NA MWANDISHI DIRAMAKINI
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, leo tarehe 06 Agosti, 2021 amewaongoza viongozi mbalimbali na waombolezaji kuaga mwili wa aliyekuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa marehemu Elias John Kwandikwa.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akiongoza Viongozi mbalimbali na Wananchi kuaga Mwili wa aliyekuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa marehemu Elias John Kwandikwa katika Viwanja vya Karimjee Jijini Dar es Salaam.
Akizungumza wakati akitoa salamu za pole, Mhe. Rais Samia amesema, kifo cha marehemu Kwandikwa kimeacha simanzi na pengo kubwa si kwa familia pekee bali pia kwa Serikali na Taifa kwa ujumla.
Amesema, Serikali imempoteza mtumishi na kiongozi mwadilifu, makini, shupavu na mchapakazi hodari.
Aidha, Mhe. Rais Samia amewashukuru viongozi wa dini kwa kuongoza ibada ya kumuaga marehemu Kwandikwa ambapo mahubiri yao yametoa faraja na kukumbusha kuwa wanadamu duniani wanapita, hivyo kutakiwa kuishi kwa wema na kutenda yale ya kumpendeza Mungu.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akiifariji Familia ya aliyekuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa marehemu Elias John Kwandikwa baada ya kuongoza Viongozi mbalimbali na Wananchi kuaga Mwili wa Hayati Kwandikwa katika Viwanja vya Karimjee Jijini Dar es Salaam leo tarehe 06, Agosti 2021. (PICHA NA IKULU).
Shughuli za kuaga mwili wa Marehemu Kwandikwa zimefanyika katika viwanja vya Karimjee Jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali akiwemo Makamu wa Rais Mhe. Dkt. Philip Mpango, Rais wa Zanzibar Mhe. Dkt. Hussein Mwinyi, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdallah, Naibu Spika wa Bunge Dkt. Tulia Ackson, Jaji Mkuu wa Tanzania Profesa Ibrahim Hamis Juma, Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Hussein Kattanga, Katibu Mkuu Kiongozi-Zanzibar Mhandisi Zena Said pamoja na viongozi wengine wa vyama vya Siasa na Serikali.