Si ajabu kukutana na Trafiki akiwa amevalia makobasi, silaha ya kivita akiongoza magari Kabul

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

Siku chache baada ya Kundi la Taliban kuteka mji mkuu wa Kabul, Afghanistan ikiwa ni miaka 20 baada ya kuondolewa madarakani. Hofu inaonekana kwa wanaoitazama nchi hiyo kutoka nje, lakini kwa raia wa kawaida sasa wanaona hali inaendelea kurejea sawa siku baada ya siku.
Kwa sasa, Wataliban wako kila mahali, kwenye vituo vya ukaguzi ambavyo zamani vilikuwa vinasimamiwa na polisi au vizuizi vya jeshi.

Ni wazi kuwa, hapa hakuna hofu kubwa kama ilivyokuwa jana au juzi. Taliban wanadhibiti usalama barabarani, wanakagua magari, wanaendelea kutafuta mali zote za kijeshi ambazo zilichukuliwa baada ya hali ya taharuki Jumapili iliyopita.

Licha ya maisha kuendelea kurejea taratibu taratibu, mashirika ya Umoja wa Mataifa yanaendelea kufuatilia kwa karibu hali nchini humo.

Mashirika hayo yanaona kuwa, hali ya usalama nchini Afghanistan hususani mjini Kabul haitoi asilimia zote za kuaminika kuwa, binadamu anaweza kuishi bila bughda.

Pia wanaona kuwa, huenda ahadi zilizotolewa na kundi la Taliban kuwanusuru wananchi ambao kwa maelfu wanahaha kukimbia kwenda kusaka usalama zinaweza kuwa ni propaganda.

Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa (OHCHR) kupitia taarifa yake iliyotolewa mjini Geneva, Uswisi imesema hali ya taharuki iliyoshuhudiwa kwenye uwanja wa ndege wa Kabul inasisitiza ukubwa wa tatitzo nchini humo na mji wa Kabul kwa ujumla.

“Kwa bahati nzuri, mji mkuu na miji mingine mikubwa ya mwisho kutekwa kama Jalalabad na Mazar-e-Sharif haikukumbwa na mapigano ya muda mrefu, umwagaji damu au uharibifu. Lakini, hofu iliyotanda kwa idadi kubwa ya watu ni kubwa, na kulingana na historia ya zamani inaeleweka kabisa.

“Wasemaji wa Taliban wametoa taarifa kadhaa katika siku za hivi karibuni, pamoja na kuahidi msamaha kwa wale ambao walifanya kazi kwa Serikali iliyopita. Wameahidi pia kuwa wajumuishi. Wamesema mwanamke anaweza kufanya kazi na wasichana wanaweza kwenda shule. Ahadi kama hizo zitahitaji kuheshimiwa, na hasa kwa wakati huu ukizingatia historia ya zamani, maazimio haya yamekaribishwa na wasiwasi.Lakini, ahadi hizo zimetolewa na ikiwa zinaheshimiwa au zitavunjwa zitachunguzwa kwa karibu,”imefafanua taarifa ya Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa.

Kwa mujibu wa OHCHR kumekuwa na maendeleo mengi yaliyopatikana kwa bidii katika haki za binadamu katika miongo miwili iliyopita hata hivyo imesisitiza kuwa haki za Waafghanistan wote zinapaswa kutetewa kwa namna yoyote ile.  

Wakati huo huo Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) kupitia mkuu wake wa shughuli na dharura, Mustapha Ben Messaoud, aliyezungumza mjini Geneva amesema,hali inaboreka kiasi Kabul.

"Wiki iliyopita, timu yetu ilienda kwenye kambi ya wakimbizi wa ndani na kuona kazi kubwa inayofanywa huko na timu za wahudumu wa afya wa UNICEF, ingawa kama ilivyoelezwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya (WHO), shughuli zimesimama katika siku chache zilizopita na tunatarajia kuanza tena operesheni hivi karibuni. Kuna uhitaji mkubwa lazima tuendelee kusaidia,"amesema Messaoud.

Kwa upande wake Shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji (IOM) limekuwa likifuatilia kwa wasiwasi mkubwa maendeleo nchini Afghanistan na matokeo mabaya kwa watu waliohamishwa na vita kwao pamoja na raia wanaohitaji msaada wa kibinadamu, katika nchi ambayo tayari imeathiriwa na majanga mbalimbali.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news