Na Munir Shemweta, MUSOMA
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amewataka watendaji wa sekta ardhi katika halmashauri na Manispaa za mkoa wa Mara kuwajibika kwa kufanya kazi kwa bidii na kuhakikisha wanatoa hati kwa wamiliki wa ardhi pamoja na kuhamasisha ukusanyaji kodi ya pango la ardhi.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Angeline Mabula akikagua moja ya Jalada la ardhi kwenye ofisi ya Msajili wa Hati na Nyaraka katika Ofisi ya Ardhi mkoa wa Mara. Wa pili kushoto ni Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Mara Hapiness Mtutwa.
Akizungumza na watumishi wa sekta ya ardhi kwenye ukumbi wa ofisi ya mkuu wa mkoa wa Mara, Dkt Mabula alisema ufanyaji kazi kwa kujituma kwa watumishi wa sekta hiyo itaiwezesha wizara ya ardhi kuongeza kasi ya utoaji hati na wakati huo kukusanya mapato yatokanayo na kodi ya ardhi.
Kwa mujibu wa Naibu Waziri wa Ardhi, kwa sasa katika mkoa huo Mara kasi ya utoaji hati za ardhi pamoja na makusanyo yatokanayo na kodi ya ardhi hairidhishi na juhudi kubwa zinahitajika katika kutoa hati na kuhamasisha wamiliki kulipa kodi ili serikali iweze kupata fedha za kuendesha shughuli zake mbalimbali.
Kwa mujibu wa Taarifa ya Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Mara Bi. Hapiness Mtutwa katika kipindi cha mwaka wa fedha 2019/2020 uliweza kukusanya shilingi bilioni 1.065 sawa na asilimia 23 katika malengo ya bilioni 4 huku mwaka wa fedha 2020/2021 ukikusanya bilioni 1.7 sawa na asilimia 47.5 kati ya malengo bilioni 3.7.
Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Maendeleo ya Makazi Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Bi. Imaculata Senje akizungumza wakati wa kikao cha Naibu Waziri wa Ardhi Dkt.Angeline Mabula na watumishi wa sekta ya ardhi mkoa wa Mara wakati wa ziara ya kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi mkoa wa Mara.
"Maelekezo yangu mkafanye kazi kwa bidii katika wilaya zenu na nikikuta mtendaji wa sekta ya ardhi hafanyi haya ninayoelekeza basi ujue wewe hutufai," alisema Dkt. Mabula.
Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Maendeleo ya makazi Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi,Bi. Imaculata Senje aliwataka watendaji wa sekta ya ardhi hasa wale wa Mipango Miji kuwa wabunifu kwa kuwaelimisha wananchi umuhimu wa maeneo yao kupimwa.
‘’Kuna miji midogo inakuwa kwa kasi katika maeneo yenu na inawezekana kama Afisa Mipango Miji ukasema huna kazi lakini unaweza kuanza kwa ktuoa elimu kwa mtu mmoja mmoja ukieleza umuhimu wa eneo lake kupangwa na kupima na kumilikishwa,’’ alisema Bi. Senje.
Watumishi wa sekta ya ardhi mkoa wa Mara wakifuatilia maelekezo ya Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula alipokutana nao katika ziara yake mkoani Mara.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akiwa na mmoja wa wananchi aliowakabidhi hati za ardhi akiwa katika ziara ya kukagua utendaji wa sekta ya ardhi mkoa wa Mara.
Naye Afisa Kodi Kutoka Wizara ya Ardhi Rehema Kilonzo aliwaeleza watendaji wa sekta ya ardhi katika mkoa wa Mara kuhakikisha wanayajua na kufuatilia kwa karibu madeni ya wadaiwa wote sugu wa kodi ya pango la ardhi na kubainisha kuwa, pamoja na Wizara kuelewa changamoto zilizopo kwenye mfumo lakini bado watendaji hao wana nafasi ya kujua madeni halisi ya wadaiwa na hivyo kuwafanya kuwa katika sehemu salama kwenye utendaji wao.