Serikali yatenga Bilioni 9/- ujenzi Hospitali ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, Dkt.Gwajima aonya upotoshaji chanjo ya UVIKO-19

Na Fresha Kinasa, Diramakini Blog

WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Dkt.Dorothy Gwajima amesema kwa mwaka huu wa fedha 2021/2022 Serikali imetenga Shilingi Bilioni 9 kuendeleza ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere iliyopo Kwangwa Manispaa ya Musoma Mkoa wa Mara, ambayo ujenzi wake umefikia kati ya asilimia73 - 75 huku huduma za matibabu ya mama na mtoto pamoja na usafishaji wa figo (Dialysis) zikitolewa.
Katika picha ni Mganga Mkuu wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara, Dkt. Joachim Eyembe akifafanua jambo kwa Waziri wa Afya, Mheshimiwa Dorothy Gwajima alipotembelea ujenzi wa Hospitali ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere iliyopo Kwangwa Musoma. (Picha zote na Diramakini Blog).

Kauli hiyo imetolewa Agosti 16, 2021 na Waziri huyo alipotembelea na kukagua Hospital ya Rufaa ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere katika Kata ya Kwangwa ambapo ameridhishwa na kazi nzuri iliyofanyika kwa asilimia 75 na kufikia hatua nzuri za ujenzi na utolewaji wa huduma ya mama na mtoto na huduma ya kusafisha figo katika wing 'C'na B zilizokamilika isipokuwa Wing 'A' ambayo ujenzi wake unaendelea hivyo fedha Shilingi Bilioni 9 zitatumika kuendeleza ujenzi huo.

Waziri Gwajima asema kwamba, uanzishwaji wa huduma ya kusafisha figo hospitalini hapo ni muhimu sana na kwamba, itapunguza gharama za wagonjwa kwenda kutibiwa Mbali huku akisisitiza kuwa dhamira ya Serikali ni kuifanya Hospitali hiyo isaidie kwa kiwango kikubwa cha utoaji wa huduma za Kibingwa hususani kusafisha Figo kusaidiana na Hospital ya Benjamini Mkapa na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

"Shilingi Bil.9 zipo zimetengwa na Serikali ya Awamu ya sita, kwa hiyo Wakandarasi fedha hizi zitumike kusudi Wing' A' ikamilike haraka wakazi wa Mkoa wa Mara na maeneo jirani wanufaike na huduma ambapo huduma zinazotolewa MOI ikibidi ziwe hapa, nimefurahi kuona huduma za mama na mtoto zikitolewa pamoja na uanzishwaji wa huduma ya kusafisha Figo. Wing 'A' ikikamilika huduma za OPD, Emergency, Maabara zitatolewa haya ni mafanikio makubwa katika kuimarisha sekta ya afya," amesema Dkt. Gwajima.

Kuhusiana na Chanjo ya (Uviko-19) Waziri Gwajima amewataka Watanzania kujitokeza kuchanja kwani chanjo ni Salama kabisa na kwamba uzushi wowote unaozushwa juu ya chanjo unapswa kupuuzwa akapongeza uongozi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara chini ya Mganga Mfawidhi Dakt. Joachim Eyembe kwa kazi nzuri wanayofanya kuhudumia Wananchi kwa ufanisi. 

Akawataka Watumishi wa afya Mkoani Mara na Tanzania kwa ujumla, kutoa elimu ya corona na kuhimiza Wananchi kuchanja.

"Watu wengi wanaolazwa na kutumia Oxygen ni wale ambao hawajachanja, chanjo ni Salama, uzushi na upotoshaji unaotolewa upuuzwe. Mtu anakataa chanjo ya Uviko-19 lakini anatumia dawa za TB na mipira ya Kondom ananunua wakati hatuna kiwanda. hizi zote zinatolewa nje, kwa hiyo chanjo ni salama kabisa hata Rais Hayati Magufuli watu hawakumuelewa alisema tusikimbilie chanjo bali tujiridhishe na serikali ya Awamu ya Sita imejiridhisha tayari na ndio maana imeruhusu chanjo ambayo ni Salama kabisa Wananchi tuepukeni uzushi na upotoshwaji juu ya chanjo. Chanjo zilikuwepo na zitakuwepo vinginevyo tungekuwa vilema na viwete Kutokana na polio na surua," amesema Waziri Gwajima.

Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Dkt.Halfan Haule akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mara, ameishukuru Wizara ya Afya kwa kuutendea haki Mkoa wa Mara ambapo kukamilika kwa Hospitali hiyo ni faraja kubwa kwa wanamara kupata huduma za matibabu karibu.

Katibu wa CCM Mkoa wa Mara,Shaibu Ngatiche amelipongeza Shirika la Nyumba (NHC) kwa kazi nzuri lililofanya na kufikia hatua nzuri za ujenzi wa hospitali hiyo ambayo itakuwa mwarobaini kwa wakazi wa Mara na maeneo jirani.

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara Dakt. Joachim Eyembe amesema tangu Hospital hiyo imeanza kutoa huduma mwezi Agosti mwaka Jana zaidi ya Kinamama 1950 wamejifungua katika Hospitali hiyo sambamba na kinamama 400 kufanyiwa upasuaji. Huku pia huduma ya kusafisha figo (Dilysis) amesema imeanza kutolewa Agosti 4, 2021.

Dkt. Eyembe ametaja changamoto zilizopo ni upungufu wa madaktari Bingwa kwani waliopo ni wanne tu, nyumba za watumishi, ambapo mkakati wa kutatua changamoto hiyo amesema watapeleka madaktari Bingwa wanane kusoma ili waje kusaidia utatuzi wa changamoto hiyo kuleta Mapinduzi chanya ya huduma za kibingwa.

Awali Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mara Dkt. Juma Mfanga amesema kwa sasa wanaendelea kutoa elimu ya kujikinga na Corona, kuhamasisha Wananchi uvaaji wa barakoa, unawaji mikono, huku akisama pia wanatarajia kupokea mitungi ya Oxygen Kutoka kwa mdau na iliyopo ni mitungi 62.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news