Na Tito Mselem, Mbeya
Waziri wa Madini, Doto Biteko ameiagiza Kampuni ya kuzalisha Gesi Asilia ya Kaboni Daioksaidi ya Tol Gases Limited iliyopo wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya kufuata Kanuni na Taratibu zilizowekwa na Wizara ya Madini ikiwemo Kanuni ya Uchangiaji Maendeleo kwa Jamii (Local Content), Menejimenti ya Kampuni ya Uchimbaji Madini kuwepo eneo la mgodi pamoja na kutunza taarifa za mauzo ya madini.
Waziri wa Madini Doto Biteko akikagua taarifa za mauzo katika Kampuni ya uzalishaji Gesi Asilia ya Kabon daioksaidi ya Tol Gases Limited iliyopo wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya.
Waziri Biteko amesema kuwa, marufuku kusafirisha gesi kutoka Kiwandani hapo bila kuwepo Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Mbeya, Afisa wa Takukuru, Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Rungwe, pamoja na Afisa kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa wilaya ya Rungwe ili wafunge lakiri (Seal) kwa lengo la kudhibiti udanganyifu.
Akizungumza baada ya kufanya ziara katika Kiwanda hicho, Waziri Biteko amesema kuna baadhi ya taarifa za mauzo zinazoonesha kiasi cha fedha kilichouzwa gesi hiyo hazipo kwenye kumbukumbu ya vitabu vya Kapuni hiyo ambapo ni kinyume na taratibu zilizowekwa na Wizara ya Madini.
Aidha, Waziri Biteko ameitaka Kampuni hiyo kuhakikisha Menejimenti ya Kampuni hiyo inakuwepo eneo la uzalishaji baada ya kugundua uongozi wote wa ngazi za juu upo jijini Dar es Salaam ambapo Sheria ya Madini inasema sehemu yoyote inayochimbwa madini menejimenti iwepo na takwimu zote ziwepo mgodini.
Waziri wa Madini Doto Biteko akipewa maelezo na Msimamizi Mkuu wa Kampuni ya Tol Gases Limited Freddy Sarat baada ya kufanya ziara yake katika Kiwanda hicho.
Pia, Waziri Biteko ameitaka Kampuni ya Tol Gases Limited kuhakikisha inachangia maendeleo kwa jamii katika eneo linalozunguka mgodi ili jamii ione manufaa ya Gesi iliopo katika mazingira yao.
Naye, Mkuu wa Wilaya ya Rungwe Dkt. Vicent Anney, amemshukuru Waziri Biteko kwa kufanya ziara wilayani Rungwe na kumuahidi kwamba, Ofisi yake ameyapokea maelezo ya Waziri na atahakikisha anayafanyia kazi kama alivyo elekezwa.
“Sisi kama wilaya ya Rungwe tutahakikisha tunasimamia vizuri maelekezo yako na tunakuhakikishia kwamba, hakutakuwa na urasimu wa aina yoyote, mimi nitashirikiana na watendaji wenzangu kuhakikisha serikali inakuwa na ofisi katika Kiwanda hiki ili kulinda rasilimali za nchi na kuziba uvujaji wa mapato ya Serikali,” amesema Dkt. Anney.
Vilevile, Dkt. Anney, ametoa agizo kwa Kampuni ya Tol Gases Limited kwenda ofisini kwake kwa lengo la kujadiliana ni namnagani na kiasi gani Kiwanda hicho kitachangia maendeleo kwa jamii katika Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe.
Waziri wa Madini Doto Biteko (katikati) akikagua taarifa za mauzo katika Kampuni ya uzalishaji Gesi Asilia ya Kabon daioksaidi ya Tol Gases Limited iliyopo wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya (kulia) ni Msimamizi Mkuu wa Kampuni ya Tol Gases Limited Freddy Sarat na (kushoto) ni Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Mbeya Godson Kamihanda.
Kwa upande wake, Msimamizi wa Kampuni ya Tol Gases Limited Freddy Sarat, amesema Kampuni anayoisimamia imeyapokea maelekezo yote yaliyotolewa na Waziri Biteko na kumuahidi kuyafanyia kazi maekezo yake yote.
Kampuni ya Tol Gases Limited inayojishughulisha na uchimbaji na uchakataji wa Gesi ya Kabon Daioksidi ilianzishwa mwaka 1982 na kuanza uzalishaji rasmi mwaka 2013 inauwezo wa kusafirisha gesi zaidi ya magari 300 yenye Tani 20 kila moja kwa mwezi ambayo inawateja ndani na nje ya nchi.