NA FRESHA KINASA
Kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Musoma Mjini, Mwalimu Makuru Lameck Joseph amewashauri viongozi na watumishi wa taasisi mbalimbali za umma kuwa wabunifu ili kuwaletea wananchi na Taifa maendeleo.
Mwalimu Makuru amesema, kwa sasa kuna haja ya Serikali kupitia wizara zake hususani Wiraza ya Maliasili na Utalii na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kuja na njia mbadala zinazoweza kuitangaza Tanzania ili kuweza kuiongezea nchi kipato na wananchi kwa ujumla.
Ameyasema hayo leo Agosti 22, 2021 mjini Musoma mkoani Mara wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na tija iliyopo katika ubunifu ili kuliwezesha Taifa kusonga mbele kiuchumi.
"Wizara ya Maliasili na Utalii inapaswa kuwa mstari wa mbele kwa ubunifu, mfano kwa kufufua historia ya nchi hususani maeneo ya kihistoria ambayo yalitumika kipindi cha mapambano dhidi ya ukoloni barani Afrika ambapo kitovu cha mapambano kilikuwa nchini Tanzania.
"Maeneo ya Kongwa, Mazimbu na maeneo ya Kusini mwa Tanzania kulikuwa na makambi ya wapigania Uhuru wa Bara la Afrika. Hivyo kuna haja kwa Serikali kupitia wizara na taasisi zake kuandaa makongamano makubwa nchini Tanzania ambayo yatawakaribisha wageni mbalimbali na viongozi mbalimbali toka bara zima la Afrika kuja kuangalia na kujifunza juu ya historia ya mapambano dhidi ya ukoloni yaliyosaidiwa na Tanzania.
"Kwa kufanya hivyo, kutaitangaza nchi pia na kuiongezea nchi na wananchi kipato kutokana na makongamano hayo ya kihistoria yatakayokuwa yanafanyika mara kwa mara nchini Tanzania,"amesema Mwalimu Makuru.
Pia amesema, kutokana na makongamano hayo yatasaidia vijana wa Afrika na Waafrika kwa ujumla kujua historia ya mapambano dhidi ya ukoloni pia itawasaidia vijana wa bara la Afrika kujua wapi walipotoka na wapi walipo na wapi wanapaswa kwenda?.
"Itasaidia kuleta chachu ya viongozi wazalendo barani Afrika na kuondoa na kupunguza migogoro ya kisiasa barani Afrika na pia itailetea heshima nchi kwa mchango wake wa ukombozi wa Bara la Afrika,"ameongeza Mwalimu Makuru.
Wakati huo huo amesema kuwa,Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo wanapaswa kuandaa mashindano mbalimbali kupitia vyama mbalimbali vya michezo ili iweze kuitangaza nchi na kuisaidia nchi kuongeza kipato na ajira kwa wananchi.
Amesema, kupitia michezo mbalimbali itakayokuwa imeandaliwa nchini kupitia vyama vya michezo mbalimbali vitafungua fursa za kiuchumi na kuboresha viwango vya michezo nchini.
Mwalimu Makuru ameongeza kuwa, pia wizara inapaswa kuwekeza katika michezo ya utamaduni na sanaa ili kuweza kuisaidia vijana kujiari katika michezo na kuongeza kipato kwa wanatanzania kupitia michezo.
Amesema, ameshanganzwa sana ushiriki wa wanamichezo wa Tanzania katika mashindano makubwa duniani yaliyokuwa yakifanyika mfano mashindano ya OLIMPIKI, Tanzania ilipeleka washiriki watatu tu na wachezaji wawili ambao mmoja alikuwa anarusha tufe na mmoja kurusha kisahani.
"Ukweli ili ni jambo la kusikitisha sana nchi kubwa kama Tanzania inakosa washiriki wa kutosha na kushindwa kupata medali yoyote ile, hivyo wizara na vyama vya michezo wanatakiwa kujitathimini,"amesema.
Ameongeza kuwa, nchi kama ya Rwanda imekuwa ikiandaa michezo mbalimbali lengo ni kuitangaza
nchi ya Rwanda ili iweze kutembelewa na wageni mbalimbali mfano mwaka huu wameandaa mpira wa kikapu barani Afrika ambapo Watanzania hawakuonekana katika hiyo ligi iliyofanyika Rwanda, kwani ilikuwa ni fursa kwa vijana wa Tanzania ambao wangekuwa na vipaji vya kucheza mpira wa kikapu.
"Maana mashindano hayo yalioneshwa na vyombo mbalimbali duniani, hivyo ilikuwa ni fursa kwa watanzania kuonekana, hivyo naomba wizara na vyama vya michezo kuliangalia suala la michezo kwa mapana ili muweze kusaidia Taifa, kwani ndiko kumebaki na fursa kubwa kwa ajira kwa vijana,"amesema.
Katika hatua nyingine, Mwalimu Makuru ameiomba Serikali kutekeleza mpango wake uliokuwa umeanza kuhusu somo la historia ya Tanzania kufundishwa katika ngazi zote kama ilivyokuwa imepangwa na Serikali, "kwani hivi sasa tunaona imekuwa ni kimya, wakati Serikali ilitumia gharama kuliandaa. Hivyo naiomba Serikali itoe tamko rasmi juu ya somo la historia ya Tanzania,"amesema.
Mwalimu Makuru alimalizia kwa kusema kuwa, “Binadamu wote ni ndugu zangu na Afrika ni moja na Dunia moja sema maendeleo ndio hatufanani ila binadamu wote ni sawa kwa Mwenyezi Mungu. Abraham Lincon wa Marekani ambaye alitafasiri demokrasia alisema kwamba, ni Serikali ya watu, kwa ajili ya watu na iliyobuniwa na watu wenyewe. Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika,"amesema.
MUHIMU
UNATAMANI DIRAMAKINI BLOG TUWE HEWANI SAA 24 KUKUPA HABARI ZA KINA KILA DAKIKA, TUNAOMBA UTUUNGE MKONO KWA KUCHANGIA GHARAMA ZA MAWASILIANO NA INTANETI KWA WAANDISHI WETU POPOTE WALIPO NDANI NA NJE YA TANZANIA; TUNAPOKEA MCHANGO WAKO KUPITIA 0719254464 (Tigo Pesa-Godfrey Nnko) AU UKIHITAJI NAMBA YA BENKI TUJULISHE. MUNGU AKUBARIKI SANA KWA SAPOTI YAKO. ASANTE