RC Kunenge amdaka Mwenyekiti wa CCM akitajwa miongoni mwa vishoka waliokuwa wakiuza viwanja kitapeli

Na Rotary Haule, Kibaha

MKUU wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge ameanza kukunjua makucha kwa kumkamata Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Godfrey Mwaipopo baada ya kugundulika kuwa ni miongoni mwa vishoka waliokuwa wakiuza viwanja kitapeli.
Mkuu wa Mkoa Pwani, Abubakar Kunenge akizungumza na wananchi wa Mtaa wa Lulazi katika Kata ya Picha ya Ndege Kibaha mkoani Pwani alipokwenda kwa ajili ya kusikiliza na kutatua kero za ardhi katika mtaa huo.(Picha na Rotary Haule).

Mbali na Mwaipopo kukamatwa, lakini ipo orodha ya watu wanaodaiwa kufanya utapeli wa ardhi na kuvamia mashamba ya watu ambao majina yao yalisomwa na Mkuu huyo wa Mkoa mbele ya mkutano huo.

Kunengeambaye aliambatana na kamati ya ulinzi na usalama amechukua hatua hiyo mbele ya wananchi wa Mtaa wa Lulanzi alipokwenda kwa ajili ya kusikiliza na kutatua kero za ardhi.

Akizungumza katika mkutano huo Kunenge,alisema kuwa amekuja Pwani kufanya kazi ya kusafisha vishoka wote wa ardhi ili kusudi Mkoa uwe salama.

Kunenge alisema kazi yake ya kukamata vishoka hao itakuwa endelevu lakini hatomuonea mtu bali atatenda haki kwa kila mtu lakini waliotenda maovu hawataachwa.

Alisema,mtu ambaye ameuza ardhi au kiwanja kimoja kwa zaidi ya watu wawili amekuwa amehatarisha usalama na kuvunja amani katika jamii na kwamba hastahili kuachwa.

"Nilisema awali wale vishoka wa ardhi Sasa hawana nafasi ,kama wewe mtumishi wa Serikali,mfanyabiashara au sijui unafanya kazi gani sitokuacha nitakukamata ili ukahojiwe, lakini nikijiridhisha kama huna kosa basi utaachiwa "alisema Kunenge.

Alisema kuwa, nchi inaongozwa kwa mujibu wa sheria na umiliki wa ardhi unafanywa kwa mujibu wa sheria huku akiongeza kuwa mtu anaweza kuwa na hati ya kumiliki ardhi kihalali na unaweza kumiliki hata miaka 30 lakini jukumu kubwa lipo mikononi mwa Serikali kulinda watu wake.

Aidha, Kunenge aliongeza kuwa mtu yeyote anayeingia katika eneo bila kufuata utaratibu wa kisheria hali akitambua eneo hilo linalomilikiwa kihalali na lina hati inayotambuliwa na Serikali huyo ni mvamizi na anapaswa kuchukuliwa hatua.

Hata hivyo, Kunenge amemtaka mkuu wa Jeshi la Polisi kuhakikisha wale wote waliotajwa katika tuhuma za kutapeli na kuuza ardhi kwa njia za panya wakamatwe maramoja ili wajibu tuhuma zao.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news