Na Dkt.Mohamed Omary Maguo
Utangulizi
Leo ninapenda kuleta kwenu wasomaji makala hii ambayo inaelezea namna umeme vijijini ulivyosaidia kukuza fursa za Elimu Huria na Masafa nchini Tanzania.
Kabla sijaanza kutoa maelezo napenda kutambulisha kwenu msamiati 'UMEMESHAJI VIJIJINI' ikiwa na maana ya Rural Electrification.
Msamiati huu umekuja baada ya makala yangu ya kwanza juu ya UMEME VIJIJINI WAFUNGUA FURSA ZA UCHUMI KWA WANANCHI kusomwa na watu mbalimbali, mmoja wa wasomaji anayefahamika kwa jina la Prof. Abdulazizi Lodhi mtaalamu wa taaluma za lugha ikiwemo Kiswahili ni Mtanzania na kwa sasa yupo nchini Sweeden akifunza Kiswahili.
Pia, huwa anafunza katika Vyuo Vikuu kadhaa ikiwemo SUZA anapofunza wanafunzi wa Uzamili na Uzamivu katika Kiswahili.
Mtaalamu huyu alisoma makala hayo na kupendekeza misamiati kama "Umemesho Vijijini" utumike kurejelea upatikanaji wa Umeme Vijijini na ndiposa tukaita "Umemeshaji Vijini." Karibu usome makala.
Katika makala yangu juu ya Umeme Vijijini na uzalishaji wa ajira na kazi bila ukomo nilieleza mengi na nikatoa ahadi ya kueleza namna upatikanaji wa umeme vijijini unavyofungua fursa za elimu huria na masafa kwa wananchi wa maeneo hayo. Karibu usome makala.
KIINI CHA MAKALA
Chuo Kikuu Huria cha Tanzania ni Taasisi ya Elimu ya Juu ya Umma ambayo imepewa ithibati ya kutoa elimu ya juu kwa njia ya Huria na Masafa tangu mwaka 1992 kwa Sheria ya Bunge namba 17 ya mwaka huo.
Tangu mwaka huo, chuo kimekuwa kikifundisha kwa kutumia masafa kwa kuchapisha vitabu na kuwapatia wanafunzi ili wajisomee huko huko walipo.
Hili limefanyika kwa miaka kadhaa na taratibu chuo kimeendelea kubuni namna ya kurahisisha upatikanaji wa nyenzo za ufundishaji na ujifunzaji za kisasa kama vile kuandaa mihadhara katika CD,Audio, Video, Power Point,ZOOM, lectures, Whatsapp, Kimbwete,Telegram,Moodle Platform na You Tube kutaja kwa uchache.
Jitihada hizi ni kwa ajili ya kuimarisha ufundishaji na ujifunzaji kwa wanafunzi wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania ili kuhakikisha kuwa tunapata wahitimu wenye ubora.
Kwa miaka mingi wanufaika wa huduma hizi wamekuwa ni wale wa mijini na wale wa Vijijini wakitumia Offline Mode au wakati mwingine hata offline ikishindikana kwa sababu kompyuta, simu janja, iPad, tabuleti walizonazo zinahitaji umeme kwa ajili ya kuchaji na umeme haukuwepo.
Hivyo ilikuwa tabu kidogo kwenda mjini kwa ajili tu ya kuchaji simu na kutumia gharama kubwa za nauli na mengine ya mjini.
Umemeshaji Vijijini umechangia kwa kiasi kikubwa kwa wanafunzi wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kutumia nyenzo zote za ujifunzaji na ufundishaji kama ilivyo kwa wale wanaoishi vijijini na hapa chini nimetoa mifano kidogo kama ifuatavyo:
MIHADHARAKWA NJIA YA ZOOM
Kwa sasa wanafunzi wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania wanapata mihadhara kutoka kwa wahadhiri kwa njia ya mtandao wa ZOOM popote pale walipo iwe mijini au vijijini.
Mwalimu anaweza kuwa yupo ofisini, nyumbani au safarini na akawafundisha wanafunzi wake bila tatizo.
Hii ni njia nzuri ambayo inatoa fursa kwa wanafunzi kuuliza maswali, kuchangia mada na hata kuongezea pale mwalimu alipoishia na wao kupata maarifa zaidi.
Hili ni darasa halisi kama yale yaliyopo kwenye vyuo vya Bweni.
Umemeshaji Vijijini umetoa fursa kwa wanafunzi wa maeneo ya Vijijini kujiendeleza katika Elimu ya Juu huko huko Vijijini.
YOU TUBE VIDEO
Mtandao wa You Tube unatumika pia katika kutoa mihadhara kwa wanafunzi wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania.
Walimu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania wamerekodi mihadhara ya masomo yao na imepakiwa katika mtandao huo na wanafunzi wanajisomea huko huko walipo.
Mwanafunzi wetu ambaye ni mkulima, mfugaji, mvuvi anaweza kuwasha You Tube yake akawa anasikiliza muhadhara wa somo fulani huku anaendelea na kazi yake.
Badala ya kusikiliza nyimbo tu muda wote, muda mwingine anasikiliza mihadhara na kuendelea kupata mihadhara.
