Naibu Waziri Dkt.Mabula azindua mradi wa nyumba za makazi Mara

Na Fresha Kinasa, Mara

NAIBU Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi,Dkt. Angeline Mabula amezindua mradi wa Nyumba za Makazi zilizojengwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) eneo la Buhare Manispaa ya Musoma.

Pia ameielekeza Bodi ya Shirika la Nyumba la Taifa kwa kushirikiana na shirika hilo kujenga shule ya msingi ya Serikali na zahanati katika eneo hilo.

Amesema, kujengwa kwa shule hiyo kutasaidia wanafunzi kusoma karibu na eneo hilo. Huku zahanati akisema itawawezesha pia kupata huduma za matibabu karibu nao. Dkt.Mabula amesisitiza kuwa, pia miradi mipya ya nyumba itakayojengwa na NHC iwe na uzio kwa ajili ya kuimarisha usalama.

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Angeline Mabula (katikati) akikata utepe kuashiria uzinduzi wa nyumba za makazi zilizojengwa na NHC eneo la Buhare Manispaa ya Musoma. Uzinduzi huo umefanyika leo Agosti 6, 2021 kulia kwake ni Mkurugenzi wa NHC,Dkt. Maulidi Banyani. (Picha na Fresha Kinasa).

Mheshimiwa Mabula meyasema hayo leo Agosti 6, 2021 wakati akizindua mradi huo wa nyumba uliogharimu zaidi ya Shilingi Bilioni 2.6 ukiwa na nyumba 25 na Uniti 50. Ambapo pamoja na mambo mengine Dkt.Mabula imeishukuru NHC kwa kazi nzuri ambazo imekuwa ikifanya na ameisisitiza iendelee kufanya kazi kwa bidii pindi inapotekeleza miradi yake.

Aidha, Naibu Waziri Mabula amezitaka taasisi za Serikali na binafsi ambazo bado zinadaiwa zilipe kodi kusudi kuiwezesha wizara hiyo kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi mkubwa na kufikia malengo ikiwemo kutoa huduma mbalimbali kwa wananchi kwani fedha hizo zikilipwa huwarudia wananchi kwa njia ya huduma mbalimbali ikiwemo kujengewa miundombinu, vituo vya afya pamoja na huduma zingine.

"Taaisi za Serikali ambazo bado zinadaiwa, niziombe ziweze kulipa madeni zipo taasisi nyingi za Serikali na binafsi Mkoa wa Mara zinadaiwa zaidi ya Bilioni 6, fedha hizi ni nyingi sana zikilipwa zinasaidia wizara kufanya majukumu yake kwa ufanisi unaotakiwa,"amesema Dakt.Mabulla.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Dkt.Maulidi Banyani amesema kuwa, mradi wa nyumba hizo umegharimu shilingi Bilioni 2.6 na pia mradi una nyumba 25 na Uniti 50.

Huku eneo zina akisema lina ukubwa wa ekari 135 ambapo kwa sasa wametumia ekari 10 pekee. Huku nyumba karibuni zote zikiwa zimepangishwa na nyumba moja pekee imeuzwa.

Dkt. Banyani amesema, shirika pia limeleta maji, barabara na kuleta huduma ya umeme katika eneo hilo. Na pia upo mradi wa jengo la Mkendo Manispaa ya Musoma ambalo limejengwa na NHC na kukamilika na kuleta sura mpya katika Manispaa ya Musoma na Mkoa wa Mara kwa ujumla, ambapo pia utazinduliwa baada ya kukamilika kabisa.

Sambamba na jengo la Hospitali ya Rufaa ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere ambalo pia limejengwa na NHC eneo la Kwangwa Manispaa ya Musoma.

Naye Mwakilishi wa Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) , Emaculate Senje amesema kuwa, mradi huo umesanifiwa na kujengwa na shirika hilo kwa ajili ya kuboresha makazi na kwamba wamebakiza miradi miwili huko Makete na Igunga. Huku pia akisema bodi imeridhia kujengwa nyumba 1,000 za makazi katika jiji la Dodoma na akasema bodi italisimamia vyema shirika kukamilika ujenzi wa mradi huo ili kuwapatia wananchi makazi bora.

Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Dkt. Halfan Haule ameipongeza Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kupitia miradi ambayo imejengwa ndani ya wilaya hiyo kwani imekuwa chachu ya maendeleo. Huku akisema changamoto ya migogoro ya Ardhi bado ni kubwa katika wilaya hiyo na ameomba suala hilo kutafutiwa ufumbuzi.

Akitoa taarifa ya Ardhi ya Mkoa wa Mara Kamishina Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Mara, Happiness Mtutwa amesema kuwa, Mkoa wa Mara una wadaiwa sugu zikiwemo taasisi za umma na binafsi ambapo jumla ya deni lote wanalozidai taasisi hizo na watu ni zaidi ya shilingi Bil.6.4 huku akisema utaratibu wa kudai fedha hizo unaendeleaj kufanyika ikiwemo kuwafikisha mahakamani wadaiwa hao.

Ameongeza kuwa, wameunda kikosi kazi cha kushughulikia migogoro ya ardhi katika wilaya za Mkoa wa Mara pamoja na kufanya uhakiki wa matumizi ya ardhi kwa waliobadilisha matumizi kinyume cha sheria sambamba na kutoa elimu ya matumizi bora ya ardhi kwa wananchi.

Neema Pius ni mkazi wa eneo la Buhare ambapo mradi huo umejengwa, amepongeza hatua ya Naibu Waziri Dakt. Angeline Mabulla ya kuagiza kujengwa shule na zahanati eneo hilo itakuwa na manufaa kwao.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news