Serikali yatangaza mageuzi ya kihistoria kupitia ujenzi wa barabara mijini na vijijini

Na Doreen Aloyce, Diramakini Blog 

SERIKALI imezindua Mpango Mkakati wa Pili wa miaka mitano wa Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (TARURA) wenye thamani ya shilingi Trilioni 3.6 ikilenga kupeleka ya neema ya barabara kwa wananchi.
Akizindua mpango huo jijini hapa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI), Ummy Mwalimu amebainisha namna Serikali itakavyoimarisha utendaji kazi wa wakala huo kwa kuwapa magari na kuajiri watumishi wa kada mbalimbali ikiwamo wahandisi.

Uzinduzi wa mpango huo ulioenda sambamba na uzinduzi wa kauli mbiu isemayo ‘TARURA tunakufungulia barabara, kufika kusikofikika’, Waziri Ummy amesema utekelezaji wa mpango huo utaleta mapinduzi makubwa ya ujenzi wa barabara nchini na kurahisisha maeneo ya mijini na vijijini kufikika.

“Mpango huu unaanza mwaka huu 2021/22 hadi 2025/26 na utaongeza mtandao wa barabara kutoka kilometa 2,404.90 hadi 3,855.65, changarawe kutoka kilometa 29,116.57 hadi 102,358.14 na madaraja kutoka 2,812 hadi 6,620 na fedha zitakazotumika ni Sh.Trilioni 3.6,”amesema.

Ameseza kuwa, kama mpango mkakati huo utatekelezwa vyema zitajengwa barabara za changarawe kilometa 73,242 na kwamba hayo ni mafanikio makubwa kwa kuwa asilimia 70 ya barabara nchini ni za vumbi.

“Mpango huu kwa miaka mitano unahitaji Sh.Trilioni 3.6 sio kabisa Rais Samia kama atashindwa kwa kuwa anauwezo wa kuzitafuta ndani ya miaka mitatu, twendeni tukaoneshe kazi yenye ubora na ufanisi,”amesema.

Akizungumzia bajeti ya mwaka huu 2021/22, Waziri huyo amesema wakati anaingia TAMISEMI moja ya malalamiko makubwa ilikuwa ni uwezo wa kifedha wa TARURA katika kutekeleza majukumu yake.

“Suala hili tuliliwasilisha kwa Rais Samia Suluhu Hassan akatuelewa, na wakati wa kampeni kwa bahati nzuri Rais alipita mikoa yote na anafahamu hali za barabara, hivyo alikubali kuongeza fedha ya kazi ya ujenzi na ukarabati wa barabara, tukapata fedha kutoka Mfuko Mkuu wa serikali Sh.Bilioni 127 haijawahi kutokea tangu Tarura imeanzishwa,”amesema.

Amesema, Rais Samia pia alisikia kilio cha wabunge na kuja na chanzo kipya ya tozo ya mafuta ambapo TARURA itapata Sh.Bilioni 326 sambamba na Sh.Bilioni 127.

“Hivyo kwa mwaka wa fedha 2021/22, Wakala umeidhinishiwa Sh.Bilioni 934.09 fedha hizi ni nyingi na ni mara tatu ya fedha ambazo Tarura ilikuwa inapata nataka Katibu Mkuu tukitoka hapa ndani ya siku tatu tuondoke na uelewa mmoja, mkishindwa kufanya vizuri kusimamia ujenzi na ukarabati wa barabara mtanyooshewa vidole na hamtaaminika kwenye macho ya watanzania,”amesema.

Ametoa angalizo kwa Wakala huo kuhakikisha kazi za ujenzi wa barabara zifanyike kwa ufanisi kwa kuwa ni kipimo chao kwa watanzania.

“Tunataka tuone tija katika suala zima la ukarabati wa barabara mijini na vijijini, ndugu zangu mnakazi kubwa mwaka huu mmoja ndio mwaka wa kuwapima je, kile kisingizio cha kuwa hamna fedha kilikuwa kisingizio au hamna uwezo na ubunifu na utashi wa kazi mnazotakiwa kuzifanya,”amesema.

Amesema, matarajio ya serikali kwa TARURA ni makubwa sana hivyo wasiiangushe na waoneshe kuwa ni taasisi sahihi ya kufungua barabara za mijini na vijijini.

“Tunataka mhakikishe miradi inayotekelezwa inalingana na fedha iliyotumika, pia hakikisheni matarajio ya watanzania na wabunge, niwaeleze tu Tarura wabunge chini ya Spika Ndugai wana matarajio makubwa kuwa mnakwenda kufanya kazi vizuri zaidi,”amesema.

Amesema kero ya barabara mijini na vijijini itatatuliwa kupitia ongezeko la bajeti kutoka Sh.Bilioni 273 mwaka 2020/21 hadi Sh.Bilioni 934.09 mwaka 2021/22, ambapo mtandao wa barabara za lami utaongezeka kutoka kilometa 2,404 hadi 2,642.

“Kilometa za barabara za changarawe zitaongezeka kutoka 29,166 hadi 41,155 kwenye Halmashauri 184 nchini na madaraja 736,”amesema.

Awali, Naibu Waziri wa Ofisi hiyo, David Silinde, amesema TARURA katika historia ya nchi kwa mara ya kwanza imetengewa fedha nyingi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news