NA MWANDISHI DIRAMAKINI
Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro linawashikilia watu sita kwa tuhuma za kuchoma moto mali mbalimbali za serikali.
Mali hizo ni pamoja gari Land Cruser DFP 9402, pikipiki tatu, kompyuta mapakato tatu aina ya HP na mashine ya kuhakiki mashamba, mali za halmashauri.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Fortunatus Musilim ameyathibitisha hayo leo mjini hapa.
Amesema, tukio hilo limetokea katika Kijiji cha Melela Kata ya Chita Wilaya ya Kilombero,ambapo watuhumiwa walitenda kosa hilo baada ya maafisa ardhi kufika katika shamba linalomilikiwa na marehemu Daud Balali ambaye alikuwa Gavana wa Banki Kuu ya Tanzania (BoT).
Kamanda Musilim amesema kuwa, katika tukio hilo dereva aliyefahamika kwa jina la Damas Sanga (51 ) alijeruhiwa baada ya wananchi hao kumkukuta kwenye gari na kuanza kumshambulia sehemu mbalimbali za mwili wake.
Naye Kamishina Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Morogoro, Frank Minzikuntwe amesema vurugu hizo zimetokea baada ya maamuzi ya serikali ya kulipima shamba hilo ili liweze kupangwa upya matumizi yake.
Ni baada ya kutelekezwa kwa muda mrefu huku wananchi wanalolizunguuka wakikosa maeneo ya kulima.
DIRAMAKINI Blog imeelezwa kuwa, mwekezaji mmoja aliuziwa shamba hilo na kijiji mwaka 2001 kwa makubaliano ya kuwajengea zahanati, shule na huduma za maji.
Aidha, mwekezaji huyo kwa zaidi ya miaka 20 hakutekeleza makubaliano hayo ndipo ulipozuka mgogoro wa wananchi kutaka warejeshewe shamba hilo ili waliendeleze.
Hata hivyo, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Martine Shigella baada ya tukio hilo amesitisha shughuli zote za upimaji kwa upande wa mwekezaji.