Utawala wa Taliban utatenda ya miaka iliyopita au wamejikung'uta mavumbi?

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

Waziri wa Ulinzi wa Uingereza Ben Wallace amesema hatma ya Afghanistan baada ya vita vya miaka 20 vilivyoongozwa na Marekani imetoa taswira kuwa azimio la mataifa ya Magharibi nchini Afghanistan sasa linaonekana kuwa dhaifu na maadui wake wakuu kama vile Urusi.

Mheshimiwa Wallace ametoa kauli yake wakati maelfu ya raia wa Afghanistan wakiendelea kuikimbia nchi hiyo kwa kuhofia utawala wa Taliban.

Ripoti za karibuni zinabainisha kuwa, vita nchini Afghanistan vimegharimu mabilioni ya dola lakini licha ya hayo, kundi la Taliban sasa limechukua madaraka kuliongoza taifa hilo huku mataifa ya Magharibi yakiendelea na juhudi za kuwahamisha wafanyakazi wake pamoja na raia wengine wa Afghanistan kutoka uwanja wa ndege wa Kabul.

Wallace amesema, ana wasiwasi juu ya utawala wa Taliban na ombwe lililoachwa na mataifa ya Magharibi baada ya kuondoa vikosi vyake vya usalama.

Wallace anasema kuondoka kwa vikosi hivyo vya usalama kutafungua mwanya kwa makundi ya kigaidi kama vile al-Qaeda kupata nafasi ya kujiimarisha tena nchini humo.

Amesema, kitu kinachonitia hofu ni kwamba sasa tuna mfumo mpya wa maisha ambapo kufeli kutatua matatizo kunachukuliwa na maadui zao kama udhaifu.

"Nafahamu kuwa hauwezi kupata suluhu ya mara moja ya hali nchini Afghanistan, na tunachofanya sasa kutakuwa na athari ya kihistoria kwa miaka mengine ijayo,"amesema.

Waziri huyo wa Ulinzi wa Uingereza ameongeza kuwa, makundi ya itikadi kali duniani kote yatapata hamasa na kuwatia moyo ya kujiimarisha zaidi kufuatia ushindi wa kundi la wanamgambo la Taliban.

Wapiganaji wa Taliban wameshika doria na kuwakagua watu wanaoingia katika uwanja wa ndege wa Kabul leo Alhamisi, wakati kukiwa na wasiwasi kuwa wanawazuia raia wa taifa hilo kuondoka nchini humo.

Serikali ya Marekani imesema imeshangazwa na hatua ya Taliban ya kuwazuia watu kuondoka nchini humo licha ya kutoa ahadi ya kuwaruhusu raia wa Afghanista waliofanya kazi kwa ushirikiano na mataifa ya Magharibi na washirika wake kuondoka.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Wendy Sherman amesema, anatarajia kuwa Taliban itatimiza ahadi yao ya kuwarahusu raia wote wa Marekani pamoja na Waafghani wanaotaka kuondoka bila ya kuwawekea vikwazo vyovyote.

Maelfu ya watu wanajaribu kuikimbia nchi hiyo wakihofia utawala wa Taliban ambao awali waliitawala Afghanistan kuanzia mwaka 1996 hadi 2001 na kuweka sheria kali za Kiislam nchini humo.

Hawa ni kina nani?

Ripoti mbalimbali zinaonyesha kuwa, Taliban ilikuwa ni mojawapo ya vikundi vinavyopigana vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Afghanistan katika miaka ya 1990 baada ya iliyokuwa Umoja wa Soviet kujiondoa nchini humo.
Aidha, kikundi hicho kiliibuka tena mwaka 1994 katika eneo la Kusini mwa Afghanistan katika mji wa Kandahar.
Mwasisi wao alikuwa Mullah Mohammad Omar ambaye alikuwa Imam katika msikiti wa mjini humo, ambaye aliwaongoza wanamgambo hao mpaka alipofariki mwaka 2013.

Taliban awali ilikuwa na wanachama kutoka kilichokuwa kikundi cha wapiganaji wa Afghanistan, maarufu Mujahedeen, ambao walikuwa wakisaidiwa na Marekani wakati wakipigana na iliyokuwa Umoja wa Soviet katika miaka ya 1980.

Inaelezwa kuwa, baada ya kuondoka kwa Umoja wa Soviet kutoka Afghanistan mwaka 1989 na hatimaye kuanguka kwa serikali ya Afghanistan, nchi hiyo ilitumbukia katika vita vya wenyewe kawa wenyewe.

Taliban walipata msaada wakiahidi kurejesha utulivu na haki. Mwaka 1994, walichukua udhibiti wa mji wa Kandahar bila upinzani mkubwa na ilipofika mwaka 1996 walikuwa wameuteka mji mkuu, Kabul.

Taliban walitawala kwa kufuata tafsiri kali ya sheria za Kiislam. Mauaji ya hadharani na watu kupigwa viboko yalikuwa mambo ya kawaida, wanawake kwa kiwango kikubwa walikuwa walizuiliwa kufanya kazi au kusoma na walilazimishwa kuvaa nguo zinazowafunika mwili mzima katika maeneo ya umma.

Hata hivyo, Taliban walipiga marufuku vitabu vya nchi za Magharibi na filamu na kuharibu vitu vya utamaduni vya tamaduni nyingine, ikiwemo sanamu kubwa zenye umri wa miaka 1,500 ya dhehebu la Buddha katika bonde la kati la Bamiyan.

Picha na AP.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news