Prof.Manya:Serikali inahimiza uwekezaji kwa kuweka mazingira rafiki, mpate faida

Na Nuru Mwasampeta, Mtwara

IMEELEZWA kwamba Serikali ya Awamu ya Sita inahimiza uwekezaji kwa kuweka mazingira rafiki ili mwekezaji yeyote nchini aweze kupata faida ya uwekezaji alioufanya.

Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri wa Madini, Profesa Shukrani Manya jana Agosti 9, 2021 alipotembelea kiwanda cha Dangote kilichopo Mkoa na Wilaya ya Mtwara kwa lengo ya kujionea namna kinavyotekeleza majukumu yao.

Prof. Manya amesema, uwepo wa kiwanda hicho nchini una manufaa makubwa kwa Taifa kwa kuzalisha ajira kwa vijana na ndiyo sababu Serikali inasisitiza kufuata sheria na kanuni zinazoingoza Sekta ya Madini ikiwa ni pamoja na ile ya Uwezeshaji wazawa.
Aliendelea kusema kutokana na sheria hiyo imepelekea kiwanda kutoa ajira kwa wafanyakazi wa Kitanzania 225 wageni wakiwa watatu tu. Hii inaonesha namna gani mwekezaji anafuata maelekezo ya sheria.

Aidha, Prof. Manya aliwahimiza wawekezaji hao kutokuruhusu mdudu rushwa kuingilia kati wakati wa utekelezaji wa CSR ili makubaliano wanayoingia na halmashauri yatekelezeke kwa weledi na uaminifu mkubwa.

Ameongeza kuwa, Serikali inatamani kuona thamani ya pesa inayotumika kwenye utekelezaji wa miradi kwa jamii na kumtaka Mkuu wa Wilaya ya Mtwara kulisimamia hilo.

“Mheshimiwa DC hili lipo katika mamlaka yako, Rais angetamani kuona thamani ya fedha ya miradi inayowekwa kwenye jamii zetu. Kwa hiyo hili ulisimamie kwa nguvu,”Prof. Manya alisisitiza.

Prof. Manya aliendelea kusema kufuatia sheria ya uwezeshaji wazawa jamii zinaweza kuona faida za mwekezaji kuwepo.

Kwa upande wao uongozi wa Dangote wameishukuru Serikali kwa kuwatembelea ili kuona uwekezaji walioufanya nchini na kubainisha kuwa wako tayari kufuata kanuni na sheria zote za madini nchini.

Pamoja na hayo, walibainisha kuwepo kwa changamoto ya upatikanaji wa bidhaa nyingine zinazohitajika kwa ajili ya kuendesha kiwanda hicho ikiwa ni pamoja na kuwa na changamoto ya kusafirisha bidhaa yao nje ya nchi kutokana na eneo walikowekeza kuwa mbali.

Walibainisha kuwa kiasi cha madini ya chokaa yanayotumiwa kiwandani hapo yana uwezo wa kutumika katika uzalishaji wa Saruji kwa muda wa miaka 180 na hivyo kuiaminisha Serikali kuwa uwekezaji huo utatumika kwa miongo miwili endapo hakutakuwa na changamoto nyingine yeyote itakayopelekea uwekezaji huo kusitishwa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news