Na Nuru Mwasampeta, Mtwara
Naibu Waziri wa Madini, Prof. Shukrani Manya akizungumza na uongozi wa Mkoa wa Mtwara. Kushoto kwake ni Katibu Tawala wa Mkoa wa Mtwara, Abdallah Mohamed Malela na kulia kwake ni Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Dunstan D. Kyobya na viongozi wengine walioshiriki kikao hicho tarehe 9 Agosti, 2021.
Amezitaja taasisi hizo kuwa ni
pamoja na Wakala wa Misitu (TFS), Baraza la Taifa la Hifadhi na
Usimamizi wa Mazingira (NEMC) na Ofisi za Madini kukaa pamoja na
kuhakikisha maeneo yenye madini yanachimbwa bila kuathiri mazingira
ili kupunguza malalamiko kutoka kwa wachimbaji.
Amesema hayo leo
tarehe 9 Agosti, 2021 wakati akizungumza na uongozi wa Mkoa wa Mtwara ambapo
alipokelewa na Katibu Tawala wa Mkoa, Abdallah Mohamed Malela na kueleza
uwepo wake mkoani hapo uliolenga kujionea namna shughuli za uchimbaji
na biashara ya madini unavyoendelea lakini pia kusikiliza na kutatua
changamoto zinazowakabili wadau wa madini katika mkoa huo.
Amesema,
kumekuwa na malalamiko yanayotokana na baadhi ya taasisi kuzuia
shughuli za uchimbaji kufanyika kutokana na mamlaka inayosimamia eneo
husika kuzuia na kuwataka wasimamizi hao wanaoingiliana kiutendaji
kukaa chini na kuona namna wanavyoweza kufanya ili madini yatolewe bila
kuathiri sekta nyingine na hivyo kusukuma mbele maendeleo ya mtu
mmojammoja na serikali kwa ujumla kutokana na maduhuli yatakayopatikana
kutokana na uchimbaji huo.
Pia amewataka viongozi wa halmashauri
kushirikiana na viongozi wa Ofisi za Madini za Mikoa ili kuhakikisha
wanasimamia ipasavyo suala la utoaji wa huduma za jamii kwa wawekezaji
wa sekta hiyo ili jamii iweze kunufaika na uwekezaji unafanyika katika
maeneo yao.
Naibu Waziri wa Madini, Prof. Shukran Manya akizungumza na uongozi wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Mtwara alipowatembelea wakati wa ziara yake mkoani humo. Katikati ni Mjumbe wa Halmashauri ya CCM Taifa Lucas Medard Milasi na Muenezi.Wa kushoto ni Selemani Sankwa, Katibu wa Siasa na Uenezi Mkoa wa Mtwara
Amesema, utoaji wa huduma kwa jamii zinazozungukwa na uwekezaji ni takwa la kisheria linalomtaka mwekezaji kukubaliana nalo kabla ya kuanza uwekezaji na utekelezaji wake unazingatia makubaliano baina ya Mwekezaji, viongozi wa wananchi na Halmashauri husika kulingana na uhitaji na vipaumbele walivyojiwekea katika kuleta maendeleo katika maeneo yao.
Akizungumzia
suala la tozo katika eneo la uchimbaji wa madini ya chumvi, Prof. Manya
amesema Mwaka 2019 Sekta ya Chumvi ilikuwa na tozo 18 ambazo baada ua
majadilianao ya wachimbaji wa chumvi zilipunguzwa na kubaki na tozo sita
ili kuweka unafuu na kuwavuta wawekezaji wengi kuingia katika uchumbaji
wa chumvi. Ameongeza tozo zilizokuwa zikitolewa zilikuwa hazileti tija
kutokana na ubora na bei ya chumvi ambazo ziliwasababishia hasara
wachimbaji kutokana na gharama za uwekezaji na tozo zilizokuwepo.
Akitoa
taarifa ya utekelezaji wa majukumu katika ofisi ya Madini Mtwara, Afisa
Madini Mkazi wa Mtwara Mhandisi Ephahimu Mushi alisema, ofisi yake
inasimamia wilaya za Mtwara, Tandahimba, Masasi, Newala, Nanyumbu pamoja
na maeneo ya mipakani, uwanja wa ndege na bandarini.
Amesema, madini yanayochimbwa kwa wingi katika maeneo anayoyasimamia ni madini ya ujenzi, madini ya viwandani, mawe ya nukshi na chumvi na kubainisha kuwa madini ya ujenzi huchimbwa zaidi na wachimbaji wadogo.
Akizungumzia kuhusu madini ya dhahabu, Mhandisi Mushi amesema kufuatia kuwepo kwa uwekezaji mdogo na nguvu kazi ndogo kwenye madini hayo uwekezaji kwenye madini hayo ni mdogo na kubainisha kuwa hivi karibuni kumekuwa na ongezeko la wachimbaji kutoka maeneo mbalimbali wanaofika ili kuchimba dhahabu mkoani Mtwara.
Akizungumzia suala la ukusanyaji wa maduhulli ya serikali Mhandisi Mushi amesema kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 Ofisi yake imepangiwa kukusanya kiasi cha shilingi 2,500,000,000 ambapo kwa kipindi cha mwezi Julai wamekusanya shilingi 211,616,530.08 ikiwa ni asilimia 101.58 ya lengo la makusanyo kwa mwezi.
Ameeleza changamoto anazokutana nazo kuwa ni pamoja na upungufu wa watumishi kwa ajili ya kusimamia shughuli za uchimbaji wa madini ya ujenzi na ya viwandani, ukosefu wa vifaa muhimu katika soko la madini hasa XRF na mizani, baaddhi ya taasisi kuzuia uwekezaji katika maeneo wanayoyasimamia na hivyo kusababisha malalamiko kutoka kwa wachimbaji pamoja na kutokuwa na taarifa ya kijiolojia kwa eneo la mkoa huo.
Katika hatua nyingine, Mjumbe wa Baraza la CCM Taifa (MNEC), Lucas Medard akizungumza na Naibu Waziri Manya baada ya kutembelea ofisi za Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mtwara ameiomba Serikali kupitia Wizara ya Madini kuona namna serikali itaigusa sekta ya Chumvi ili iweze kuleta tija kwa wananchi na kuongeza mapato ya serikali, aidha ameiomba Serikali kuongeza Msukumo kwa serikali katika kuhamasisha shughuli za uwekezaji kwa mikoa ya kusini.