Na Doreen Aloyce, Diramakini Blog
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi ametoa siku 90 kwa wamiliki wa viwanja kwa ajili ya ujenzi wa viwanda katika eneo la Kizota Mbuyuni jijini Dodoma, kuviendeleza na atakaye shindwa kutimiza agizo hilo atanyang’anya na kupewa mtu mwingine.
Mheshimiwa Lukuvi amebainisha hayo leo jijini Dodoma wakati alipokuwa akitoa maagizo ya wizara yake kuhusu mgogoro wa ardhi uliokuwepo wa wananchi kuvamia na kujenga kwenye maeneo ya watu wanayoyamiliki kisheria.
Amesema,wizara yake inatoa siku 90, kwa wamiliki wa maeneo hayo kuyaendeleza na atakayeshindwa kufanya hivyo atanyang’anywa na kupewa mtu wengine.
“Kwa wamiliki wenye hati kwa ajili ya kujenga viwanda wafanye hivyo ndani ya siku 90, waende kwa Mkurugenzi kuchukua vibali vya kuendeleza maeneo haya vinginvyo tutawanyang’anya na kuwapa watu wengine,”amesisitiza Lukuvi.
Akizungumzia mgogoiro wa ardhi uliyokuwepo Lukuvi, amesema aliunda kamati yake ambayo imefanyia kazi malalamiko kwa kuhoji kila mwananchi.
“Niliunda kamati ambayo leo hii ripoti yake ndiyo naitolea maamuzi hapa hili eneo wananchi walivamia na kujenga katika viwanja ambavyo vilikuwa vinamilikiwa kisheria na watu wengine wenye hati,”amesema.
Aidha, amesema kuwa kwa mujibu wa uchunguzi wapo baadhi ya watu ambao waliwauzia wananchi viwanja katika maeneo hayo yenye hati kwa madia kuwa wao ndiyo wamiliki.
Amesema, kutokana na hali hiyo watu wengi walinunua bila kujua kuwa maeneo hayo yalikuwa yanamilIkiwa tayari kisheria na watu wengine.
“Kutokana na hali hii nimeamua kwa wale ambao waliuziwa viwanja bila kujua kuwa ni mali ya watu wengie na kuviendelea wataendelea kubaki hapa lakini watalazimika kulipa gharama za urasimishaji pamoja na kiasi cha fedha kwa ajili ya kuwalipa wale wenye hati ili waende kutafua maeneo mengine,”amesema.
Pia Lukuvi alimwagiza Kamanada wa Polisi na Mkuu wa Takukuru mkoa wa Dodoma kuwakamata watu wote 51, waliohusika katika kuuza viwanja ambayo haikuwa mali yao kinyume na sheria.
“Tatizo la uvamizi katika mkoa wa Dodoma limekuwa kubwa sana hapa kuna watu wao walivamia na kusema kuwa eneo hili ni mali yao bila kujali kuna watu ambao tayari walikuwa na hati kisheria za kumiliki maeneo haya, hawa wote watafutwe na sheria ichukue mkondo wako,”amesema.
Vile vile, aliiagiza hati za viwanja ambavyo wananchi walivamia zipelekwe Wizarani ili zifutwe na wananchi wapatiwa hati za viwanja watakavyopimiwa na kumilikisha kisheria.
Hata hivyo, Waziri Lukuvi alipiga marufuku tabia ya wananchi kujenga bila kuwa na vibali kutoka mamlaka husika.
“Niwaagize Jiji kukagua kila mtaa na kama matakuta nyumba inajengwa bila kibali wekeni alama ya ‘x’ nyekundu, na wenyeviti wa mitaa na vitongoji hawana mamlaka ya kuuza viwanja hata mara moja wakome kabisa kujihusisha na hili jambo,”amesisitiza Lukuvi.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Anthony Mtaka, ameahidi kuyafanyia kazi maagizo yote yaliyotolewa ili kila mwananchi mwenye haki aipate.
Mtaka pia amemtaka Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Jabir Shekimweri, kusimamia zoezi hilo kwa kushirikiana na wataalam wake wa ardhi jiji la Dodoma.
“Mkuu wa wilaya lazima Jambo hili ubebe hasira ya kuhakikisha linafanikiwa wewe kwa kushirikiana na watu wako hatutaki tena leo baada ya maelekezo ya waziri sisi tunarudi hapa kufanya kazi yako, hiyo itaonyesha kuwa hamtoshi katika nafasi zenu,”alisisitiza Mtaka.