RC Makongoro: Mwalimu muonekano wako haufanani kabisa kufanya jambo kama hili

Na Mary Margwe, Simanjiro

MKUU wa Mkoa wa Manyara, Makongoro Nyerere amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro, Dkt.Suleiman Serera kufanya uchunguzi juu ya matumizi ya sh.milioni 5 zilizotolewa na mfuko wa jimbo kwa ajili ya ukarabati wa madarasa ya shule ya msingi Namelock ya Kijiji cha Orbili Kata ya Shambarai wilayani Simanjiro.
Ameyabainisha hayo wakati akipewa taarifa ya ujenzi wa zahanati ya Obil ambapo Diwani wa Kata ya Shambarai, Julius Mamasita alimwambia mkuu huyo kuwa, licha ya hilo kuwa nje ya ratiba, lakini alimuomba apitie kuangalia ukaguzi ndipo walipobaini ubadhirifu uliofanya na mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Namelock, Peter Kaleki.

Ukarabati wa madarasa hayo, ulipaswa kufanyika kwa fedha zilitolewa kupitia mfuko wa mbunge wa jimbo la Simanjiro, Christopher Ole Sendeka sh.milioni 5 kwa ajili ya ukarabati wa madarasa matano, hali ambayo imeonekana kufanyika kinyume kulingana na matarajio.

Kufuatia tukio hilo, Makongoro alimuagiza mkuu wa wilaya hiyo, Dkt.Suleiman Serera kufuatilia na kufanya uchunguzi juu ya suala hilo, ambalo limeonekana kuchafua hali ya hewa siku ya ziara hiyo ili kubaini namna gani sh.milioni 5 zilivyotumika katika ukarabati wa madarasa matano ya shule hiyo.

"Pengine niwaambie mimi siyo muumini kabisa wa kuweka watu ndani, leo nakupa mkono wa wangu wa heri usiuzabe, namuagiza Mkuu wa wilaya afanye uchunguzi na taarifa nipatiwe ili tufahamu kilichotokea na endapo kukiwa na ubadhirifu tuchukue hatua juu yako...sawa mwalimu, muonekano wako haufanani kabisa kufanya jambo kama hili, acha uchunguzi ufanyike tuone uhalisia wa suala hili," alisema Makongoro.

Aidha, alishangazwa kuona madarasa hayo kutosakafiwa huku vibaraza vya nje vilivyosakafiwa kukuta vimebanduka banduka saruji, hali iliyompa mashaka na kuagiza uchunguzi ufanyike haraka iwezekanavyo, ambapo alisema kutosakafiwa kwa madarasa hayo imesababisha kuwepo kwa vumbi na hivyo kuathiri wanafunzi pindi wakiwa madarasani wakisoma.

Awali, Diwani wa Kata ya Shambarai, Julius Mamasita alisema japokuwa yeye siyo mtaalamu wa ufundi ila hakubaliani na namna fedha hizo zilivyotumika kwa ajili ya kukarabati wa madarasa hayo.

"Mwalimu mkuu hataki ushirikiano na jamii inayomzunguka akidai kuwa hawawezi kumfanya chochote, ndiyo sababu anajiamulia kila kitu anachotaka kufanya yeye mwenyewe, hivyo mheshimiwa Mkuu wa mkoa najua hili haliko kwenye ratiba yako, lakini naomba upitie pale ili uweze kujionea hali halisi," alisema Mamasita.

Mbunge wa Jimbo la Simanjiro, Christopher Ole Sendeka alisema, anasikitishwa na kitendo cha usimamizi mbovu wa ukarabati wa majengo hayo ya shule hiyo uliofanywa na mwalimu mkuu.

"Unapopewa nafasi ya kusimamia jambo unapaswa kutimiza wajibu wako ipasavyo na siyo kufanya ubabaishaji kama hiki tunachokiona hapa, siku zote ukiaminiwa nawe jiaminishe," alisema Ole Sendeka.

Hata hivyo, mwalimu mkuu wa shule hiyo, Peter Kaleki alisema chuki binafsi ndiyo zimesababisha achukiwe eneo hilo, hivyo hajafuja fedha zozote za mradi huo, na hivyo uamuzi uliochukuliwa na kufanyiwa uchunguzi litakuwa ndio suluhisho la huo utata uliopo juu yake.

"Fedha zilizotolewa kwa ajili ya ukarabati ni ndogo, hivyo thamani ya mradi inaonekana kupitia fedha hizo japokuwa kuna baadhi ya vifaa vimebaki tulivyonunua hivyo hapo," alisema Kaleki.

Hata hivyo naye mkuu wa wilaya ya Simanjiro, Dkt. Suleiman Serera alimuhakikishia mkuu huyo wa mkoa kufanya uchunguzi kwenye shule hiyo ili kubaini thamani halisi ya gharama za ujenzi ulivyotumika.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news