Wakati huo huo, Dkt. Sospeter Bulugu amesema alipatwa na tatizo la kushuka kwa sukari kwenye damu ambayo kitaalamu inajulikana kama Hypoglycemia, ANARIPOTI MWANDISHI DIRAMAKINI Blog.
Dkt.Bulugu amesema kuwa, wakati akizungumza alipata hali ya kizunguzungu ambayo hata yeye hakuielewa baada ya wataalamu kumuangalia akiwemo, Dkt. Kaushik na timu yake walimpa huduma ya kwanza na baada vipimo ilionekana sukari yake imeshuka.
Daktari huyo ameyasema hayo leo Agosti 13,2021 ambapo wakati akizungumzia kuhusiana na hali hiyo.
Amesema, alipatiwa vinywaji vyenye sukari na chakula na baada ya hapo hali yake ikawa vizuri na kuendelea na shughuli zake kama kawaida.
Daktari huyo ambaye ni Kamishna wa Afya Jumuiya ya Wanafunzi wa Taasisi za Elimu ya Juu (TAHLISO) alipatwa na hali hiyo wakati akitoa mada kuhusu uelewa wa vijana juu chanjo ya Covid-19 katika mdahalo wa kitaifa kisayansi uliofanyika ulifanyika mkoani Dar es Salaam.
Ufafanuzi huo umefuatia baada ya video fupi kusambaa mitandaoni ikimwonyesha daktari huyo akipatwa na hali ya kizunguzungu hivyo, wataalamu kulazimika kumpatia huduma ya kwanza na baadaye ilisikika sauti ya waziri ikihoji baadhi ya maswali iwapo alikuwa amepata chanjo.
Kwenye video hiyo Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Wazee na Watoto, Dkt. Doroth Gwajima amesikika akihoji iwapo Dkt. Bulugu alikuwa amepata chanjo na ilipothibitika hakupata ya Uviko-19 sauti ya Waziri wa Afya ilisikika tena ikisema, basi amepatwa na kushuka kwa sukari hasa ukizingatia tangu kuanza kwa mkutano huu hakukuwa na mapumziko ya chai.