MAJALIWA, DKT. MOTSEPE WAJADILIANA KUKUZA MICHEZO

NA MWANDISHI MAALUM

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa leo amekutana na Rais wa Shirikisho la Mpira barani Afrika (CAF), Dkt. Patrice Motsepe na kujadiliana naye masuala muhimu ya kuendeleza michezo nchini.
Akizungumza na Dkt. Motsepe ofisini kwake Mlimwa, jijini Dodoma leo Ijumaa, Agosti 13, 2021, Waziri Mkuu amemweleza mikakati ambayo Serikali inatumia ili kuinua kiwango cha soka nchini.

“Sisi tumeanza kuboresha michezo nchini chini ya mpango unaohusisha Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia; Ofisi ys Rais TAMISEMI na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo. Mpango huu unalenga kuibua vipaji vya vijana kupitia mashindano ya UMITASHUMTA, UMISETA, Vyuo Vikuu na Vyuo vya Kati,” amesema.

Katika mazungumzo yao, walijadiliana suala la kuendelea kutenga bajeti ya kuinua michezo kwa vile nchi nyingi zinashindwa kufanya vizuri kwenye michezo kwa sababu hazitengi bajeti. “Nimemweleza kuwa hapa kwetu kupitia Bunge letu tukufu, tumekuwa tukitenga bajeti hiyo japokuwa tunajua kuwa haitoshelezi mahitaji yote.

“Kuhusu uendelezaji wa michezo nchini, Rais wa CAF ametusihi tuwe na mpango madhubuti wa kupata maeneo ya kufanyia mazoezi, tuwe na viwanja bora vyenye vipimo vya kisasa, jambo ambalo nimemweleza linatekelezwa na shirikisho la soka nchini. Pili, ametutaka tuandae vijana kuanzia umri mdogo, tuwe na taasisi za Serikali na za sekta binafsi zinazofundisha soka, waamuzi, makocha ili tuwaibue akina Samatta wengi zaidi kwani na sisi tunaamini kuwa wapo.”

Kwa upande wake, Dkt. Motsepe amesema katika uongozi wake amelenga mambo makuu matatu ambayo ni haja ya sekta binafsi kuwekeza kwenye michezo na kuongeza udhamini; ujenzi wa vituo vya michezo (sports academies) na vituo vya kuendeleza vijana (youth development centres).

Amesema chini ya mfuko wa dola bilioni moja (One Billion Dollar Fund), amedhamiria kuimarisha miundombinu ya michezo. Kuna baadhi ya nchi za Afrika zina viwanja vikubwa vya michezo lakini havijakidhi vigezo vya FIFA. Tunataka na wao wafikie viwango vya kimataifa,” amesema.

Amesema timu ya Taifa ya Tanzania ina uwezo kuwa timu bingwa barani Afrika kutokana na umahiri walionao hivi sasa na ametumia nafasi hiyo kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa jitihada zake za kuunga mkono michezo nchini ambapo wiki ijayo atapokea kombe la CECAFA -2021 la vijana wenye umri chini ya miaka 23.

Ameipongeza Tanzania kwa kuwa nchi ya kuigwa kutokana na wananchi wake wengi kupenda michezo na hasa kunapokuwa na mechi zinazokutanisha vilabu vikubwa nchini kwa vile zinawaleta mashabiki hata kutoka nchi jirani.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news