Na Fresha Kinasa, Diramakini Blog
Serikali imeshauriwa kuangalia mitaala ya elimu iliyopo kwa sasa na kuona namna bora ya kuifanyia marekebisho kusudi iendane na mazingira ya eneo husika ambayo wanafunzi wanatoka.
Hatua ambayo itasaidia kukabiliana na mazingira wanayoishi na kuchochea ubunifu na maendeleo ndani ya jamii na Taifa kwa ujumla.
Ushauri huo umetolewa na Kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Musoma Mjini, Mwalimu Makuru Lameck Joseph wakati akizungumza na Diramakini Blog Mjini Musoma.
Ambapo alisema Serikali ina wajibu wa kuangalia njia bora ya utunzi wa mitihani isiwe ya Kitaifa bali iwe ya kikanda kutokana na mazingira ambayo mwanafunzi anatoka ukanda huo husika hali ambayo itasaidia mwanafunzi kumpima kulingana na mazingira yake na yale aliyofundishwa eneo husika.
Mwalimu Makuru amesema kuwa, mitaala ya sasa itambue pia vipaji na talanta za wanafunzi ambazo Mwenyezi Mungu amewajalia, kwani pasipo kuzitambua mitaala hiyo ni kazi bure maana haitakuwa na tija katika jamii na Taifa.
Akisisitiza mitaala itakayoandaliwa ijali vipaji na talanta kupitia mitaala hiyo ya Serikali ikiwemo viwanja vizuri vya michezo shuleni, pamoja na kuajiri walimu wa michezo wenye talanta na vipaji katika kuviibua na kuviendeleza kwa manufaa ya Taifa, kwani michezo na talanta kwa sasa hivyo itaisaidia Serikali kutatua bomu na wimbi kubwa la ukosefu wa ajira nchini.
"Mfano wanafunzi wa Kanda ya Ziwa wanapaswa kuwa na mtaala mahususi kulingana na eneo hilo na mazingira waliyomo, mathalani Kanda ya Ziwa ina maziwa, mito mingi, maeneo ya uchimbaji madini, ardhi yenye rutuba, hivyo mitaala inapaswa ijikite katika nyanja hizo na mitihani yao iendane na mazingira yao na isiwe ya Kitaifa.
"Kanda ya Kusini pia wawe na mitihani yao inayoendana na mazingira na mitaala iendane na mazingira yao tofauti na kanda zingine,"amesema Mwalimu Makuru.
Ameongeza kuwa, fursa zilizopo Kanda ya Ziwa haziwezi kuendana na Kanda ya Kati, Nyanda za Juu Kusini, Kanda ya Magharibi kwa hiyo kuwapa mtihani mmoja wa Kitaifa ni kuwanyima fursa na ubunifu ambao wangeutumia kulingana na maeneo yao jambo ambalo lingeongeza chachu katika jamii na Taifa kwa ujumla.
Pia, Mwalimu Makuru ameishauri Serikali kupitia Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia kupunguza idadi ya masomo kwa wanafunzi kwa hivi sasa kwani wanapaswa kuwa na masomo machache kulingana na eneo husika ili yakidhi mahitaji ya wanafunzi, jamii na vipaumbele vya eneo husika badala ya kuwapa masomo mengi yasiyoendana na mahitaji ya maeneo yao na changamoto zilizopo katika maeneo hayo.
Amesema, kitendo cha wanafunzi kuwa na idadi kubwa ya masomo huwafanya wanafunzi kukariri masomo badala ya kuelewa ambapo mwisho wa siku wanapohitimu masomo yao hukosa ubunifu, umahiri na ubobezi wa kitaalamu na hivyo kukosa wasomi wenye tija ambao wangeleta mapinduzi chanya katika maeneo yao na Taifa kwa ujumla.
Ameiomba Serikali, kutumia lugha ya Kiswahili katika kufundishia masomo katika mitaala kwani Kiswahili mwaka 1963 baada ya Uhuru, kilithaminishwa kutumika katika lugha ya kufundisha na kujifunza katika elimu ya msingi peke yake, huku katika elimu ya sekondari na elimu ya juu lugha ya Kiingereza ikiendelea kutumika katika mitaala ya elimu ya juu.
