Na Abubakari Akida,MOHA
Madereva wa bodaboda visiwani Zanzibar wametakiwa kufuata Sheria za Usalama barabarani ili kuepusha ajali na vifo vilivyoshamiri chanzo ikiwa kutofuatwa kwa Sheria za Usalama Barabarani.
Rai hiyo imetolewa leo na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi ambae pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Usalama Barabarani, Khamis Hamza Chilo wakati wa kikao na madereva bodaboda wa Mkoa wa Mjini Magaharibi jijini Zanzibar ambacho pia kilihudhuriwa na uongozi wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi.
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, ambae pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Usalama Barabarani, Khamis Hamza Chilo akizungumza na madereva bodaboda (hawapo pichani) wakati wa kikao cha kukumbushana kufiuata Sheria za Usalama Barabarani kilichofanyika leo katika Viwanja vya Polisi Madema Visiwani Zanzibar,kushoto ni Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Kamishna Msaidizi wa Polisi Awadh Juma Haji.
“Serikali yenu Sikivu chini ya Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dkt. Hussein Mwinyi iko katika mchakato ili mruhusiwe kutoa huduma za usafiri katika maeneo mbalimbali ya Zanzibar sasa nawaomba muanze kujifunza na kufuata sheria za usalama barabarani ili tunayoona yanayotokea kule Bara yasitokee huku.
"Kuna mambo kadhaa huku mmeshaanza kuhusishwa nayo kabla hata hamjaruhusiwa nawaombeni jiepusheni na mambo hayo lengo la serikali ni kuwatengenezea mazingira mazuri ya kujiajiri sasa ushiriki katika uhalifu yakiwemo matendo ya uporaji, kukata watu mapanga sio jambo nzuri, jueni tu jeshi la polisi liko macho na halitosita kuwachukulia hatua pindi mtakapobainika kujihusisha na matendo ya uhalifu,” aliongeza Naibu Waziri Chilo.
Akizungumzia takwimu za ajali za bodaboda, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Kamishna Msaidizi wa Polisi Awadh Juma Haji amesema kumekuwepo na kupungua kwa ajali za bodaboda na vifo kutokana na elimu inayotolewa kwa madereva hao wa bodaboda lengo ni kuhakikisha utii wa sheria bila shuruti.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Kamishna Msaidizi wa Polisi Awadh Juma Haji akizungumza na madereva bodaboda (hawapo pichani) wakati wa kikao cha kukumbushana kufiuata Sheria za Usalama Barabarani kilichofanyika leo katika Viwanja vya Polisi Madema Visiwani Zanzibar.(Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi).
“Mwaka huu tuna ajali 17, watu waliofariki mwaka jana ni watu 18 na mwaka huu tuna vifo 17 huku upungufu ukiwa ni mtu mmoja, lakini ajali zilizosababisha majeruhi kwa mwaka jana ni ajali 19 na mwaka huu ni ajali 6 kwa hiyo kuna upungufu wa ajali 15, watu waliojeruhiwa mwaka jana watu 37 na mwaka huu ni watu 6 kwahiyo tunaona kuna kushuka kwa ajali na athari zake,” alisema RPC Awadh.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti katika kikao hicho bodaboda hao waliiomba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa nia ya kuandaa utaratibu ili waweze kuruhusiwa kufanya kazi zao Visiwani hapo huku wakiahidi kuendelea kufuata sheria za usalama barabarani.