Mwalimu Makuru atoa darasa wanaopotosha kuhusu chanjo, atoa onyo

NA AMOS LUFUNGILO, Diramakini Blog

Kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Musoma Mjini mkoani Mara, Mwalimu Makuru Lameck Joseph amewandoa hofu wananchi juu ya habari zinazosambazwa mitandaoni kuhusiana na chanjo ya Corona, huku akiwataka kuzipuuza na kutumia fursa iliyopo kila mmoja kwenda kuchanjwa ili aweze kujikinga dhidi ya virusi vya Corona (COVID-19).
Mwalimu Makuru ameyasema hayo mjini Musoma alipokuwa akiongea na wandishi wa habari huku akisisitiza kuwa, hatua ya Serikali kutuletea chanjo ni ya kupongezwa kwa kuwa, tiba ya kisayansi na kuendelea kumuomba Mungu ni bora zaidi kuliko kutumia njia zingine ambazo bado zipo katika tafiti.

Amesema, kwa hapa tulipofikia katika ugonjwa wa Corona hatuna budi kujua Serikari kitu inachofanya ni kutafuta njia za kusaidia watu wake juu ya gonjwa hilo hatari ili waweze kuwa salama.

"Kwani njia ambazo Serikari ilikuwa ikizitumia hapo awali zilikuwa ni tofauti ukilinganisha na sasa ambapo mlipuko wa wimbi la tatu umekuwa na kasi kubwa, hivyo ni vema kuendelea kuzingatia miongozo yote inayotolewa na Serikali yetu,"amesema Mwalimu Makuru.

Amesema, njia ambazo huko nyuma zilikuwa zinatumika juu ya mapambano dhidi ya Corona kama vile uhamasishaji wa matumizi ya dawa za asili kama kunywa na kujifukiza (kupiga nyungu) zinaweza kuendelea, lakini ni bora zaidi kila mmoja ambaye anakidhi vigezo vilivyowekwa na Serikali akafika kupata chanjo.

Mbali na hayo, Mwalimu Makuru ameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuruhusu chanjo kuingia nchini na kila Mtanzania ambaye yupo tayari kwenda kuchanja.

"Hii hatua ya Serikali ya Awamu ya Sita katika kupambana na huu ugonjwa kwa kutumia mbinu za kisayansi ni muhimu sana, maana huko ndiko Dunia inataka twende wote, kwani baada ya kujiridhisha ubora wa chanjo, tumeona Mheshimiwa Rais Samia alianza kwa kuchanjwa, hivyo kutuongoza njia.

"Mafanikio ya chanjo hii ya kisayansi ni mengi, kwa sababu awali tulishuhudia mateso ambayo wafanyabiashara na ndugu zetu ambao walikuwa wanasafiri nje ya nchi walikuwa wakiyapitia kwa kuwa tu hawajachanjwa.

"Wafanyabiashara wengi walilazimika kutoa fedha nyingi kupata chanjo wakati wakiingia nchi hizo, lakini sasa wanapata chanjo bure tena katika maeneo yao, hivyo juhudi hizi zinafaa kupongezwa sana na kila mmoja wetu,"amesema Mwalimu Makuru.

Mwalimu Makuru pia amewatahadharisha viongozi wa kisiasa wakiwemo viongozi wa chama juu ya kauli zao kuhusu mpambano dhidi ya Corona ambapo alisema, kwa sasa kumekuwa na malumbano na hali ya sintofahamu juu ya ujio wa chanjo ya corona, kwani kuna baadhi ya viongozi wamekwenda kinyume kwa kutaja madhara ya chanjo hiyo bila utafiti na uthibitisho wa kutosha, hivyo kuwatia hofu wananchi juu ya matumizi ya chanjo hiyo.

Aidha, Mwalimu Makuru amehitimisha kwa kuwaasa wananchi juu umuhumu wa kujitokeza kwa wingi ili waweze kupewa chanjo.

Pia amewashauri viongozi wa Serikari na wabunge na viongozi wa dini juu ya kuwa mstari wa mbele katika kutoa elimu na uhamasishaji kuhusu chanjo hiyo.

"Pia ukweli unatabia kubwa nzuri sana katika jamii,kwani huwa haujali mkubwa,mdogo,mwenye uongozi au asiyekua na uongozi,mwenye pesa au asiyekua na pesa, rafiki au adui,mwenye dini au asiyekua na dini,kwani ukweli kwake watu wote ni sawa,yaani ukweli siku zote hutenda haki.

"Aidha,una tabia ya kujilipiza kisasi kama ukipuuzwa na viongozi kwa kauli zao zinazochanganya wananchi na kufanya wananchi wasijue cha kufanya na hilo ni pigo kubwa katika Taifa, lazima lishungulikiwe mapema hususani tunapokuwa kwenye mapambo ya hili janga kubwa la Corona, tuwe kitu kimoja katika kuunganisha jamii na kwa umoja huo twendeni tukachanje ili tuwe salama,"amefafanua Mwalimu Makuru.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news