Serikali yakusanya Bilioni 48/- tozo za miamala ya simu

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Mwigulu Nchemba amesema tangu makato ya tozo za miamala ya simu yaanze wiki nne zilizopita, Serikali imekusanya zaidi ya bilioni 48 ambazo zimepelekwa kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ya kijamii ikiwepo ujenzi wa Vituo vya Afya, Miundombinu ya Barabara pamoja na kuimarisha Sekta ya Elimu.
"Ombi langu moja kwa Watanzania wanaonitazama kwamba jambo hili ni letu sote sio la serikali, nchi hii ni yako wewe hapo ulipo na pesa ni yako na haya mambo tuliyokuwa tunapangilia tuyafanye ni yako, hivyo haya yote ni yetu;

Dkt. Mwigulu amesema, licha ya upatikanaji wa fedha hizo ambazo zinapelekwa kwenye miradi ya maendeleo, Serikali imesikia maoni ya wananchi kuhusu tozo za miamala na kwamba inalifanyia kazi kwa kuliangalia upya suala hilo.

Akizungumza na Waandishi wa Habari Jijini Dar es Salaam leo Agosti 20, 2021, Waziri Nchemba amesema Serikali imesikiliza maoni ya wananchi na sasa imeanza mazungumzo na makampuni ya simu ili kuangalia ni kwa namna gani watawaondolea wananchi mzigo huo wa tozo za miamala.

"Tangu makato ya tozo yaanze kwa hizi wiki nne, tumekusanya zaidi ya shilingi bilioni 48, na kati ya hizo, shilingi bilioni 22 tulishapeleka kwenye ujenzi wa vituo 90 vya afya, na tumezielekeza hasa kwenye maeneo ambayo hayana kabisa vituo hivyo, shilingi bilioni saba tumepeleka kwenye madarasa na zitajenga madarasa zaidi 500 ambayo ni Watoto wetu watakaosoma humo,"amesema Dkt. Nchemba.

Kwa upande wa Zanzibar Dkt.Nchemba amesema wamekusanya Bilioni 1.66 za tozo hizo za miamala.

Ameyataja mambo yaliyochelewesha kupitia upya makato ya tozo hizo za miamala ya simu, kama ilivyoagizwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kuwa,ni mchakato wa ukokotoaji ili kubaini kiwango cha tozo watakachokubaliana na watoa huduma za simu.

“Kilichochelewesha mapendekezo hayo ilikuwa ni hizi namba zilivyokuwa zinasomeka wakati tunaziweka, tulizikadiria kama zenyewe lakini pembeni kulikuwa na namba ambazo watoa huduma walikuwa wanazipata kuanzia, na hapo kulikuwa na makundi mawili, lakini jumla anayoipata mwananchi inakuwa na gharama zilizowekwa na mtoa huduma na zilizowekwa na Serikali," amesema Dkt. Mwigulu.

Aidha, ametoa mfano wa baadhi ya tozo zinazotozwa na Serikali na watoa huduma za simu, kuwa hazilingani na kinachoelezwa kwenye jamii kuwa Serikali inachukua fedha nyingi kutoka kwa watumia huduma hizo.

"Mfano kama kuna eneo la watumiaji Serikali inachukua shilingi 10, mtoa huduma anachukua sh 360, kwenye eneo ambalo Serikali inachukua shilingi 16, mtoa huduma anachukua shilingi 300, kwenye eneo ambalo Serikali inachukua shilingi 27, mtoa huduma anachukua sh. 400, eneo ambalo Serikali inachukua shilinng 56, mtoa huduma anachukua shilingi 500 na sehemu ambayo Serikali inachukua shilingi 125, mtoa huduma anachukua shilingi 780, haya mambo mnayajua ndugu zangu,"amesema.

Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe. Ummy Mwalimu amesema Wizara yake imeshapokea zaidi ya bilioni 22.5 za tozo za miamala ya simu kwa ajili ya juenzi wa vituo vya afya 90 vitakavyojengwa katika Halmashauri 82 za Tanzania Bara, na kwamba fedha hizo zimeshafika kwenye Halmashauri husika.

Nae Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt. Faustine Ndugulile amesema kufuatia agizo la Rais Samia Suluhu Hassan kuhusu kufanyia mapitio tozo hizo, vikosi kazi vinaendelea na kazi hiyo na kwamba punde Wizara yake itatoa mwelekeo mpya wa tozo hizo na kuwaomba watanzania kuwa na subira wakati zoezi hilo likiendelea.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news