa Oparesheni na mafunzo Liberatus Sabas amesema, "ukiachia watu wanne waliouwawa leo tuna watu sita ambao wamejeruhiwa kwenye tukio hili na wanaendelea na matibabu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, taarifa zaidi tutaendelea kupeana kadri muda unavyokwenda, ni mapema sana kubaini kwanini alifanya vile, lakini tumeshaanzisha timu ya upelelezi na muda sio mrefu tutakamilisha.
"Kuhusu baadhi ya video kusema kwamba huyu mtu ni mkazi wa Upanga sisi hatuthibitishi mambo kupitia clips za video, tunathibitisha mambo kupitia upelelezi kwa hiyo upelelezi ndio utakaoeleza, kuhusu swali la waandishi kuhusu kuwepo kwa dalili zozote za ugaidi kwenye tukio la leo hatuwezi kusema chochote hii ni mapema, lakini uchunguzi ndio utakaosema kama kuna ugaidi au hakuna ugaidi.
"Kwa sasa hatuwezi kusema amekutwa na kitu gani mfukoni, polisi bado wapo eneo la tukio... ni mapema sana kusema amekutwa na nini kwasababu Wataalamu wapo kazini, kuhusu kama ni raia kama sio raia uchunguzi ndio utasema baada ya upelelezi kukamilika tunachojua sasa huyu ni mhalifu,"amesema Sabas.