Na Yusuph Mussa, Bumbuli
MBUNGE wa Jimbo la Bumbuli mkoani Tanga January Makamba ametoa msaada wa vitanda 20 vyenye thamani ya sh. milioni nne (4) ili kuwanusuru wasichana waliokuwa wanalala chini kwenye bweni la wasichana Shule ya Sekondari Soni iliyopp Halmashauri ya Bumbuli, Wilaya ya Lushoto.
Mbunge wa Jimbo la Bumbuli mkoani Tanga January Makamba (kulia) akizungumza na wanafunzi wa Shule ya Msingi Msongolo iliyopo Kijiji cha Wena Kata ya Dule B, ambapo amenunua rola sita za mabomba ya maji zenye thamani ya sh. 780,000 ili kupeleka maji kwenye shule hiyo. Ni baada kumlalamikia kuwa wanapata shida ya maji kwa kila asubuhi wanafunzi kwenda na ndoo za maji shuleni (kama zinavyoonekana kwenye picha). (Picha na Yusuph Mussa).
Alitangaza kutoa msaada huyo Agosti 2, 2021 baada ya kutembelea shule hiyo iliyopo Tarafa ya Soni, na kuagiza utengenezaji wa vitanda hivyo ambavyo vitabeba wanafunzi 40 kati ya 47 waliopo kwenye bweni hilo, uwe umekamilika baada ya wiki moja.
"Mkuu wa Shule (Ally Lwena) nataka hivi vitanda viwe vimekamilika baada ya wiki moja. Nia yangu nataka hawa wanafunzi waweze kuvitumia. Hatuwezi kuacha kununua vitanda tukiacha mabinti zetu wakiteseka kwa baridi kwa kulala chini," alisema Makamba.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Mkuu wa Shule hiyo ambayo ina wanafunzi mchanganyiko wa kutwa na bweni, Lwena, alisema mabweni mawili ya wasichana yaliungua moto mwaka 2016, ambapo hadi leo chanzo chake hakijajulikana, na tangu wakati huo wanafunzi hao wanalala kwa kutandika magodoro chini.
Mbunge wa Jimbo la Bumbuli mkoani Tanga January Makamba (kulia) akikabidhi sh. milioni 1.4 kwa Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Wena Mbazi Shemntambo (wa pili kushoto) kwa ajili ya ujenzi wa Zahanati ya Wena. Wengine ni Diwani wa Kata ya Dule B Ali Mkwavinga (wa pili kulia) na Mwenyekiti wa Kijiji cha Wena Hamidu Mntangi (kushoto). Alikabidhi fedha hizo kwenye mkutano wa hadhara Agosti 2, 2021 uliofanyika Kijiji cha Wena. (Picha na Yusuph Mussa). "Tumemueleza mheshimiwa tunao wasichana 47 kwenye bweni lile na wote wanalala chini, lakini tukipata vitanda 20, vitawasaidia wasichana 40. Tulijikuta kwenye matatizo makubwa baada ya mabweni yetu mawili kuungua moto mara mbili mwaka 2016. Na tangu wakati huo hatujajua chanzo chake, lakini tayari uchunguzi unaendelea na upo mikononi mwa vyombo vya usalama.
"Hata katika kujihami, bweni lile wanaloishi wasichana, pamoja na kuwa shule yetu ina umeme, tumeshindwa kuliweka umeme kwa ajili ya kulinda usalama wao, na wanatumia Solar kule ndani," alisema Lwena wakati akizungumza na mwandishi wa habari hizi.
Akiwa kwenye Kata ya Dule B, kwenye mkutano wa hadhara Kijiji cha Wena, Tarafa ya Bumbuli, Makamba alichangia kwa kutoa papo hapo fedha taslimu sh. milioni 1,600,000 kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya Wena baada ya kuona wananchi wameshakusanya nguvu zao kwa michango ya fedha na vifaa vya ujenzi ikiwemo mchanga na mawe.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Mpalai, Kata ya Dule B Hemed Hassan (kushoto) akimshukuru Mbunge wa Jimbo la Bumbuli mkoani Tanga January Makamba (kulia) baada ya kukabidhiwa sh. milioni moja na Mbunge huyo Agosti 2, 2021. Makamba alitoa fedha hiyo ili kuendeleza ujenzi wa Shule ya Msingi Mpalai iliyopo Kata ya Dule B ambayo inaanza kama shikizi kwa ajili ya wanafunzi wa darasa la kwanza na pili, ambayo inajengwa madarasa mawili na ofisi ya walimu, na sasa imefikia hatua ya linta. Na alifika hapo kukagua ujenzi wake. Kabla ya hapo, Makamba alitoa bati 50 kupitia Mfuko wa Jimbo zenye thamani ya sh. milioni 1,475,000. (Picha na Yusuph Mussa). Katika fedha alizotoa, sh. 960,000 ni kwa ajili ya kununua mifuko 60 ya saruji na sh. 40,000 kusafirisha mifuko hiyo, na sh. 600,000 ni kumlipa fundi kwa ajili ya ujenzi wa msingi wa zahanati hiyo. Pia amenunua rola sita zenye thamani ya sh. 780,000 kwa ajili ya kupeleka maji Shule ya Msingi Msongolo iliyopo Kijiji cha Wena, Kata ya Dule B.
