NA MWANDISHI DIRAMAKINI
Mkuu wa Mkoa (RC) wa Mara, Ally Hapi amebaini ulegevu katika kusimamia baadhi ya miradi ya maendeleo wilayani Serengeti na kuagiza hatua zichukuliwe kuondoa kasoro zilizobainika.RC huyo ameanza ziara ya ukaguzi wa miradi hiyo katika kila halmashauri, ambayo imeanza hadi Agosti 20,mwaka huu.
Miongoni mwa miradi iliyokaguliwa leo ni Jengo lenye Vyumba Viwili vya Madarasa na Ofisi Moja ya walimu la Sekondari ya Machochwe Kata ya Machochwe lenye thamani ya Sh milioni 40 pamoja na ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Serengeti wenye thamani ya Sh bilioni 1.3
Akiwasilisha taarifa ya mradi, Mkuu wa Shule hiyo, Vitalis Mayanja amesema mpaka sasa zimetumika Sh milioni 36 na kwamba bado hawajajenga miundombinu ya umeme, kuingiza umeme kwenye jengo, kununua viti na meza kwa ajili ya madarasa hayo.
Ukaguzi wa RC Hapi ulibaini kuwa licha ya kuelezwa kuwa bado hawajajenga miundombinu ya umeme ndani ya jengo hilo, ujenzi ulishakamilika hata "gypsum" zimefungwa na jengo zima kupakwa rangi.
"Haiwezekani kuvaa nguo ya ndani juu ya suruali, kuna kila dalili jengo hili lisingewekewa umeme," amesema RC Hapi huku wananchi waliohudhuria mkutano huo wakimshangilia.
Sintofahamu nyingine imejitokeza kwenye mradi wa ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ambako kumeshuhudiwa kasoro tofauti ikiwamo maji kuvuja na kuharibu dari (gypsum) ilhali jengo bado jipya.
RC Hapi alieleza kutofurahishwa na aina ya umaliziaji ujenzi katika hospitali hiyo, kwamba pamoja na kutaka ubora wa majengo wenye kuzingatia thamani ya fedha, Serikali inataka kuona majengo yake yakivutia.
Katika mahojiano na Mhandisi wa Ujenzi wa Halmashauri hiyo, Alex Albinus kuhusu kasoro hizo RC Hapi alimtaka kuongeza umakini kwenye kusimamia miradi vinginevyo ataangukiwa na jumba bovu.
"Pale shuleni ulishapigwa tobo, utapigwa matobo mangapi sasa mkuu? kuwa makini utaumizwa,"amesema.