RUWASA GEITA: BILIONI 15/- KUPELEKA MAJI VIJIJI VYOTE 474

Na Robert Kalokola, Diramakini Blog

Wakala wa Maji na Usafi wa Mzingira Vijijini (RUWASA) Mkoa wa Geita imepanga kwenye bajeti yake ya mwaka wa fedha wa serikali wa 2021/2022 kutumia Shilingi bBilioni 15,085,186,782.05 kumaliza upungufu wa maji lita milioni 2,160,470 katika vijiji vyote 474 vya mkoa huo ambayo ni sawa na asilimia 40 ya upungufu wa maji katika Wilaya zote tano za mkoa mzima.
Mkuu wa Mkoa wa Geita Rosemary Senyamule akiwasha pikipiki kati ya tano alizokabidhi kwa RUWASA Wilaya ya Nyang'hwale na Mbogwe. (Picha na Robert Kalokola).

RUWASA itatumia fedha hizo kujenga miradi mbalimbali 55 katika Wilaya ya Geita(12) ,Nyang’hwale(10),Mbogwe (15),Bukombe(10) na Chato (8) ikiwa ni fedha kutoka katika Mipango ya Program for Results( P4R),Payment for Results(PBR) na National Water Fund ( NWF).
Hayo yamesemwa na Meneja wa RUWASA Mkoa wa Geita, Mhandisi Jabiri Kayila katika hafla fupi ya kukabidhi magari mawili na pikipiki tano kwa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Wilaya ya Nyang’hwale na Wilaya Mbogwe ambayo yalikabidhiwa na Mkuu wa Mkoa wa Geita, Rose Senyamule.

Mhandisi Jabiri Kayila amesema kuwa Mkoa wa Geita una mahitaji ya maji lita 5,401,175 kwa siku lakini wastani wa uzalishaji wa maji kwa siku hadi sasa ni lita 3,240,705 ambapo upungufu ni lita milioni 2,160,470 sawa na asilimia 40 na upatikanaji wa maji kwa wananchi ni wastani wa asilimia 60.

Meneja wa RUWASA Mkoa, Jabiri Kayila ameongeza kuwa,katika mwaka wa fedha 2020/2021 RUWASA Mkoa wa Geita imetekeleza na kukamilisha miradi ya maji 16 katika wilaya zote za mkoa wa Geita na baadhi ya Miradi ya maji inaendelea kutekelezwa katika hatua mbalimbali.
Mkuu wa Mkoa wa Geita, Rosemary Senyamule (aliyenyoosha mikono) baada ya kukabidhi magari mawili na pikipiki tano kwa Ruwasa Wilaya ya Nyang'hwale na Mbogwe ,kushoto ni Meneja wa Ruwasa mkoa wa Geita Jabiri Kayila (picha na Robert Kalokola).

Aidha,ameongeza kuwa ujio wa magari mawili na pikipiki tano kwa ajili ya Ruwasa Wilaya Mbogwe na Nyang’hwale itasaidia katika usimamizi mzuri wa miradi hiyo ya maji katika wilaya hizo kwani kabla ilikuwa Changamoto kufikia miradi hiyo kwa ajili ya usimamizi.
Meneja wa RUWASA Mkoa wa Geita, Mhandisi Jabiri Kayila. (Picha na Robert Kalokola).

Mkuu wa Mkoa wa Geita, Rosemary Senyamule amepongeza RUWASA kwa namna inavyofanya kazi za kujenga miradi ya maji katika mkoa huo na kuakikisha wananchi wa mkoa huo wanapata huduma hiyo ambapo wameweza kufikisha asimilia 60 ya usambazaji wa maji vijijini.

Rosemary Senyamule amesema kuwa, kwa mujibu wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020/2025 inaelekeza kufika mwaka 2025 Maji Vijijini iwe ni kwa asilimia 85 na Mjini iwe asilimia 95 na hivyo kuwaagiza RUWASA kuongeza kasi katika utendaji wao ili kuakikisha kwa miaka ilisalia asilia 25 zikamilike ili iwe asilimia 85 vijijini kwa mkoa wa Geita.
Mkuu wa Mkoa (ndani ya gari), Rosemary Senyamule akiwasha moja ya magari mawili yaliyokabidhiwa kwa RUWASA Wilaya ya Nyang'hwale na Mbogwe nje ni Meneja wa RUWASA Mkoa wa Geita Jabiri Kayila, ( Picha na Robert Kalokola).

Aidha, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Rose Senyamule ameagiza mamlaka hiyo kuangalia utaratibu mzuri wa kupunguza gharama za maji hasa yanayotoka Ziwa Viktoria ili bei zake ziwe za kutoa huduma kwa wananchi zisiwe za kibiashara kwani malalalamiko ya gharama hizo kuwa kubwa amekutana nayo Wilaya ya Nyang’hwale katika Mradi wa Nyamtukuza na Wilaya ya Chato.

Mbunge wa Jimbo la Nyang’hwale, Nassor Kasu amesema kitendo cha mradi wa Nyamtukuza kuanza kutoa maji ni utendaji mzuri wa RUWASA na kwamba umepokelewa vizuri na wananchi na msisitizo itakuwa na kulinda na kuhifadhi miundombinu ya mradi huo.

Aidha, ameomba RUWASA kufanya haraka kupeleka wakandarasi katika mradi huo ili kukamilisha eneo lililobaki ili wananchi wengi wapate maji katika Wilaya hiyo kama mradi ulivyopangwa kuwafikia wananchi.

RUWASA ilianzishwa kwa sheria Namba 5 ya maji safi na usafi wa mazingira mwaka 2019 na kwa mkoa wa Geita ilianza kufanya kazi mwaka huo huo ikiwa chini ya Wizara ya Maji na inaendelea kusimamia na kutekeleza miradi mbalimbali ya maji vijijini mkoa mzima wa Geita.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news