Katika Shule ya Msingi Mpalai (Shikizi) ambayo itaanza kusoma watoto wa darasa la kwanza na pili, na tayari imefikia usawa wa madirisha, Makamba amechangia fedha taslimu sh. milioni moja papo hapo kwa ajili ya kukamilisha vyumba viwili vya madarasa na ofisi moja ya walimu. Kabla ya hapo, kupitia Mfuko wa Jimbo alitoa bati 50 zenye thamani ya sh. 1,475,000.
Mtendaji wa Kata ya Dule B Akarelia Leandry alimueleza Mbunge, ili kukamilisha vyumba viwili na ofisi kunahitajika mifuko ya saruji 50, bati 100 na pesa ya fundi sh. 950,000, ambapo Makamba aliahidi ataendelea kutoa fedha na vifaa hadi kukamilisha ujenzi huo.
Akiwa katika Kijiji cha Mbelei, Kata ya Mamba, ambapo aliweza kuzungumza na Halmashauri Kuu ya CCM Kata ya Mamba, alisema hatua waliyofikia kwenye Jimbo la Bumbulo ni vitongoji kutokuwa na umeme na sio vijiji. Ni baada ya viongozi wa kata hiyo kulalamika kuwa vijiji vyao vinne (4) vyote vina umeme, huku baadhi ya vitongoji vikiwa na umeme, lakini vingine havijafikiwa na huduma hiyo.
Mbunge wa Jimbo la Bumbuli mkoani Tanga January Makamba (wa tatu kushoto) akikwea mlima kwenda kukagua ujenzi wa nyumba ya walimu yenye uwezo wa kuishi familia mbili (inayoonekana pichani) Shule ya Sekondari Mbelei yenye kidato cha kwanza hadi cha sita. Nyumba hiyo inajengwa kwa gharama ya sh. milioni 50. (Picha na Yusuph Mussa).
Mbunge wa Jimbo la Bumbuli mkoani Tanga January Makamba (kushoto) akipata maelezo kutoka kwa Kaimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Mbelei iliyopo Kata ya Mamba Marieta Samwel (kulia). Makamba alifika shuleni hapo kukagua ujenzi wa Bwalo la shule hiyo ambalo limejengwa kwa sh. milioni 130, na bado halijakamilika. (Picha na Yusuph Mussa).
"Kama ningeweza kuja na baadhi ya wabunge wenzangu, halafu wakawasikia mnalalamikia kukosa umeme kwenye baadhi ya vitongoji wangewashangaa! sababu katika nchi hii kuna baadhi hata tarafa nzima haijapata umeme achilia mbali kata, vijiji na vitongoji. Ninachoomba kuweni na subira, kwani umeme utafika kwenye vitongoji vyote kwa vile itakuwa ni rahisi zaidi umeme kufika kwenye vitongoji sababu kwa sasa upo kwenye vijiji.
"Wakati naanza ubunge (mwaka 2010) Jimbo la Bumbuli lenye kata 18 na vijiji 83, ni kata nne (4) tu ndizo zilikuwa na umeme ambazo ni Soni, Bumbuli, Mponde na Mamba. Lakini tunapozungumza sasa hivi, ni kata tatu tu ndizo hazina umeme, ambazo ni Kisiwani, Milingano na Kwamkomole. Kama tungemualika mwananchi wa Kata ya Kisiwani kwenye kikao hiki, ambaye hajawahi kuona nguzo ya umeme kwenye kata nzima, halafu wewe unadai umeme kwenye kitongoji, nadhani angekushangaa," alisema Makamba.
Katika Shule ya Sekondari Mbelei, ambapo alitembelea kuona mradi wa bwalo la shule hiyo ambalo limegharimu sh. milioni 130 na bado halijakwmilika, Makamba aliahidi kuwanunulia Projector.