Na Doreen Aloyce,Diramakini Blog
IMEELEZWA kuwa takwimu zinaonyesha kuwa katika kipindi cha robo ya mwaka Januari mpaka Machi,2021 Pato la Taifa limeongezeka hadi Shilingi Trilioni 38.0 kutoka Shilingi Trilioni 36.4 Katika kipindi kama hicho mwaka 2020.
Aidha, Pato la Taifa kwa bei za mwaka 2015 liliongezeka hadi shilingi trilioni 33.2 katika robo ya kwanza ya mwaka 2021 kutoka shilingi trilioni 31.7 Katika kipindi kama hicho mwaka 2020 sawa na ukuaji wa asilimia 4.9.
Takwimu hizo zimetolewa na Naibu Mkurugenzi wa Takwimu za Uchumi, Daniel Maswola wakati alipokuwa akizungumza na waaandishi wa habari katika Ofsi Kuu za Takwimu jijini Dodoma juu ya ukuaji wa uchumi,robo ya kwanza,2021.
Aidha, amesema ukuaji wa shughuli za kiuchumi katika kipindi cha robo ya kwanza 2021,shughuli ya uchimbaji wa madini na mawe iliongezeka kwa kiwango cha juu zaidi kufikia asilimia 10.2 ikifuatiwa na Habari na Mawasiliano asilimia 9.1,uchukuzi na uhifadhi wa mizigo asilimia 9.0, maji safi na maji taka asilimia 9.0,huduma za kitaalamu ,sayansi na ufundi asilimia 7.8, huduma zinazohusiana na Utawala asilimia 7.4 na umeme asilimia 7.2.
Pia ameongeza kuwa, kuna mchango wa shughuli kuu za kiuchumi kwa kuzingatia mchanganuo wa shughuli kuu za kiuchumi za msingi, shughuli za kati na shughuli za huduma ambapo unaonesha huduma hizo zilichangia asilimia 40.1 ya Pato la Taifa zikifuatiwa na shughuli za msingi asilimia 37.1 na shughuli za Kati asilimia 22.7.
"Ukuaji wa pato la Taifa Katika robo ya kwanza ya mwaka 2021 wa asilimia 4.9 ulichangiwa na shughuli zote za kiuchumi zilizofanyika nchini katika kipindi hicho hususani ujenzi kwa asilimia 14.9,uchukuzi na uhifadhi wa mizigo kwa asilimia 14.6,kilimo kwa asilimia 12.7, uzalishaji viwandani kwa asilimia 9.8 na uchimbaji wa madini na mawe kwa asilimia 8.8,"amesema Maswola.
Vilevile, ameongeza kuwa ukokotoaji wa pato la Taifa umezingatia matakwa ya mfumo wa Umoja wa Mataifa wa kutayarisha Takwimu za Pato la Taifa unaojulikana kama System of National Accounts 2008 kwa lengo la kutayarisha takwimu linganifu kati ya nchi moja na nyingine.
"Kwa mujibu wa Sheria ya Takwimu Sura 351 ,Takwimu hizi za Pato la Taifa kwa robo ya kwanza ya mwaka 2021 ni rasmi na zinatumika katika kufuatilia na kutathmini malengo yaliyowekwa Katika Sekta za kiuchumi,"ameongeza Maswola.