Jambo ambalo limekuwa kikwazo katika elimu hapa nchini kutokana na wengi kutoelewa lugha, kwani misingi yao ilianza katika lugha ya Kiswahili.
"Wengine hukata tamaa na kuacha masomo kutokana na lugha ya Kiingereza kuwa ngumu pindi wanapojiunga na elimu ya sekondari. Kutumia lugha isiyokuwa mama ni kuondoa ubunifu na uwezo thabiti wa mwanafunzi kuelewa somo fulani au jambo fulani.
"Nishauri Serikali kubadili mitaala iwe na lugha moja ya kufundishia na kujifunza ambayo ni Kiswahili, kwani hata nchi zilizoendelea, zenye teknolojia kubwa na maendeleo makubwa lugha zao za kufundishia ni lugha mama mfano China, Burma, Singapore hizo nchi elimu yao ni bora na yenye tija na ndio maana zimepiga hatua. Serikali iliangalie jambo hili kwa mapana na kina,"amesema Mwalimu Makuru.
Katika hatua nyingine, Mwalimu Makuru ameishauri Serikali kuanza kulifundisha somo la historia ya Tanzania kama ambavyo mpango huo ulivyokuwa hapo awali, kwani mpaka sasa kumekuwepo ukimya ambao unaleta mashaka miongoni mwa wananchi, wanafunzi na walimu kwani ukimya huo umezidi kuleta maswali mengi katika jamii nini kinachoendelea? Kuhusu somo hilo la historia ya Tanzania kufundishwa shuleni.
"Kama bado wanafunzi wanafundishwa historia ya nchi zingine na mambo mengine ya nchi hizo mfano kilimo cha mahindi duniani ni Marekani, kilimo cha migomba Jamaica, kilimo cha mpunga Burma, kwani hayana tija kwa wanafunzi wetu hivi sasa hususani nchini ingefaa sana wanafunzi wafundishwe kutokana na mazingira ya nchi yetu mfano kilimo cha chai Kagera.
"Kilimo cha mahindi Sumbawanga, Ruvuma na Iringa. Iweje somo la historia ya Tanzania lishindwe kuanza kufundishwa na wakati tayari lilikuwa limekwishaandaliwa na lingeanza kufundishwa mwaka huu katika mitaala ya elimu yetu Tanzania,"amesema Mwalimu Makuru.
Mwalimu Makuru amesisitiza wanafunzi kufundishwa masomo kulingana na maeneo yao na ustawi mzuri wa kila zao mkoa na wilaya husika wayatambue, badala ya mambo ya Kitaifa na Kimataifa huku akisisitiza pia mitaala ya chini iendane na mazingira na kwa elimu ya juu pawepo na mtaala mmoja ambao utawaunganisha wasomi wote kwa pamoja kuonesha ubobezi wao katika fani zao mbalimbali na kuongeza tija kwa Taifa kiuchumi.
Amesema kuwa, ana imani na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan jambo hilo italifanyia kazi kwani lina afya kwa maendeleo ya nchi hasa ikizingatiwa kuwa, elimu ni dira, ufunguo kwa maendeleo ya jamii na nchi kwa ujumla.
Pia alisema, mitaala inatakiwa ijikite zaidi katka vitendo kuliko nadharia kusudi iweze mitaala kuwajengea wanafunzi weledi na ujuzi zaidi katika masomo na mwisho tuweze kupata wataalamu wa kutosha na wabobezi katika fani mbalimbali hapa nchini.
Mwalimu Makuru alimalizia kwa kusema kuwa, cheo ni dhamana, hivyo kila mmoja hapaswi kutumia cheo chake au cha mtu mwingine kwa manufaa yake mwenyewe.
"Mwenyenzi Mungu isaidie elimu yetu ya Tanzania iwe na mantiki na ilete ufanisi katika jamii yetu na Taifa kwa ujumla,ibariki Tanzania, ibariki Afrika,"amesema.