NA MWANDISHI DIRAMAKINI
Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), Keenan Kihongosi amesema wanasikitishwa na matendo yanayofanywa na Mbunge Humphrey Polepole kuhusu suala la chanjo ya virusi vya Corona.
Umoja huo umesema, tayari Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano Wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ameshasema chanjo ni hiari na maamuzi yake lazima yaheshimiwe.
“Tunapenda kumwambia Mbunge Polepole kwamba awe na nidhamu na adabu kama aliyokuwa nayo wakati wa utawala wa Awamu ya Tano.
"Nidhamu ile ile aiendeleze pia katika utawala huu wa Awamu ya Sita. Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, mijadala yake kuhusu chanjo ni bora akakaa kimya kama haitaji kuchanja, lakini sio kujificha katika kivuli cha chanjo kuipinga Serikali.
“Kamwe hatutovumilia utovu wowote wa nidhamu kwa Rais Samia na Serikali yake, sasa kuendelea kutengeneza maneno ya kejeli, dhihaka na mengine ya aina hiyo yanabeba mazingira yanayotia shaka dhamira yake aliyonayo kwa Mwenyekiti wetu na Rais wetu wa Tanzania, tunamtaka aache mara moja,"amesema.
Kihongosi ameongeza kuwa, Chama Cha Mapinduzi si chama cha harakati bali ni chama kilichojijenga katika misingi ya kutii na kuheshimu viongozi, hivyo jambo lolote la kupinga au kuendeleza mijadala ambayo Mwenyekiti wa CCM Taifa ameshaitolea maelekezo ni utovu wa nidhamu kwa chama na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi.
“Tunamuonya na tunamtaka aache mara moja kwani hatutakubali kiongozi yoyote avunje heshima ya Rais Samia Suluhu Hassan au kupinga yale aliyoyaelekeza,"amesema.