Hili nalo limepanuka zaidi kutokana na Umemeshaji Vijijini na kwa mijini upatikanaji wa Umeme wa uhakika umefanya wanafunzi wa Chuo Kikuu Huria kupata maarifa kwa urahisi zaidi na gharama nafuu.
MOODLE PLATFORM
Huu ni mfumo wa Ujifunzaji wa Kielektroniki ambapo vitabu, makala, ripoti za tafiti, majarida, Power Point,Audio na Video juu ya zomo husika vinapatikana katika mfumo huo.
Vitu vyote hivi vimepangwa kulingana na muhtasari wa kozi (Course Outline) na mwanafunzi anaposoma anakuwa anasoma kwa mujibu wa muhtasari wa kozi.
Pia, kuna ziada ya vile ambavyo havipo kwenye muhtasari wa kozi na hapo wanafunzi wetu wanakuwa wameiva kwelikweli.
Katika mfumo huu mwalimu anapata fursa ya kuuliza maswali na wanafunzi wanajadili kila mmoja akiwa huko huko alipo.
Wanafunzi wao kwa wao juu ya swali au mada iliyowekwa na mwalimu kwenye mfumo huo.
Hii inasaidia sana katika kukuza maarifa na uelewa mpana kwa wahitimu wetu.
Umemeshaji Vijijini umeimarisha upatikanaji wa maarifa.
WHAT'S APP KIMBWETTA
Wanafunzi wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania wanatumia What's App kama Kimbwetta kwa ajili ya kufanya mijadala juu ya masomo yao.
Kimbwetta hiki kinamwezesha mwanafunzi kuchangia mada kila mara anapokuwa na nafasi ya kushiriki.
Majadiliano ya wenzake anayapata hata kama yeye hakuwa na nafasi ya kuingia kwenye mjadala wakati wenzake wanajadili.
Sambamba na hilo pia mwalimu wa somo husika anakuwa ni mmoja kati ya washiriki wa What's App Kimbwetta na anapata fursa ya kutoa ufafanuzi na kuwatoa wanafunzi katika mkwamo. Hapo maarifa na ujuzi vinaingia kwelikweli.
HITIMISHO
Umemeshaji vijijini umeshafika kwenye vijiji zaidi ya 10,000 na kubaki vijiji vichache sana anbavyo navyo siku chache zijazo vitafikiwa.
Maana yake ni kuwa watu wengi wamefikiwa na wanapata huduma kwa unafuu zaidi kama ifuatavyo:
(a) Mwanafunzi hatumii gharama kusafiri kwenda mjini kwa ajili ya kupata huduma
(b) Mwanafunzi anatumia muda mwingi kujisomea na kujifunza badala ya kuwa barabarani kufuata huduma kwenye vituo vyetu vya mijini.
(c) Mwanafunzi anapata wigo mpana wa vyanzo vya maarifa kujisomea kupitia mifumo iliyopo hapa chuoni kwa njia ya TEHAMA Kama ilivyoelezwa katika makala.
(d) Mwanafunzi haachi shughuli zake na kama ameajiriwa hakuna haja kuombaomba ruhusa na kugombana na mwajiri.
(e) Mwanafunzi ambaye ni baba au mama anasoma huku akiendelea na malezi ya watoto wake kwa uangalizi mzuri wa karibu akiwa huko huko na familia yake.
(f) Waajiriwa wanaendelea kuhudumia wananchi huku wakiendelea kusoma. Hawatoki Vijijini kwenda mjini kwa ajili ya kusoma na kutoaka kazini.
(g) Wanafunzi wanaendelea kusoma huku wakisimamia miradi yao nyumbani bila kuiacha.
Umemeshaji Vijijini hauwatoi watu vijijini kwenda mijini wanaendelea kuzalisha Mali wakiwa Vijijini na huku wanapata elimu.
Kimsingi, Umemeshaji Vijijini umefungua fursa pana zaidi ya upatikanaji wa Elimu Huria na Masafa katika jamii.
Kwa muhtasari sana nimeeleza haya kwa lengo la kuwaeleza wale wote wenye sifa za kujiunga na Chuo Kikuu Huria cha Tanzania waje wajiunge na watasoma huko huko walipo.
Pamoja na maendeleo haya yote ambayo sisi tunayaona kuwa yanaimarisha ufundishaji na ujifunzaji na si kwamba yanafuta mifumo mingine iliyokuwepo hapo awali.
Mifumo yote ipo na tunawakaribisha sana kuchangamkia fursa ya masomo ili mkuze ujuzi na maarifa kwa Maendeleo ya nchi yetu.
Makala haya ni sehemu ya Insha za Maendeleo nchini Tanzania na itatoka katika kitabu maalumu.
Tuma maombi yako Sasa dirisha lipo wazi katika Astashahada, Stashahada, Shahada za awali, Shahada za Uzamili na Uzamivu.
Unaweza kutuma maombi moja kwa moja kupitia www.out.ac.tz Au fika kituo cha karibu cha Chuo Kikuu Huria cha Tanzania ujaze fomu. Kwa maswali na ushauri andika ujumbe mfupi kupitia 0719017254
Mwandishi
Dkt. Mohamed Omary Maguo
Mwana Elimu, Mawasiliano, Masoko, Fasihi na Maendeleo.
Chuo Kikuu Huria cha Tanzania