NA GODFREY NNKO
Rais wa Jamhuri ya Uganda, Mheshimiwa Yoweri Kaguta Museveni amemshukuru Rais mstaafu wa Awamu ya Nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Jakaya Kikwete kwa ujumbe mzuri unaoonyesha amekuwa akijifunza mambo mengi kwake yakiwemo masuala ya kilimo.
"Ndugu yangu, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, asante sana kwa ujumbe huu mzuri. Ninakushukuru na nikutakie mafanikio wewe na timu yako katika Mkutano ujao wa Baraza la Mapinduzi ya Kijani la Afrika (AGRF), 2021,"ameeleza Rais Museveni katika ujumbe wake aliouandika Twitter.
Ujumbe huo wa faraja kwa Mheshimiwa Dkt.Jakaya Kikwete unakuja ikiwa zimesalia siku chache Mkutano wa AGRF ufanyike mjini Nairobi, Kenya.
Mkutano huo utafanyika Septemba, mwaka huu, huku matumaini ya wengi yakiwa ni kuona mwanga mpya katika sekta ya kilimo.
Pia ushirikiano katika kubadilisha mifumo ya chakula ya bara la Afrika wakati huu wa wasiwasi unaoongezeka juu ya uhaba wa chakula Duniani kwa sababu ya kuongezeka kwa idadi ya watu, kupungua kwa ardhi na mabadiliko ya hali ya hewa.
Pia kuna matumaini ya kuona njia zilizopangwa kwa ajili ya kuokoa mifumo ya chakula iliyodhoofika katika maeneo mengi.
Wakati huo huo tunaona namna ambavyo, wadau wa kilimo barani Afrika wanahimiza serikali barani kote kushirikiana na sekta binafsi kujenga mifumo ya chakula bora ili kuziba pengo linalozidi la uzalishaji.
Hivi karibuni wakizungumza wakati wa Alliance for a Green Revoluton in Africa (AGRA) ambao ndiyo waliyoandaa Mkutano wa Baraza la Mapinduzi ya Kijani la Afrika (AGRF) wadau walisisitiza kuwa, usalama wa chakula hauwezi kupatikana bila serikali kuwezesha mazingira ya biashara ya kilimo kufanikiwa kwa ufanisi.