Na Mwandishi Wetu,Mara
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mara, Samuel Kiboye (No.3) amesema kuwa, wana CCM wote ambao wanamuombea mabaya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan hayatamfikia badala yake yatawarudia wenyewe.
Amesema kuwa,Mungu ameweka kusudi jema ndani Rais Samia ili kuipeleka Tanzania katika ustawi bora wa kiuchumi.
"Watambue tu kwamba, wanaomuombea mabaya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, wataumbuka na yatawarudia wenyewe, kila siku tunasimama katika maombi kumuombea na kila amtegemeaye Mungu kwa ajili ya kuwaombea viongozi wa Serikali na Taifa lake, Mungu uonekana.
"Bado natafakari ni kwanini gazeti la uhuru limeandika habari kama hii.Pia ni nani yuko nyuma yao, niliwahi kusema kuna watu wana macho mekundu wanamuonea Rais wivu na wako ndani ya CCM na utakuta kuna mafisadi wameamua kuunda mipango yao ili wamdhoofishe Rais wetu.Nasema hawataweza hata siku mmoja;
Mheshimiwa Kiboye ameyasema hayo mjini hapa wakati akizungumza na waandishi wa habari kuelezea namna ambavyo umakini unahitajika katika kuwasilisha na kusikiliza taarifa mbalimbali zinazotolewa na viongozi wa nchi akiwemo Rais.
"Sasa niliposoma gazeti lile (Uhuru) nikafanya marejeo ya hotuba ya Mheshimiwa Rais katika mahojiano na BBC sikuona mahali alipotaja kuwa, hana wazo la kuwania urais 2025 nikashtuka, kumbe yale,labda kwa kujisahau au kwa makusudi waliamua kuyapitisha ili kutuumiza miyoyo yetu, ninaamini hatua zitachukuliwa maana chama chetu ni sikivu na waliotenda kosa hilo kubwa ni chombo cha chama, hivyo nichukue nafasi hii kuwataka wale wote wenye nia mbaya na Rais waache mara moja.
"Inawezekana kuna mipango na mbinu nyingi, maana mafisadi huwa wana kila dalili ya kujipenyeza mahali ili kutaka kuvuruga mfumo mzuri wa Serikali, hivyo niwaambie tu wasahau kuwa, waliyoyakusudia hawatayaweza," amefafanua Kiboye.
Pia Kiboye amewataka Watanzania kuendelea kuchapa kazi na kuyapuuza malengo mbalimbali ya wenye nia mbaya na Serikali kwa dhamira ya kudhoofisha juhudi za kuwaletea maendeleo.