Maandalizi ya Sensa nchini yashika kasi, Dodoma na NBS wafanya jambo

Na Doreen Aloyce, Diramakini Blog
 
OFISI ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma kwa kushirikiana na Ofisi ya Taifa ya Takwimu imewakutanisha viongozi, wawakilishi wa Serikali ngazi mbalimbali,makundi ya kijamii,taasisi za dini,umma,binafsi na vyama vya siasa katika kikao cha pamoja kwa lengo la uhamasishaji na utoaji wa elimu ya Sensa ya Watu na Makazi inayotarajiwa kufanyika mwaka 2022 nchini.
Akieleza umuhimu wa kikao hicho, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma,Anthony Mtaka amesema wameandaa kikao hicho na kuyashirikisha makundi hayo ili kurahisisha utoaji wa elimu ya sensa kwa jamii huku akisisitiza kwamba kwa kufanya hivyo zoezi hilo litafanikiwa kama inavyotarajiwa.

Kwa kutambua umuhimu wa zoezi hilo, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,George Simbachawene amewataka watanzania kujitokeza kwa wingi katika zoezi la sensa ya watu na makazi linalotarajiwa kufanyika mwakani ili kuiwezesha Serikali kupanga maendeleo na kukuza uchumi.

Akiongea katika kikao hicho amesema, “Serikali inategemea sana zoezi hili,hatuwezi kuwa na maendeleo bila kujua idadi ya watanzania,kila mmoja kwa nafasi yake anatapaswa kuwa balozi wa uhamasishaji ni muhimu hivyo watanzania wanatakiwa kujitokeza kwa wingi ili kuisaidia Serikali kupanga mipango ya maendeleo”.

Mbali na hayo ametumia nafasi hiyo kumshukuru Mkuu wa Mkoa wa Dodoma,Anthony Mtaka kwa kuona haja ya kuandaa mkutano huo huku akisisitiza kwamba sensa ni muhimu kwani inaleta ushahidi wa kisayansi na maendeleo.
Naye Spika wa Bunge na Mbunge wa Jimbo la Kongwa, Job Ndugai amesema zoezi hilo ni muhimu kwa Taifa kwani litasaidia Nchi kupanga maendeleo hivyo watanzania wanatakiwa kujitokeza kwa wingi katika zoezi hilo.

“Tarehe 31 vikao vyetu vya Bunge vitaanza na vikao vilivyopita tumepitisha mambo mengi ikiwemo na tozo,safari hii itakuwa salama,hili ni jambo muhimu sana hivyo niwaombe watanzania wajitokeze kwa wingi,sisi wagogo hata zoezi la kuhesabu mifugo linakuwa na shida ni utamaduni wetu,”amesema.

Naye Kamisaa wa Sensa nchini ambaye pia ni Spika wa Bunge Mstaafu,Anne Makinda ametoa wito kwa watanzania kujitokeza katika zoezi la kuhesabiwa kwani hilo sio suala la kisiasa na kwamba zoezi hilo watatumia tehama katika maeneo ya kuhesabiwa lengo likiwa ni kuwafikia watanzania wengi ambapo amedai watawafikia watu wengi mpaka katika maeneo ya vijijini.

Makinda amesema wamejipanga kuhakikisha zoezi hilo linafanyika kwa ufanisi kwani kwa sasa wataaalamu wameongezeka tofauti na miaka ya nyuma.

Kutokana na hayo Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dkt. Albina Chuwa amesema Serikali imejipanga kikamilifu kusimamia zoezi la Sensa ya Watu na Makazi inayotarajiwa kufanyika mwakani huku akitoa wito kwa watanzania kujitokeza kwa wingi wakati wa zoezi hilo.

“Sensa hii itakuwa ni ya sita itasimamiwa na Serikali ya awamu ya sita kwa weledi mkubwa tunatarajia watahesabiwa zaidi ya watu milioni 64 kwani kila mwaka watu wanaongezeka milioni 3.1 na sensa mwisho ya mwaka 2012 tulikuwa milioni 49,”amesema.

Amesema kwa sasa wanauzoefu wa kutosha na wamejipanga kuhesabu watu mbalimbali ikiwemo watu wenye ulemavu ambapo ambapo amedai zoezi hilo lipo kwa mujibu wa sheria hivyo ni lazima watu wahesabiwe.

Kwa upande wake,Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Bill Chidabwa ameiomba Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kutoa elimu kwa wananchi kuhusiana na umuhimu wa kuhesabiwa katika zoezi la sensa ya watu na makazi inayotarajiwa kufanyika mwakani ili kuiwezesha Serikali kupanga maendeleo na kukuza uchumi.

Amesema, wao vijana wanaunga mkono zoezi hilo ambapo ameitaka pia NBS mara baada ya zoezi hilo kuja na majibu vijana wapo wangapi na wanatakiwa kupewa kipaumbele kwa kaisi gani.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news