Mjumbe wa Baraza la UWT Taifa Mkoa wa Mara, Rhobi Samwelly awapa neno Wanawake

Na Fresha Kinasa, Diramakini Blog

MJUMBE wa Baraza la Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Taifa Mkoa wa Mara, Rhobi Samwelly amesema ataendelea kushirikiana na wanawake wa jumuiya hiyo mkoani humo katika kuhakikisha kwamba, maendeleo ya jumuiya yanazidi kuimarika na Wanawake wanakuwa na uchumi imara, kwa kuibua miradi na fursa mbalimbali za kiuchumi katika maeneo yao.
Mjumbe wa baraza la UWT Taifa Mkoa wa Mara Mara, Rhobi Samwelly akizungumza na Wajumbe wa Baraza la UWT Wilaya ya Tarime Agosti 26, 2021 kulia kwake ni Mwenyekiti wa UWT Wilaya ya Tarime, Joyce William.
Amesema, Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) imekusudia kuwainua Wanawake na Watanzania wote kuhakikisha wanakuwa na maendeleo chanya. 
Hivyo amesema wanawake wana mchango mkubwa wa maendeleo kuanzia ngazi ya familia na taifa pia. Ambapo ameahidi kuendeleza ushirikiano na umoja miongoni mwa wanawake ili kufikia maisha bora.

Rhobi ameyasema hayo Agosti 26, 2021 wakati wa kikao cha kawaida alipokuwa akizungumza na Wajumbe wa UWT Wilaya ya Tarime alipofika kujitambulisha wilayani humo baada ya kuchaguliwa na Wajumbe wa baraza hilo kufuatia kifo cha aliyekuwa mtangulizi wake,  Christina Samo.
Ambapo amesisitiza kuwa, jumuiya hiyo ina jukumu la kumuunga mkono kwa dhati Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kwa kufanya kazi za maendeleo sambamba na kusomesha Watoto wa kike ambao wana mchango katika uchumi wa jamii na taifa kwa ujumla.

"Lazima tushirikiane kwa pamoja kuchochea maendeleo ya jamii na taifa letu, tushiriki kukijenga chama kwa kuingiza wanachama wapya kutoka vyama vingine. Kazi nzuri zinazofanywa na Rais Samia ambaye ni kiongozi mwanamke lazima tumuunge mkono kinamama, tuwasomeshe Watoto wa kike na tupinge vitendo vya kikatili kwa maendeleo ya Wanawake wa Mkoa wa Mara na taifa pia," amesema Rhobi.

Aidha, Rhobi ameahidi kushirikiana na Wanawake wa UWT mkoani humo katika kutetea haki zao hususani kuondoa mila kandamizi ambazo haziruhusiwi na serikali na Chama Cha Mapinduzi kwa Ustawi bora wa Maendeleo na hivyo amewaomba Wanawake kuripoti matukio ya kikatili na kutowafumbia macho wanaobainika kujihusisha na vitendo hivyo ili Serikali iwachukulie hatua.

Katika Hatua nyingine, Rhobi amewahimiza wajumbe wa (UWT) Wilaya ya Tarime kuchanja chanjo ya (UVICO-19) Katika kukabiliana na janga la Corona ambapo amewaomba watambue kuwa chanjo ni Salama na haina madhara yoyote. Na pia akawasisitiza wasikubali upotoshwaji unaofanywa na baadhi ya watu wa chache kuhusiana na Chanjo. Huku pia akiwasisitiza kujitokeza kwa wingi kujiandikisha kwa mfumo wa TEHAMA.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa UWT Wilaya ya Tarime, Joyce William amewaomba wajumbe wa baraza hilo Wilayani humo kumpa ushirikiano wa dhati katika kuhakikisha chama kinapiga hatua na kufikia malengo chanya kwa ufanisi.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Tarime,Marema Soro akizungumza jambo kwa Mjumbe wa Baraza la UWT taifa Mkoa wa Mara Rhobi Samwelly (katikati) na Mwenyekiti wa UWT Wilaya ya Tarime,Joyce William.

Kwa upande wake Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Tarime, Marema Solo ameiomba jumuiya hiyo kuendeleza mshikamano wa dhati pamoja na kukitumikia chama kwa uaminifu katika maeneo yao kwa kuyasema mazuri yote ambayo yanatekelezwa na Chama Cha mapinduzi na kulipa ada za chama kwa wakati.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Tarime, David Ngicho amesema Wana CCM wanapaswa kutembea kifua mbele na kujivunia mafanikio mbalimbali ambayo yametekelezwa na Serikali ya chama Cha Mapinduzi ikiwemo miradi mbalimbali ya kimkakati maeneo mbalimbali nchini.

"Rais Samia kaonesha kinamama wanaweza kwa uongozi wake mzuri, kazi anafanya kila mmoja anashuhudia. Kinamama muendelee kukisemea chama kwa wananchi, kuvaa sare za chama bila kuogopa, fanyeni kazi za maendeleo ambazo zitakuza uchumi wenu. naamaini chama kitaendelea kuongoza kwa sababu CCM imejipanga vyema kuwatumikia Wananchi tushikamani, tushirikiane na kupendana kwa dhati." amesema Ngicho.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news